Papa Leo XIV:Sitisheni mapigano huko Gaza na heshimu sheria ya kibinadamu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, alipaza sauti yake ya kutaka kusitisha mapigano kutoka katika Uwanja wa Mtakatifu Petro Mjini Vatican, Jumatano tarehe 17 Septemba 2025 kuhusiana na milipuko ya mabomu ambayo imekuwa ikiukumba mji wa Gaza, na juu ya kile ambacho wanajeshi wa Israel wamekiita awamu ya mwisho ya kuangamiza eneo la Palestina kwa lengo la kuangamiza Hamas na kuwaachilia huru wale wote waliotekwa nyara, huku zaidi ya waathiriwa 100 wakiwa tayari wamethibitishwa, majengo 140 yameharibiwa, na takriban raia 370,000 waliokuwa wakikimbia.
Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu alizinduwa tena wito wa amani wakati nchi hiyo ikiendelea kuteseka: “Ninaelezea ukaribu wangu wa kina kwa watu wa Palestina huko Gaza, ambao wanaendelea kuishi kwa hofu na kuishi katika mazingira yasiyokubalika, waliohamishwa kwa nguvu - kwa mara nyingine tena - kutoka katika ardhi zao wenyewe. Mbele ya Mwenyezi Mungu, ambaye aliamuru "Usiue", na mbele ya historia yote ya mwanadamu, kila mtu daima ana hadhi isiyoweza kukiukwa, ya kuheshimiwa na kudumishwa. Ninawasilisha upya ombi langu la kusitishwa kwa mapigano, kuachiliwa kwa mateka, na suluhisho la kidiplomasia lililojadiliwa, linaloheshimu kikamilifu sheria za kimataifa za kibinadamu. Ninawaalika nyote kujumuika katika maombi yangu ya dhati ili mapambazuko ya amani na haki yatokee hivi karibuni.
Maombezi ya amani ya Mtakatifu Stanislaus Kostka
Papa pia alikuwa ameomba amani muda mfupi kabla, wakati wa salamu zake kwa waamini wa Poland. Papa Leo XIV alikumbusha kumbukumbu ya tarehe 18 Septemba ya kiliturujia ya Mtakatifu Stanislaus Kostka, Mjesuit, na kijana wa Poland aliyekuwa na umri wa miaka 18, Msimamizi nchi na vijana kwamba: "awe kielelezo na msukumo kwa vizazi vipya vya waamini katika kutafuta mapenzi ya Mungu na katika kutimiza kwa ujasiri wito wao." Kwa maombezi yake ameikabidhi Poland na amani duniani.
Asante kwa matashi memaye yenu kwa ajili ya somo wangu!
Baba Mtakatifu kabla ya kutoa Baraka, amekumbuka Somo wake kwa jina la Ubatizo Robert Francis Prevost na kutoa shukrani kwa wale ambao wameelezea matashi mema katika siku ya jina lake la siku kuu ya Mtakatifu Robert Bellarmine. Ishara nyingi zilioneshwa, ikiwa ni pamoja na moja iliyoonesha mtoto aliyeinuliwa juu ya umati na maneno: "Siku njema ya Furaha kwa somo wako !" Na vile vile wazungumzaji katika lugha mbalimbali waliosoma ambao walichukua zamu kusoma wakati wa katekesi walimpatia heri Papa Leo XIV. Papa mwenyewe alisema: “Kabla ya kuhitimisha, ningependa kuwashukuru nyote kwa kunitakia heri siku ya jina langu. Asante sana.”
