Papa Leo XIV:hakuna historia iliyo na alama ya kukatishwa tamaa au isiyofikiwa tumaini
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Hakuna chochote cha jinsi tulivyo, hakuna kipande cha uwepo wetu ambacho ni kigeni kwake. Hata hivyo tunaweza kuhisi mbali, kupotea, au kutostahili. Upendo wa Mungu una nguvu zaidi. Mwaliko wa kusali Rozari kila siku kwa ajili ya amani duniani. Haya namengine yamo katika Tafaka ya Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Mzunguko wa Katekesi yake, Jumatano 8 Oktoba 2025 kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro, jua likiwa linawaka na kujaa waamini hadi njia ya Conciliazione, wote takribani 60,000. Lakini kabla ya hapo Papa alifanya mzunguko mkubwa kuwabariki wengi na zaidi watoto kadhaa. Pia anakaribishwa na mlio wa kengele kadhaa zinazoletwa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro na wanachama wa Chama cha Wapiga Kengele wa Reggio Emilia, ambao walipia shauku wakati Papa anawapitia. Kutoka jukwaani katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro Papa Leo XIV aliendeleza Mzunguko wa Jubilei kwenye mada "Yesu Kristo, tumaini letu." Kwa kujikita na Injili ya Luka inayosimulia historia ya wanafunzi wa Emau ambao baadaye waligundua kuwa wamezungumza na Mfufuka.
Papa alianza kusema kuwa “Leo ningependa kukualika utafakari juu ya kipengele cha kushangaza cha Ufufuko wa Kristo: unyenyekevu wake. Tukikumbuka masimulizi ya Injili tunatambua kwamba Bwana aliyefufuliwa hafanyi jambo lolote la ajabu ili kujilazimisha kwenye imani ya wanafunzi wake. Haonekani akiwa amezungukwa na majeshi ya malaika, hafanyi mambo ya ajabu, hatoi hotuba nzito ili kufichua siri za ulimwengu. Kinyume chake, anakaribia kwa busara, kama msafiri mwingine yeyote, kama mtu mwenye njaa anayeomba kushiriki mkate (taz. Lk 24:15, 41). Maria Magdalena anamkosea kama mtunza bustani (taz. Yh 20:15). Wanafunzi wa Emau wanaamini kuwa yeye ni mgeni (rej. Lk 24:18). Petro na wavuvi wengine wanafikiri yeye ni mpita njia tu (taz. Yh 21:4). Tungetarajia athari maalum, ishara za nguvu, ushahidi mwingi. Lakini Bwana hatafuti hili: anapendelea lugha ya ukaribu, ya kawaida, ya kushiriki chakula.
Papa aliendelea kusistiza kuwa, kuna ujumbe muhimu katika hili: Ufufuko sio mapinduzi ya maonesho; ni mabadiliko ya kimya ambayo hujaza kila ishara ya mwanadamu na maana. Yesu mfufuka anakula kipande cha samaki mbele ya wanafunzi wake: hii si maelezo ya kando, ni uthibitisho kwamba mwili wetu, historia yetu, mahusiano yetu si ganda la kutupwa mbali. Imekusudiwa utimilifu wa maisha. Ufufuko haumaanishi kuwa roho zinazopita, lakini kuingia katika ushirika wa ndani zaidi na Mungu na pamoja na kaka na dada zetu, katika ubinadamu uliogeuzwa na upendo.
Katika Pasaka ya Kristo, kila kitu kinaweza kuwa neema. Hata mambo ya kawaida: kula, kufanya kazi, kusubiri, kutunza nyumba, kusaidia rafiki. Ufufuko hauondoi maisha kutoka katika wakati na bidii, lakini hubadilisha maana yake na "Ladha." Kila ishara inayofanywa katika shukrani na ushirika inatazamia Ufalme wa Mungu. Hata hivyo, kuna kikwazo ambacho mara nyingi hutuzuia kutambua uwepo wa Kristo katika maisha yetu ya kila siku ambacho ni: dhana kwamba furaha lazima iwe huru kutoka katika mateso.
