Maadhimisho ya Siku ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni tarehe 19 Oktoba 2025: Ushiriki mkamilifu wa hali na mali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Maadhimisho ya Siku ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni tarehe 19 Oktoba 2025: Ushiriki mkamilifu wa hali na mali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu 

Papa Leo XIV: Maadhimisho ya Siku ya 99 ya Kimisionari Ulimwengu Kwa Mwaka 2025

Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kushiriki kikamilifu kwa hali na mali katika Maadhimisho ya Siku ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa tarehe 19 Oktoba 2025. Mchango wao wa hali na mali ni muhimu sana katika kusaidia kueneza Injili sehemu mbalimbali za dunia, kwa kusaidia kuendeleza katekesi, ujenzi wa Makanisa mapya pamoja na kusaidia kuendeleza huduma za afya, elimu, ustawi na maendeleo kwa watu wa Mungu katika nchi za kimisionari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni Dominika tarehe 19 Oktoba 2025 unanogeshwa na kauli mbiu: "Wamisionari wa Matumaini Kati ya Watu Wote," himizo ni kwa Wakristo wote waliobatizwa kuwa wajumbe wa matumaini katika Maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Ujumbe huu unakazia pamoja na mambo mengine kwamba: tumaini si hisia tu bali ni zawadi ya kukumbatiwa na waamini wote, lakini hasa wale walio katika hali ngumu ya umaskini, nyanyaso na dhuluma. Unakazia mshikamano wa Kimataifa, matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Lengo ni kupandikiza mbegu ya upendo kwa watu wote, lakini zaidi wale waliotengwa na wanaokabiliana na changamoto mamboleo: uchoyo na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka; migogoro na kinzani.

Changieni kwa hali na mali katika maadhimisho ya Siku ya Kimisionari
Changieni kwa hali na mali katika maadhimisho ya Siku ya Kimisionari   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kila mwaka Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya Kimisionari Ulimwenguni, hii ni siku ya sala kwa ajili ya kuwaombea wamisionari walionea sehemu mbalimbali za dunia, ili utume wao uweze kuzaa matunda mengi. Anasema, alipokuwa nchini Perù alihudumu kama: Padre na hatimaye kama Askofu na kwa macho yake alishuhudia jinsi waamini walivyo imarisha imani yao kwa njia ya sala na ukarimu, ulioweza kuleta mabadiliko makubwa kwa watu wa Mungu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kutoka Parokia mbalimbali duniani kushiriki kikamilifu kwa hali na mali katika Maadhimisho ya Siku ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa Dominika tarehe 19 Oktoba 2025. Mchango wao wa hali na mali ni muhimu sana katika kusaidia mchakato wa kueneza Injili sehemu mbalimbali za dunia, kwa kusaidia kuendeleza katekesi, ujenzi wa Makanisa mapya pamoja na kusaidia kuendeleza huduma za afya, elimu, ustawi na maendeleo kwa watu wa Mungu katika nchi za kimisionari.

Mchango ni muhimu katika kuendeleza huduma za afya.
Mchango ni muhimu katika kuendeleza huduma za afya.

Kauli mbiu ya Maadhimisho haya kwa Mwaka 2025 ni mwaliko kwa waamini kutafakari wito wao wa kimisionari, yaani wanaitwa na kutumwa kuwa ni: “Wamisionari wa Matumaini Kati ya Watu Wote." Huu ni mwaliko kwa waamini kujisadaka bila ya kujibakiza, ili kushiriki furaha ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu Tumaini la waja wake hadi miisho ya dunia. Tangu sasa, Baba Mtakatifu Leo XIV anawashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi, watakaomsaidia ili aweze kuwasaidia wamisionari kutekeleza dhamana na wajibu wao sehemu mbalimbali za dunia. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, katika maisha na utume wake, yanapaswa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa ushirika, kwa kuongozwa na kipaji cha ubunifu pamoja na ukakamavu, daima yakichota amana na utajiri wake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linalofumbatwa katika upendo unaotolewa kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ni mwaliko kwa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kuendelea kujipyaisha. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa linalosafiri duniani, kwa tabia yake ni la kimisionari, sababu limepata asili yake katika kutumwa na Mungu Mwana na kutumwa kwa Roho Mtakatifu, kufuatana na agizo la Mungu Baba Mwenyezi. Ad gentes, 2.

Changieni kwa hali na mali kusaidia ujenzi wa Makanisa mapya
Changieni kwa hali na mali kusaidia ujenzi wa Makanisa mapya   (don Marek Pogorzelski SVD)

Utume huu wa Kanisa unafumbatwa katika kutangaza na kushuhudia kweli za kiinjili zinazofumbatwa katika upendo wa Mungu kwa waja wake; na hivyo kushuhudiwa katika maisha na utume wa Kanisa. Si dhamana wala wajibu wa Kanisa kufanya wongofu wa shuruti, bali watu watakatifu wa Mungu wavutwe na ushuhuda wa upendo, wenye mvuto na mashiko. Baba Mtakatifu Leo XIV wakati akizungumza na wajumbe wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, tarehe 22 Mei 2025 aliwashukuru kwa kuonesha umuhimu wa huduma yao katika utume wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Siku ya 99 ya kimisionari Ulimwenguni
13 Oktoba 2025, 16:05