Papa,Jubilei Kimisionari:ahadi zake ni Ushirikiano na Wito wa kimisionari
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika Ibada ya Misa Takatifu ya Jubilei ya Ulimwengu wa Kimissionari na Wahamiaji, iliyofanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika ya 27 ya Mwaka C wa Kawaida, Baba Mtakatifu Leo XIV kati ya mengi aliyotafakari katika mahubiri tarehe 5 Oktoba 2025 kwa waamini na mahujaji wote 30,000 wakiwa na miavuli mvua ikinyesha, ni pamoja na kuendeleza kazi ya Kristo katika viunga vya Ulimwengu, wakati mwingine kukiwa na vita, ukosefu wa haki na mateso. Na kwa wale wanaopaza kilio kwamba Mungu yuko wapi? katika wakati huu wa giza, Papa alitoa mwaliko wa kukuza imani, sio tu inatusaidia kupinga uovu kwa kudumu katika mema, bali hubadili uwepo wetu hata kuufanya kuwa chombo cha wokovu. Hali kadhalika katika mahubiri yake Papa amekemea sintofahamu na ubaguzi wanaoupata wahamiaji wakati wa kutafuta bandari salama.
Baba Mtakatifu Leo XIV akianza mahubiri alisema: Leo tunaadhimisha Jubilei ya Ulimwengu wa Kimisionari na wa Wahamiaji. Ni fursa nzuri ya kuamsha tena mwamko wetu wa wito wetu wa kimisionari, unaozaliwa na nia ya kuleta furaha na faraja ya Injili kwa wote, hasa wale ambao maisha yao ni magumu na yenye majeraha. Nafikiria hasa kaka na dada zetu wahamiaji, ambao wamelazimika kuacha nchi zao, mara nyingi wakiwaacha wapendwa wao, wakiishi usiku wa hofu na upweke, wakipitia ubaguzi na jeuri moja kwa moja. Baba Mtakatifu kwa njia hiyo alisema: “Tuko hapa kwa sababu, kwenye kaburi la Mtume Petro, kila mmoja wetu lazima aweze kusema kwa furaha: Kanisa zima ni la kimisionari, na ni jambo la dharura—kama Baba Mtakatifu Francisko alivyosema—kwamba “liende kutangaza Injili kwa kila mtu, kila mahali, katika kila tukio, bila kusita, na bila woga” (Waraka wa Kitume, Evangelii gaudium, 23).
Roho hututuma kuendeleza kazi ya Kristo katika viunga vya ulimwengu, wakati mwingine kukiwa na vita, ukosefu wa haki, na mateso. Wakikabiliwa na matukio haya ya giza, kilio ambacho kimeinuliwa kwa Mungu mara nyingi sana katika historia kinatokea tena: Kwa nini, Bwana, usiingilie kati? Mbona unaonekana haupo? Kilio hiki cha uchungu ni aina ya maombi ambayo yameenea katika Maandiko yote Matakatifu, na asubuhi ya leo tumesikia kutoka kwa nabii Habakuki: "Ee Bwana, hata lini nitalia usinisikie [...]. Kwa nini unanifanya nione uovu, na kutazama ninavyoonewa?" (Hab 1:2-3 ).
Baba Mtakatifu akiendelea alisisitiza kwamba “Papa Benedikto wa XVI, ambaye alikuwa amejibu maswali haya wakati wa ziara yake ya kihistoria huko Auschwitz, alirejea mada katika katekesi, akisema: "Mungu yuko kimya, na ukimya huu hulia roho ya mtu anayeomba, ambaye huita bila kukoma, lakini hapati jibu. […] Mungu anaonekana kuwa mbali sana, msahaulifu, na hayupo" (Katekesi 2 Septemba). Jibu la Bwana, hata hivyo, hutufungua kuwa na matumaini. Nabii akishutumu nguvu isiyoepukika ya uovu inayoonekana kuwa na nguvu, Bwana, kwa upande wake, anatangaza kwamba haya yote yatakuwa na mwisho, tarehe ya mwisho, kwa sababu wokovu utakuja wala hautachelewa: "Tazama, mtu ambaye si mnyoofu katika nafsi yake ataanguka, lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake" ( Hab 2:4 ).
Kuna maisha, Papa aliongeza, kwa hiyo uwezekano mpya wa maisha na wokovu unaotokana na imani, kwa sababu hautusaidia tu kupinga uovu kwa kudumu katika mema, lakini hubadilisha uwepo wetu kiasi kwamba inakuwa chombo cha wokovu ambacho Mungu bado anataka kufanya kazi duniani leo. Na, kama Yesu anavyotuambia katika Injili, ni nguvu ya upole: imani haijilazimishi kwa njia zenye nguvu na kwa njia zisizo za kawaida; ni ndogo kama punje ya haradali kufanya yasiyowazika (Lk 17:6), kwa sababu inabeba ndani yake nguvu ya upendo wa Mungu ambayo hufungua njia za wokovu.
