Papa Leo:Kutambuliwa kwa Palestina kunasaidia,lakini mazungumzo yamevunjika
Na Sebastián Sansón Ferrari – Castel Gandolfo.
Papa Leo XIV alirejea mjini Vatican siku ya Jumanne jioni 23 Septemba 2025, baada ya kukaa siku moja huko Castel Gandolfo. Hata hivyo, kabla ya kuondoka, alijibu kwa ufupi waandishi wa habari kuhusu hali ya Mashariki ya Kati. “Vatican imeunga mkono suluhisho la serikali mbili kwa miaka mingi," alikumbusha. Pia alitaja kwamba siku hiyo hiyo, alikuwa amewasiliana na Parokia ya Kikatoliki huko Gaza. Alipoulizwa kuhusu kutambuliwa kwa Palestina kama taifa, Baba Mtakatifu alisisitiza tena kwamba, Vatican ilitambua suluhisho la serikali mbili muda uliopita. Hiyo ni wazi: lazima tutafute njia inayoheshimu watu wote." Kuhusu utambuzi huo, aliongeza, "Inaweza kusaidia, lakini hivi sasa hakuna utayari wa kweli wa kusikiliza upande wa pili; mazungumzo yamevunjika." Kuhusu hali ya Gaza, alieleza: “Asante Mungu, Parokia iko sawa, ingawa uvamizi unazidi kukaribia... Mchana wa leo niliwasiliana nao.”
Kuhusu suala la uvamizi Urusi
Waandishi wa habari pia walimwuliza kuhusu uvamizi wa Urusi: "Mtu anatafuta kuongezeka. Inazidi kuwa hatari. Ninaendelea kusisitiza juu ya haja ya kuweka silaha chini, kusimamisha maendeleo ya kijeshi, na kurudi kwenye meza ya mazungumzo." Katika muktadha huo, alisisitiza kwamba "Ikiwa Ulaya ingeunganishwa kweli, naamini inaweza kufanya mengi."
Diplomasia ya Vatican: "kuwa katika mazungumzo ya mara kwa mara na mabalozi"
Alipoulizwa ikiwa silaha nyingine ni muhimu, alijibu, "Haya ni masuala ya kisiasa, ambayo pia yanaathiriwa na shinikizo la nje kwa Ulaya. Sipendi kutoa maoni." Zaidi ya hayo, Papa alijibu swali kuhusu mipango ya kidiplomasia ambayo Vatican inaweza kufanya katika miezi ijayo, na kusema, "Tuko katika mazungumzo ya mara kwa mara na mabalozi. Pia tunajaribu kuzungumza na wakuu wa nchi wanapokuja, daima kutafuta suluhisho."Baada ya mabadilishano ya maswali na majihayo, Papa Leo XIV alirejea Vatican, tayari kujiandaa na katekesi yake yak ila Jumatano.
