Kamati ya Ushauri Kitaifa Dhidi ya Michezo ya Kamari na Upatu ya Mtakatifu Yohane Paulo II: " Consulta Nazionale Antiusura" Kamati ya Ushauri Kitaifa Dhidi ya Michezo ya Kamari na Upatu ya Mtakatifu Yohane Paulo II: " Consulta Nazionale Antiusura"  (@Vatican Media)

Papa leo XIV: Madhara ya Mchezo wa Kamari na Upatu Katika Jamii

Kuna madhara makubwa yanayotokana na mchezo wa kamari na upatu, katika mfumo wa fedha. Mababa wa Kanisa wanasema, “Wale ambao shughuli zao za riba na za ubahili zinapelekea njaa na vifo vya ndugu zao katika familia wanafanya mauaji ya ndugu zao, ingawaje si moja kwa moja, na hawana budi kuhesabiwa hatia.” Rej. KKK 2269. Kumbe kuna haja kwa watu kusimama kidete katika: Kanuni maadili na utu wema, vinginevyo mwanadamu anaweza kuteseka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Michezo ya kamari na upatu ni donda ndugu linaloendelea kusababisha maafa na majanga makubwa katika maisha ya watu sehemu mbalimbali za dunia. Mchezo huu ni matokeo ya myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa, uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka. Kamari ni dhambi kubwa inayopukutisha maisha ya watu na kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na hivyo kuwa ni chachu ya rushwa, ufisadi na kizingiti kikubwa katika ustawi, maendeleo fungamani na mafao ya wengi. Unaweza kusikia kuhusu upatu toka kwa marafiki, familia ama jirani. Kwa kawaida upatu hujishuhulisha na ukusanyaji wanachama katika semina mbalimbali, katika vikao majumbani, kwa kupigiana simu, kwa kutumiana barua pepe, kwa kuweka kwenye mitandao ya kijamii, kwenye magroup ya whatsapp, na kadhalika. Kwa kawaida utaambiwa ulipe kiasi fulani ujiunge na wewe utafute wanachama wengine wengi wajiunge ili upate pesa zaidi. Ila kila mmoja avune pesa kwenye upatu ni lazima kiasi cha wanachama wapya wanaojiunga kiwe kinaongezeka bila ukomo. Kwa kutambua madhara makubwa ya michezo hii, kunako mwaka 1991 Padre Massimo Rastrelli alianzisha Mfuko wa kwanza nchini Italia, dhidi ya michezo ya kamari na upatu, kiasi cha changamoto hii kuvaliwa njuga na wadau sehemu mbali mbali za Italia. Lengo ni kujenga utamaduni wa kuwasikiliza na kuwasaidia waathirika wa michezo ya kamari na upatu; kwa kuwapatia elimu makini, sheria, kanuni na taratibu zinazoweza kuwakwamua kutoka katika hali hii sanjari na kuhakikisha kwamba, waathirika wanasaidiwa kujenga na kudumisha dhamiri nyofu, itakayowawezesha kutafuta kilicho chema, kizuri na kitakatifu katika maisha.

Michezo ya kamari na upatu ni donda ndugu katika jamii
Michezo ya kamari na upatu ni donda ndugu katika jamii   (@Vatican Media)

Katika kipindi cha miaka kadhaa Kamati ya Ushauri Kitaifa nchini Italia dhidi ya michezo ya Kamari na Upatu ya Yohane Paulo II “Consulta Nazionale Antiusura, CNA,” imeweza kuzisaidia familia nyingi kuokoa: nyumba na vitega uchumi, kiasi hata cha kuweza tena kurejesha utu na heshima yao kama binadamu.Huu ni mchango mkubwa unaopaswa kuthaminiwa na kutambuliwa na wengi. Michezo ya kamari na upatu inadhalilisha na kuua; ni ugonjwa wa zamani sana, lakini bado unaendelea kuwadhalilisha watu wengi hata katika Ulimwengu mamboleo. Kumbe, kuna haja ya kujizatiti kikamilifu ili kuzuia na kuokoa maisha ya waathirika na vitega uchumi vyao; madeni makubwa ambayo mara nyingi wanashindwa kuyalipa kwa kuwapatia elimu ya kuwa na kiasi katika maisha pamoja na kujifunza kujinyima kwani kamwe mwanadamu hawezi kupata yote katika maisha. Watu waelimishwe umuhimu wa kuzingatia sheria pasi na shuruti, kujenga na kudumisha fadhila ya uaminifu, ukweli na uwazi katika maisha ya mtu binafsi na katika taasisi mbalimbali. Kuwepo na ongezeko la watu wa kujitolea ili kuwahudumia waathirika kwa kuwasikiliza, kuwashuri na kuwaongoza ili hatimaye, kuondokana na hali inayowanyanyasa na kuwatesa katika maisha, kiasi hata cha kuwanyima furaha, amani na utulivu wa ndani!

