Nia ya Sala ya Papa Oktoba 2025:Ushirikiano kati ya dini

Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa nia ya maombi kwa mwezi wa Oktoba,akiwaalika waamini kuombea ushirikiano kati ya tamaduni mbalimbali za kidini."Dini zisitumike kama silaha au kuta,badala yake ziishi kama madaraja na unabii:kuifanya ndoto ya wema wa wote kuaminika,kusindikiza na maisha, kudumisha matumaini endelevu na kuwa chachu ya umoja katika ulimwengu uliogawanyika.Amina."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika nia ya maombi ya kila mwezi ya Papa Jumanne tarehe 30 Septemba 2025 imechapishwa Nia ya maombi ya Papa  Leo XIV,  kwa  mwezi Oktoba 2025 ambayo amejikita na mada ya : "ushirikiano kati ya tamaduni  tofauti za kidini." Katika nia hizo Baba Mtakatifu anatoa mwaliko kwa Kanisa kuombea nia hiyo katika Ujumbe wake kwa njia ya Video ya Mwezi huu, ambayo imekabidhiwa kwa Kanisa Katoliki zima kupitia Mtandao wa Maombi ya Papa Kimataifa. Katika Video hiyo inaanza kwa sauti yake kuwaalika waamini kuungana katika kusali ili waamini katika tamaduni tofauti za kidini wafanye kazi pamoja kutetea na kukuza amani, haki na udugu wa kibinadamu.

Sala ya Papa inaanza: "Bwana Yesu, Wewe, ambaye  kwa utofauti ni wa umoja na unamtazama kila mtu kwa upendo, utusaidie kujitambua kuwa ni kaka na dada, walioitwa kuishi, kusali, kufanya kazi na kuota pamoja." Papa anabainisha kwamba licha ya kuwa"ulimwengu uliojaa uzuri, pia umejeruhiwa na migawanyiko mikubwa, ambapo wakati mwingine, dini, badala ya kutuunganisha, zinakuwa sababu ya malumbano.” Kwa hiyo, anaomba kwamba "Utupe Roho wako aitakase mioyo yetu, ili tuweze kutambua kile kinachotuunganisha na, kutoka hapo, tujifunze tena jinsi ya kusikiliza na kushirikiana bila kuharibu."

Baba Mtakatifu Leo ameendelea kusali kwamba, “mifano halisi ya amani, haki na udugu katika dini itutie moyo wa kuamini kwamba, inawezekana kuishi na kufanya kazi pamoja, zaidi ya tofauti zetu. "Dini zisitumike kama silaha au kuta, badala yake ziishi kama madaraja na unabii: kuifanya ndoto ya wema wa wote kuaminika, kusindikiza na maisha, kudumisha matumaini endelevu na kuwa chachu ya umoja katika ulimwengu uliogawanyika. Amina," Papa Leo anahitimisha.

Video ya Papa

Video ya Papa ni mpango rasmi wa kimataifa wenye madhumuni ya kusambaza nia ya maombi ya kila mwezi ya Baba Mtakatifu. Inatekelezwa na Mtandao wa Maombi ya Papa Ulimwenguni Pote. Na tangu mwaka 2016, Video ya Papa imekuwa na maoni zaidi ya milioni 247 katika mitandao yote ya kijamii ya Vatican, na imetafsiriwa katika lugha zaidi ya 23, ikitangazwa kwa vyombo vya habari katika nchi 114.

Video hiyo, iliyotayarishwa na timu ya Mtandao wa Maombi ya Video ya Papa, iliyoratibiwa na Andrea Sarubbi, na iliyoundwa kwa usaidizi wa Chombo cha Habari cha Coronation, inasambazwa kwa msaada wa wakala wa La Machi na ushirikiano wa Vyombo vya Habari Vatican. Mtandao wa Maombi ya Papa Ulimwenguni ni Jumuiya ya Kipapa, yenye utume wa kuwahamasisha Wakatoliki  wote kwa njia ya sala na matendo ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanadamu na utume wa Kanisa.

30 Septemba 2025, 18:23