Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, tarehe 16 Oktoba 2025 linaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwake Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, tarehe 16 Oktoba 2025 linaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwake   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Maadhimisho ya Miaka 80 ya FAO NA Siku ya Chakula Duniani 2025

Hotuba ya Papa Leo XIV: Mapambano dhidi ya baa la njaa, ili kujenga amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. FAO itoe kipaumbele cha kwanza kwa uhakika na usalama wa chakula duniani kwa kutumia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya kilimo; ili kuokoa maisha ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa, ambalo wakati mwingine linatumika kama silaha ya vita. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni chanzo kikuu cha balaa la njaa, umaskini na maafa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa: "Food and Agriculture Organzation of the United Nations"; kifupi: FAO, ni kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachopambana na tatizo la njaa duniani. Inalenga kuboresha uzalishaji na ugawaji wa mazao na vyakula duniani kwa shabaha ya kuboresha hali ya lishe ya watu duniani. FAO iliundwa tarehe 16 Oktoba 1945 mjini Québec nchini Canada, ili kuweza kufikia uhakika na usalama wa chakula kwa wote, kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Fiat panis” (Let there be bread) huakisi utume huo.  Tangu mwaka 1981 tarehe hiyo hukumbukwa kila mwaka kama "Siku ya Usalama wa Chakula Duniani." Mwaka 1951 Makao makuu yalihamishwa kwenda Roma, nchini Italia. Hadi kufikia Mwezi Oktoba 2025 FAO ilikuwa na nchi wanacahama 194 pamoja na Umoja wa Ulaya na hivyo jumla ya wanachama ni 195. FAO inajishughulisha na mambo makuu manne: FAO inawasilisha mawasiliano kati ya wataalamu kwenye uwanja wa lishe na chakula. Inaajiri wataalamu wa kilimo, biolojia, misitu, uvuvi na ufugaji. Inaendesha semina na warsha za kimataifa ambako watalaamu wanakutana na kubadilishana habari na mawazo. Tovuti ya FAO inakusanya habari husika na inatembelewa zaidi ya mara milioni kila mwezi. FAO inatuma washauri katika nchi nyingi wanaosaidia kupanga sera za kilimo. FAO inakutanisha serikali za nchi nyingi katika masuala ya lishe na kilimo. FAO inakusanya ujuzi kwa kazi ya kila siku, inaongoza au kushauri miradi elfu kadhaa ya kilimo kote duniani. Pamoja na Mradi wa Lishe Duniani inasaidia pia katika maeneo yenye njaa kwa kuleta msaada wa haraka kwa watu wasio na chakula.

Kumbukizi ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwa FAO
Kumbukizi ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwa FAO   (ANSA)

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, tarehe 16 Oktoba 2025 linaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwake sanjari na Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Usalama wa Chakula Duniani kwa Mwaka 2025 yanayonogeshwa na kauli mbiu: “Tuungane pamoja kupata Chakula Bora Kwa Maisha Bora ya Baadaye.” Sherehe hii imehudhuriwa na Baba Mtakatifu Leo XIV ambaye katika hotuba yake elekezi amegusia kuhusu: Mapambano dhidi ya baa la njaa, ili kujenga amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. FAO haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uhakika na usalama wa chakula duniani kwa kutumia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya kilimo; ili kuokoa maisha ya mamilioni ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa, ambalo wakati mwingine linatumika kama silaha ya vita. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii ni chanzo kikuu cha baa la njaa na umaskini duniani. Kuna umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu, ili kutekeleza sera na mikakati ya kuwa na uhakika na usalama wa chakula duniani, kwa kuwawezesha wanawake katika sekta ya kilimo pamoja na kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata maji safi na salama sanjari na huduma bora za afya. Kuna watu wanapoteza maisha kutokana na vita, changamoto na mwaliko wa kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki. Mwishoni ameitakia FAO kuwa ni chombo cha tuumaini ambalo halitahayarishi: Spes non confundit" Rum 5:5. Kwa hakika kila binadamu ana njaa na kiu ya: furaha, imani, matumaini na mapendo.