Wanafunzi wa Emau wanatembea kwa huzuni kwa sababu walitumainia mwisho tofauti, kwa Masiha ambaye hakujua msalaba. Ingawa wamesikia kwamba kaburi ni tupu, hawawezi kutabasamu. Lakini Yesu anatembea pamoja nao na kuwasaidia kwa subira kuelewa kwamba uchungu sio kukataliwa kwa ahadi, bali ni njia ambayo Mungu amedhihirisha kipimo cha upendo wake (rej. Lk 24:13-27).
Wakati hatimaye wameketi pamoja naye mezani na kuumega mkate, macho yao yanafumbuliwa. Wanatambua kwamba mioyo yao tayari ilikuwa inawaka, ingawa hawakujua (rej. Lk 24:28-32). Huu ndio mshangao mkubwa zaidi: kugundua kwamba chini ya majivu ya kukata tamaa na uchovu daima kuna makaa hai, yanayosubiri tu kuwashwa tena.
Papa Leo alizidi kukazia kwamba ufufuko wa Kristo unatufundisha kwamba hakuna historia iliyo na alama ya kukatishwa tamaa au dhambi ambayo haiwezi kutembelewa na tumaini. Hakuna anguko lililo dhahiri, hakuna usiku ni wa milele, hakuna jeraha lililokusudiwa kubaki wazi milele. Ingawa tunaweza kuhisi kuwa mbali, kupotea au kutostahili, hakuna umbali ambao unaweza kuzima nguvu isiyoweza kushindwa ya upendo wa Mungu. Wakati mwingine tunafikiri kwamba Bwana huja kututembelea tu katika nyakati za kutafakari au ari ya kiroho, tunapojisikia kuwa tunastahili, wakati maisha yetu yanaonekana kuwa ya utaratibu na angavu. Badala yake, Aliyefufuka yuko karibu nasi hasa katika sehemu zenye giza zaidi: katika kushindwa kwetu, katika mahusiano yetu yaliyoharibika, katika mapambano ya kila siku yanayotulemea mabegani, katika mashaka yanayotukatisha tamaa.
Hakuna kitu ambacho si kipande cha uwepo wetu na ambacho ni kigeni kwake. Leo hii, Bwana mfufuka anatembea kando ya kila mmoja wetu, tunaposafiri njia zetu, zile za kazi na kujitolea, lakini pia zile za mateso na upweke na kwa uzuri usio na kikomo, anatuomba tumruhusu aichangamshe mioyo yetu. Halazimishi kwa sauti kubwa; hataki kutambuliwa mara moja. Anangoja kwa subira wakati ambapo macho yetu yatafunguka ili kuona uso wake wa kirafiki, wenye uwezo wa kubadilisha tamaa kuwa matarajio yenye matumaini, huzuni kuwa shukrani, kujiuzulu kuwa tumaini. Aliyefufuka anatamani tu kudhihirisha uwepo wake, kuwa mwenzetu njiani na kuwasha ndani yetu uhakika kwamba maisha yake ni yenye nguvu kuliko kifo chochote.
Basi Papa kwa kuhitimisha alisema na tuombe neema ya kutambua uwepo wake mnyenyekevu na wa busara, tusitarajie maisha yasiyo na majaribu, kugundua kwamba kila maumivu, yakikaliwa na upendo, yanaweza kuwa mahali pa ushirika. Na kwa hivyo, kama wanafunzi wa Emau, sisi pia tunarudi nyumbani kwetu na mioyo ikiwaka kwa furaha. Furaha rahisi ambayo haifuti majeraha, lakini inayaangazia. Furaha inayotokana na uhakika kwamba Bwana yu hai, hutembea nasi, na hutupa uwezekano wa kuanza tena kila wakati.
Asante sana kusoma makala hii. Kama unataka kubaki na sasisho, tunakualika kujiandikisha hapa ili kupata habari za kila siku: cliccando qui
