Mahujaji wa Matumaini Kutoka Urusi Wajenzi wa Kanisa la Kristo Yesu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kristo Yesu anasema Yeye ni njia, ukweli na uzima” Rej. Yn 14:6. Ni Njia: Kwani anafundisha kwamba yeye ndiye njia pekee ya kwenda kwa Mungu Baba. Ukweli: Yeye ni kweli yote kuhusu Mungu, wokovu na uzima wa milele, na Neno la Mungu ni ukweli uliotimizwa katika maisha na utume wake. Uzima: Kristo Yesu anafafanua kuwa yeye ndiye chanzo cha uzima wa milele. Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Huu ni Mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, daima wakimwangalia Kristo Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha, amani na utulivu wa ndani. Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Kristo Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Yesu anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani.
Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Leo XIV, Ijumaa tarehe 17 Oktoba 2025 amekutana na kuzungumza na watu wa Mungu kutoka nchini Urusi wanaofanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma, ili kutafuta maana ya maisha, kupitia katika Malango ya Makanisa makuu ya Roma, ili kusali katika makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, Mashuhuda wa Injili, ili kujichotea imani, matumaini na mapendo katika hija ya maisha ya kiroho. Kwa hakika mji wa Roma kwa sasa umefurika na mahujaji wa matumaini, hawa ni waamini wanaoshuhudia imani ambayo imetangazwa na kushuhudiwa na watakatifu na mashuhuda wa imani kwa vizazi vingi. Mji wa Roma umebahatika kuwa na kumbukumbu ya ustaarabu wa zamani, makanisa na monasteri, pamoja na alama nyingi zinazogusa imani ya Kanisa na kwamba, sehemu zote hizi zinakita mizizi yake katika sakafu ya nyoyo za waamini na hivyo kuwa na uwezo ya kuhamasisha waamini kutenda mema.
Kwa hivyo anasema Baba Mtakatifu Leo XIV mji wa Roma unaweza kuwa ni ishara ya uwepo wa mwanadamu, ambamo "magofu" ya uzoefu wa zamani, dhiki, kutokuwa na hakika, na kutotulia yameunganishwa, pamoja na imani inayokua na kupyaishwa kila siku katika upendo, na kwa tumaini lisilokatisha tamaa na kututia moyo kwa sababu hata kwenye magofu, licha ya dhambi na uadui, Kristo Yesu anaweza kujenga ulimwengu mpya na maisha mapya. Majengo matakatifu ya Roma yanaibua ukweli wa kiroho: kwamba kupitia Sakramenti ya Ubatizo, sisi pia "tunatumiwa, kama mawe yaliyo hai, kujenga nyumba ya kiroho, ukuhani mtakatifu, kutoa dhabihu za kiroho zinazokubalika kwa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Rej. 1 Pet 2:5. Kila jiwe lina umuhimu wake katika ujenzi wa Kanisa na kwamba, watu wa Mungu kutoka Urusi hawana sababu ya kuogopa kama Kristo Yesu mwenyewe anavyosema: “Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni ufalme.” Lk 12:32.
Hata baada ya kuhitimisha hija ya maisha ya kiroho mjini Roma, bado watapaswa kuendeleza hija hii katika maisha ya Kikristo, huku wakiwa wameambatana na wachungaji wao, kwa kuchukuliana mizigo, ili kati yao, chemchemi ya upendo, mshikamano na udugu wa kibinadamu; kwa kuendelea kuwa ni mashuhuda katika maeneo wanamoishi, wanamofanya kazi na kusoma, ili kuwasha moto wa mapendo ya kikristo ili kupasha joto hata zile nyoyo ngumu na baridi kupindukia! Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, umetimia mwaka mmoja, tangu watu wa Mungu kutoka Urusi walipopewa Sanamu ya Bikira Maria, Afya ya Warumi: “Salus Populi Romana” kwa ajili ya Kanisa la Urusi na Hayati Baba Mtakatifu Francisko, kama kielelezo cha Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu. Hija inayofanywa na Sanamu hii kwenye majimbo mbalimbali ya Kikatoliki nchini Urusi ni faraja kwa watu wa Mungu na hasa zaidi wagonjwa na wale wanaoteseka; chemchemi ya matumaini inayowawezesha kukutana na Mwenyezi Mungu, kwa njia ya: Sala, Maandiko Matakatifu na faraja kwa wagonjwa na wale wanaoteseka. Bikira Maria Mama wa Mungu na Malkia wa amani, aendelee kuwatunza katika hija ya wito na maisha yao ya Kikristo na kwamba, anawakumbuka na kuwaombea!