Ni wokovu unaokuja pale tunapojitoa binafsi na kujali, kwa huruma ya Injili, kwa mateso ya jirani yetu; ni wokovu unaofanya njia yake, kuwa kimya na kuonekana kutofaa, katika ishara na maneno ya kila siku, ambayo yanakuwa kama mbegu ndogo anayozungumzia Yesu; Ni wokovu unaokua polepole tunapojifanya sisi wenyewe kuwa “watumishi wasio na faida,” yaani, tunapojiweka wenyewe katika huduma ya Injili kwa kaka na dada zetu, bila kutafuta maslahi yetu wenyewe, bali tu kuleta upendo wa Bwana kwa ulimwengu. Kwa uaminifu huu, tunaitwa kufanya upya ndani yetu moto wa wito wetu wa kimisionari. Kama Mtakatifu Paulo VI alivyosema, "Ni juu yetu kutangaza Injili katika kipindi hiki kisicho cha kawaida cha historia ya mwanadamu, wakati ambao haujawahi kutokea ambamo, upana usio na kifani wa maendeleo unaambatana na kina cha kufadhaika na kukata tamaa.(Ujumbe wa Siku ya Kimisionari 25 Juni 1971).
Papa aliendelea kuwaelekea waamini wote waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kwamba, leo enzi mpya ya umisionari inafunguliwa katika historia ya Kanisa. Ikiwa kwa muda mrefu tulihusisha utume na "kuondoka," kwenda nchi za mbali ambazo hazikuwa zimeijua Injili au walikuwa katika umaskini, leo hii mipaka ya utume si ya kijiografia tena, kwa sababu umaskini, mateso, na tamaa ya tumaini kubwa zaidi ndivyo vinavyotujia. Historia za wengi wa kaka na dada zetu wahamiaji zinashuhudia hili: janga la kukimbia vurugu, mateso yanayofuatana nao, hofu ya kushindwa, hatari ya kuvuka bahari, kilio chao cha maumivu na kukata tamaa: ambapo mitumbwi ile inayotarajia kuiona bandari salama ya kusimama, na macho yale yaliyojaa dhiki na matumaini ambayo yanatafuta ardhi madhubuti ya kutua, hayawezi na hayapaswi kukutana na ubaridi wa kutojali au unyanyapaa wa ubaguzi!
Sio sana kuhusu "kuondoka," bali ni "kukaa" kumtangaza Kristo kwa njia ya ukaribisho, huruma, na mshikamano: kukaa bila kupata kimbilio katika faraja ya ubinafsi wetu, kukaa kutazama uso wa wale wanaowasili kutoka nchi za mbali na za mateso, kukaa ili kufungua mikono na mioyo yetu kwao, kuwakaribisha kama kaka na dada, kuwa uwepo wa faraja na matumaini kwao. Papa alikazia kusema kuwa kuna wamisionari wengi, lakini pia waamini na watu wenye mapenzi mema, wanaofanya kazi katika huduma ya wahamiaji na kukuza utamaduni mpya wa udugu kuhusu suala la uhamiaji, zaidi ya fikira na chuki. Lakini huduma hii ya thamani inatoa changamoto kwa kila mmoja wetu, kwa kadiri ya uwezekano wetu wenyewe: huu ndio wakati—kama Papa Francisko alivyosema—kujiimarisha katika “hali ya kudumu ya utume” ( Evangelii Gaudium, 25). Haya yote yanahitaji angalau ahadi kuu mbili za kimisionari: ushirikiano wa kimisionari na wito wa kimisionari.
Awali ya yote, nakuomba uendeleze ushirikiano mpya wa kimisionari kati ya Makanisa. Katika jumuiya zenye utamaduni wa kale wa Kikristo, kama zile za Magharibi, uwepo wa kaka na dada wengi kutoka Kusini mwa Ulimwengu lazima uchukuliwe kama fursa ya kubadilishana ambayo hufanya upya sura ya Kanisa na kuhamasisha Ukristo ulio wazi zaidi, uchangamfu na wenye nguvu zaidi. Wakati huohuo, kila mmisionari anayesafiri kwenda nchi nyingine anaitwa kukaa katika tamaduni anazokutana nazo kwa heshima takatifu, akielekeza kwa mema yale yote anayoyaona kuwa ni mema na mazuri, na kuwaletea unabii wa Injili. Kisha Papa alipenda kukumbuka uzuri na umuhimu wa miito ya kimisionari. Mtazamo Papa ulikuwa hasa kwa Kanisa la Ulaya kwamba: "leo kuna haja ya msukumo mpya wa kimisionari, kwa walei, watawa, na mapadre wanaotoa huduma yao katika nchi za utume, kwa ajili ya mapendekezo mapya ya ufundi stadi na mang’amuzi yanayoweza kuamsha hamu hii, hasa kwa vijana."
Baba Mtakatifu, kwa hiyo kwa upendo amewatumia baraka zake kwa mapadre wazawa wa Makanisa mahalia, kwa wamisionari, na kwa wote walio katika malezi. Kwa wahamiaji, Papa alisema: wanakaribishwa kila wakati! Bahari na majangwa waliyovuka katika Maandiko ni "mahali pa wokovu," ambapo Mungu alijifanya kuwapo ili kuokoa watu wake.” Ni matumaini ya Papa kwamba watapata uso huo wa Mungu katika wamisionari wanaokutana nao! Anawakabidhi wote kwa maombezi ya Maria, mmisionari wa kwanza wa Mwanawe, ambaye alisafiri kwa haraka kuelekea vilima vya Yuda, akiwa amembeba Yesu tumboni mwake na kujiweka kwenye huduma ya Elizabeti. Na atawategemeza, ili kila mmoja wetu aweze kuwa mshiriki katika Ufalme wa Kristo, Ufalme wa upendo, haki, na amani.
Asante sana kusoma makala hii, ikiwa unakata kubaki na masasisho zaidi, tunakualika kujiandikisha hapa: Just click here