Papa Leo XIV akisalimiana na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa
Papa Leo XIV akisalimiana na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa   (ANSA)

Mapambano dhidi ya baa la njaa, ili kujenga amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika kipindi cha miaka 80 ya uhai wake, FAO bado inapambana na baa la njaa na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, hii ni changamoto ya wadau mbalimbali kushiriki kikamilifu ili kuwepo na uhakika wa usalama wa chakula duniani na kwamba, mtu anayeteseka kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha ni ndugu na kwamba, anapaswa kusaidiwa kwa haraka sana. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kujenga ari na moyo wa mshikamano na udugu wa kibinadamu, ili kuhakikisha kwamba, watu wanapata chakula bora na cha kutosha, ili kukuza na kudumisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baa la njaa linazidi kuongezeka kila kukicha kutokana na vita, kinzani na misigano ya kijamii; athari za mabadiliko ya tabianchi bila kusahau majanga asilia. Na matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasikitika kusema kwamba, licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, bado kuna watu milioni sabini na tatu wanasiginwa na baa la njaa sehemu mbalimbali za dunia na watu milioni elfu mbili na mia tatu wanateseka kutokana na utapiamlo pamoja na kukosa uhakika wa usalama na lishe bora. Kuna wanawake wanaoshindwa kuwapatia watoto wao lishe bora na chakula cha kutosha matokeo yake ni madhara makubwa kwa afya na makuzi kwa watoto hawa, kielelezo cha uchumi usiojali; maendeleo tenge na ugawaji wa rasilimali za dunia usio sawa na wala si endelevu. Maendeleo ya sayansi na tekenolojia yasaidie kuleta matumaini ya watu kuishi, ili kukomesha vifo, kielelezo cha ukosefu wa ushirikiano, kanuni maadili na utu wema.

Papa Leo XIV akisalimiana na wajumbe wa mkutano wa FAO 2025
Papa Leo XIV akisalimiana na wajumbe wa mkutano wa FAO 2025   (@Vatican Media)

Kuna baadhi ya watu wanatumia baa la njaa kama silaha ya vita, jambo ambalo lililaaniwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, tarehe 24 Mei 2018. Kimya kikuu cha baa la njaa kinachosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu si tu kashfa, bali ni kilio kinachopaswa kuamsha dhamiri nyofu, kwani baa la njaa linaendelea kuharibu maisha ya mwanadamu na kwamba, linahitaji kupatiwa suluhu ya haraka na ya kudumu, kwa njia ya ushirikiano na mshikamano wa wote, kwani haya ni mapambano ya wote. Kuna mamilioni ya watu wanateseka kwa baa la njaa, wakati kuna kundi la watu wachache wanaokula na kusaza, kiasi cha kuhatarisha Injili ya uhai. Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika baa la njaa, umaskini na maafa makubwa, changamoto na mwaliko kwa watu wote kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani; kwa kuwafariji wale wanaoteseka kwa vita, kuna haja ya kukomesha vita, ili kukijengea kizazi cha sasa na kile kijacho amani, ustawi na maendeleo, kwa kukazia tunu msingi za maisha ya kijamii kwa kujikita katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na uhakika wa usalama wa chakula sehemu mbalimbali za dunia; watu wawe na uwezekano wa kupata rasilimali zitakazo saidia kuchochea maendeleo endelevu vijijini. Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Usalama wa Chakula Duniani kwa Mwaka 2025 yanayonogeshwa na kauli mbiu: “Tuungane pamoja kupata Chakula Bora Kwa Maisha Bora ya Baadaye.” Historia mamboleo inaacha alama ya kinzani na migawanyiko.

Kumbukizi ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwa FAO
Kumbukizi ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwa FAO   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kutumia fursa hii, kutoa mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa, kuwajibika kikamilifu, ili kuhakikisha kwamba, watu wanaosiginwa na baa la njaa wanapata chakula, kwa kuhakisha kwamba kuna kuwepo na sera na mikakati bora, kwa njia ya ushirikiano mkamilifu na wa kweli, ili kuwa na uhakika wa usalama na ubora wa chakula, kama sehemu ya haki msingi za binadamu, na wala si kielelezo cha upendeleo. Wanawake wawezeshwe ili kuhakikisha kwamba, ndani ya familia kunakuwepo na uhakika na usalama wa chakula; kwa kupandikiza mbegu ya matumaini kwa wakulima kwani wanawake wana mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya baa la njaa duniani na kwamba, kutambua mchango wa wanawake ni kitendo cha haki kinachoweza kuhakikisha kwamba, chakula bora na utu wa mwanadamu ni mambo yanayowezekana.Ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa kati ya nchi maskini zaidi duniani zinazotumainia kupewa fursa ya kuchangia ili kupata suluhu ya changamoto na matatizo yanaozikabili, kwa kuzingatia utamaduni na mapokeo hai yanayokita mizizi yake kwa hekima ya wazee. Nyuso za watu wanaoteseka kwa baa la njaa na umaskini sehemu mbalimbali za dunia anasema Baba Mtakatifu Leo XIV ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya tafakari ya kina mintarafu mitindo ya maisha yao katika ulimwengu mamboleo. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwaangalia kwa makini watu wanaoteseka kutokana na kukoswa maji safi na salama; uhakika wa usalama na chakula bora; watu wanaoteseka kwa kukosa huduma bora za afya, makazi bora; elimu ya msingi na kwamba utu, heshima na haki msingi za binadamu ndicho kipimo halisi cha heshima ya kazi.

