Papa Leo XIV atatembelea rasmi Ikulu ya Italia Oktoba 14
Vatican News
Kufuatia Mkutano wa kwanza na Rais wa Italia Bwana Sergio Mattarella mjini Vatican tarehe 6 Juni, 2025, Papa Leo XIV na Mkuu wa Nchi watakutana tena. Kama ilivyotangazwa na Ofisi ya Vyombo vya Habari Vatican, kwamba Papa atafanya ziara rasmi kwenye Ikulu ya Quirinale ya Italia Jumanne tarehe 14 Oktoba 2025. Huu utakuwa ni mkutano wa tatu kati ya Papa Leo XIV na Rais Mattarella aliyehudhuria Ibada ya Misa Takatifu ya kuadhimisha kusimikwa kwa Upapa tarehe 18 Mei 2025 na kisha kumsalimia Papa katika Kanisa kuu la Vatican mwishoni mwa maadhimisho hayo.
Siku kumi mapema, kwenye tukio la kuchaguliwa kwa Papa mnamo Mei 8, Bwana Mattarella alikuwa ametuma matashi mwema "kumtakia mema kwa bidii," akiihakikishia Jamhuri ya Italia juu ya dhamira yake "kukuza maono ya ulimwengu na kuishi pamoja kati ya watu ambao msingi wake ni amani, dhamana ya haki zisizoweza kukiukwa, adhama, na uhuru kwa watu wote." Mara ya mwisho Papa alitembelea Quirinale, Ikulu ya Italia ilikuwa mnamo tarehe 10 Juni 2017, wakati Papa Francisko alipomtembelea Rais Sergio Mattarella, aliyechaguliwa tena kwa muhula wa pili.
Katika tukio hilo, Papa wa Argentina alikutana na takriban wanafunzi 200 wa shule za msingi na sekondari kutoka maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi ya Lazio, Umbria, Abruzzo, Marche, na Emilia-Romagna. Ziara ya kwanza ya Papa katika Quirinale, ambayo mara moja ilikuwa makazi ya Mapapa, ilianza tarehe 28 Desemba 1939; Papa Pio XII alijibu mkutano rasmi huko Vatican na watawala wa Italia.