Mwaka 1991 Padre Massimo Alianzisha Mfuko Dhiri ya Kamari na Upatu
Mwaka 1991 Padre Massimo Alianzisha Mfuko Dhiri ya Kamari na Upatu   (@VATICAN MEDIA)

Je, mtazamo wa wale wanaowadhulumu watu hadi kuwafanya watumwa uko mbali sana na Mungu? Hii ni dhambi kubwa, wakati mwingine mbaya sana, kwa sababu haiwezi kupunguzwa kuwa hesabu tu; riba inaweza kuleta shida kwa familia, inaweza kudhoofisha akili na moyo hadi kupelekea mtu kufikiria kujiua kama njia pekee ya kutoka katika mtego wa kamari na upatu. Mienendo hasi ya riba inajidhihirisha katika viwango mbalimbali. Kuna aina ya riba ambayo inaonekana kutaka kuwasaidia wale walio katika matatizo ya kifedha, lakini ambayo hujidhihirisha hivi punde kwa jinsi ilivyo: mzigo mzito. Walio hatarini zaidi hupata matokeo, kama vile wale ambao ni waathirika wa mchezo wa kamari na upatu. Hata hivyo, huathiri pia wale ambao lazima wakabiliane na nyakati ngumu, kama vile matibabu ya ajabu, gharama zisizotarajiwa zaidi ya uwezo wao na wa familia zao. Kile ambacho hapo awali kilionekana kuwa msaada kinakuwa mateso baada ya muda si mrefu.

Kamari na Upatu ni michezo yenye madhara makubwa kwa jamii, ni dhambi
Kamari na Upatu ni michezo yenye madhara makubwa kwa jamii, ni dhambi   (@VATICAN MEDIA)

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 18 Oktoba 2025 kwa Kamati ya Ushauri ya Kamari na Upatu ya Yohane Paulo II “Consulta Nazionale Antiusura, CNA.” Kuna madhara makubwa yanayotokana na mchezo wa kamari na upatu, katika mfumo wa fedha. Mababa wa Kanisa wanasema, “Wale ambao shughuli zao za riba na za ubahili zinapelekea njaa na vifo vya ndugu zao katika familia wanafanya mauaji ya ndugu zao, ingawaje si moja kwa moja, na hawana budi kuhesabiwa hatia.” Rej. KKK 2269. Kumbe kuna haja kwa watu kusimama kidete katika: Kanuni maadili na utu wema, vinginevyo mwanadamu anaweza kutumbukia katika shimo kubwa la mchezo wa kamari na upatu. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Kamati ya Ushauri ya Kamari na Upatu ya Yohane Paulo II “Consulta Nazionale Antiusura, CNA,” inajikita katika kuwarejeshea tena matumaini, wale waliokata tamaa na kupondeka moyo, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kufakari mwaliko wa Yesu kwa Zakayo Mtoza Ushuru, aliyetubu dhambi zake, akamwongokea Mungu kwa kufanya malipizi. Rej. Lk 19: 1-10. Zakayo Mtoza ushuru kwa kukutana na Kristo Yesu, akawa mtu mpya kabisa. Baba Mtakatifu Leo wa XIV anakaza kusema, ukarimu pekee ndio unaoweza kutufunulia maana ya ubinadamu wetu. Utafutaji wa faida unapotawala, wengine si watu, hawana uso tena, ni vitu tu vya kunyonywa; na hivyo tunaishia kujipoteza na nafsi zetu wenyewe. Wngofu wa ndani wa wale wanaotoa riba ni muhimu sawa na ukaribu wa wale wanaoteseka nayo.” Baba Mtakatifu mwishoni mwa hotuba yake, amewataka wajumbe wa Kamati hii, kuendelea na utume wao ambao ni halali zaidi kwani unaonesha dhamira ya Jumuiya inayoungwa mkono na wachungaji wa Kanisa, Anawaombea na kuwakabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Mathayo Mtume.

Papa Kamari na Upatu
20 Oktoba 2025, 14:55