Papa Leo akisalimiana na Mkurugenzi mkuu wa FAO
Papa Leo akisalimiana na Mkurugenzi mkuu wa FAO   (@Vatican Media)

 Kazi ni kwa ajili ya mwanadamu na wala si mwanadamu kwa ajili ya kazi na kwamba, kazi ni sehemu ya utambulisho wa mwanadamu. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kushiriki machozi na machungu ya wale wasiokuwa na fursa za ajira, wanaoishi katika hali ya umaskini na hali ya kukata tamaa. Ufumbuzi wa baa la njaa ni wajibu wa kila mtu na kwamba, kila mtu atekeleze kikamilifu wajibu wake, ili kutenda haki, ili hatimaye kwa kukazia ukweli na haki, ili kwamba, asiwepo mtu yeyote anaye achwa nyuma.Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV ameitaka FAO kuwa ni chombo cha tumaini ambalo halitahayarishi: Spes non confundit" Rum 5:5. Kwa hakika kila binadamu ana njaa na kiu ya: furaha, imani, matumaini na mapendo. Baa la njaa lina majina mengi katika uso wa nchi kwa familia kubwa ya binadamu. Kuna njaa ya imani, matumaini, na upendo ambayo lazima yaelekezwe katika mwitikio wa Jumuiya ya Kimataifa unaopaswa kutolewa kwa pamoja na jumuiya ya Kimataifa. Kile ambacho Yesu aliwaambia wanafunzi wake mbele ya umati wa wenye njaa kinasalia kuwa changamoto ya kimsingi na ya dharura kwa jumuiya ya Kimataifa: “Ninyi wapeni chakula” (Marko 6:37). Kwa mchango mdogo wa wanafunzi, Yesu alifanya muujiza mkubwa. Kwa hiyo, wasichoke kumwomba Mungu leo ​​ili awape ujasiri na nguvu za kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya haki inayotoa matokeo ya kudumu na yenye manufaa. Wanapoendelea na jitihada zao, wanaweza daima kutegemea mshikamano wa kujitolea kutoka mjini Vatican pamoja na Taasisi za Kanisa Katoliki tayari kwenda nje na kuwahudumia maskini zaidi na wasio na uwezo zaidi duniani kote.

Papa Leo XIV akizungumza na wajumbe wa FAO, Oktoba 2025
Papa Leo XIV akizungumza na wajumbe wa FAO, Oktoba 2025   (@Vatican Media)

Naye MKURUGENZI MKUU wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) Dkt. Qu Dongyu, katika hotuba yake elekezi, amewapongeza na wakushuruku viongozi wakuu wa Serikali kwa kushiriki katika tukio hili hadhimu na kwamba, maadhimisho haya ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kuhakikisha kwamba Jumuiya ya Kimataifa inakuwa na uhakika wa usalama wa chakula, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, na kwamba,  binadamu, mahitaji yake msingi na utu wake anapaswa kuwa ni kiini cha sera na mikakati ya maendeleo katika uzalishaji, lishe bora, mazingira na maisha bora. Katika kipindi cha miaka 80 tangu kuanzishwa kwa FAO kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya baa la njaa linalosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu, lakini pia bado kuna mapungufu na changamoto nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa, hasa mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini, athari za mabadiliko ya tabianchi, myumbo wa uchumi Kitaifa na Kimataifa, wadudu waharibifu na magonjwa. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kufanya kazi kwa ushirikiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa utu, heshima na haki msingi za wanawake, wanaokabiliwa na umaskini mkubwa wa hali na kipato. FAO imetumia fursa hii kuzindua Makumbusho ya Chakula na Kilim ona kwamba, chakula kinafumbata utu wa mwanadamu, matumaini na amani na kwamba, haki ya chakula inakwenda sanjari na usalama, haki na amani, changamoto na mwaliko wa kujenga utamaduni wa upendo, usawa na amani. Kumbukizi ya Miaka 80 tangu kuanzishwa kwa FAO sanjari na Maadhimisho ya Kimataifa ya Siku ya Usalama wa Chakula Duniani kwa Mwaka 2025, iwe ni fursa ya kuendeleza mapambano dhidi ya ukosefu wa uhakika na usalama wa chakula, kwa kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na chakula bora na cha kutosha kwa miaka mingine 80 ijayo, huku utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza, kama chemchemi ya matumaini kwa watu wote, bila kumwacha mtu awaye yote chuma ya maendeleo haya!

Papa Leo XIV FAO Miaka 80
16 Oktoba 2025, 15:59