Papa Leo XIV:Mungu atawawajibisha wasio tafuta amani au wameanzisha migogoro

Papa amehimitisha tukio la mkutanno wa Kimataifa kwa ajili ya kuombea amani duniani,ulioandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio.Wakiwa ndani ya gofu la kale Colosseum,Papa alisema:“asiyesali anatumia dini hadi kufikia kuua”.Pia alionya,“Ole wake anayeweka Mungu katika vita.

Na Angella Rwezaula – Vatican

Akiwa Chini ya Tao (Arco)la Constantine, katika kivuli cha Colosseum, ishara ya jiji la Roma na mahali pa kale sana pa mateso ya Wakristo na mauaji ya kishahidi, ambapo mkutano wa kimataifa ulioandaliwa na  Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, wenye kauli mbiu: "Thubutu Kuishi kwa Amani," maombi yaliinuliwa juu mbinguni kuomba amani duniani. Baba Mtakatifu Leo XIV alitoa  mwito alasiri tarehe 28 Oktoba 2025, katika kuhitimisha tukio la kidini linaloandaliwa kila mwaka na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio  ili kuwaleta pamoja wawakilishi wa imani za dini Ulimwenguni na kufufua ahadi ya haraka zaidi kuliko wakati wowote katika wakati huu wa machafuko ya kuungana na kufanya kazi kwa ajili ya amani. Kila mwaka kwa miaka 39, tangu mkutano wa kihistoria wa viongozi wa kidini duniani huko Assisi mnamo tarehe 27 Oktoba 1986, na Papa Yohane Paulo II.

Magofu ya kale walipouawa wakristo wa kwanza
Magofu ya kale walipouawa wakristo wa kwanza   (@Vatican Media)

Papa katika hotuba yake alianza kusema: Tumeomba amani kulingana na tamaduni zetu mbalimbali za kidini, na sasa tumekusanyika pamoja kutangaza ujumbe wa upatanisho. Migogoro ipo katika sehemu zote za maisha, lakini vita havisaidii katika kushughulika navyo au kutafuta suluhisho. Amani ni safari ya upatanisho inayoendelea. Ninawashukuru kufika hapa kuomba amani na kwa kuonesha ulimwengu jinsi sala ilivyo muhimu. Moyo wa mwanadamu lazima uwe wazi kwa amani. Ni kupitia kutafakari ndipo tunapofungua mioyo yetu, na katika sala ndipo tunapozidi kujiamini. Tunajikumbuka ili tuzidi kujiamini. Huu ni ushuhuda wetu: kutoa hazina kubwa za kiroho za kale kwa wanadamu wa kisasa. Ulimwengu una kiu ya amani. Tunahitaji enzi ya kweli na thabiti ya upatanisho ambayo inakomesha matumizi mabaya ya madaraka, maonyesho ya nguvu na kutojali utawala wa sheria. Vita vinatosha, pamoja na maumivu yote yanayosababishwa, kupitia kifo, uharibifu na uhamisho! Tukiwa tumekusanyika hapa leo, hatuonyeshi tu hamu yetu thabiti ya amani, bali pia imani yetu kwamba sala ni nguvu yenye nguvu ya upatanisho.

Wale wanaofuata dini bila maombi wana hatari ya kuitumia vibaya, hata kufikia hatua ya kuua. Sala ni harakati ya roho na ufunguzi wa moyo. Sio maneno ya kupiga kelele, kuonyesha tabia au kauli mbiu za kidini dhidi ya viumbe vya Mungu. Tuna imani kwamba sala hubadilisha mkondo wa historia. Sehemu za sala ziwe hema za kukutana, mahali pa upatanisho na mahali pa amani. Mnamo tarehe 27 Oktoba 1986, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwaalika viongozi wa kidini kutoka ulimwenguni kote kwenda Assisi kuombea amani, akiwasihi: tusije tukapingana tena, bali tusimame pamoja. Tukio hili la kihistoria liliashiria mabadiliko katika mahusiano ya kidini. Mwaka baada ya mwaka, mikutano hii ya maombi na mazungumzo imeendelea katika "roho ya Assisi," na kuunda mazingira ya urafiki miongoni mwa viongozi wa kidini na kukaribisha miito mingi ya amani.

Sala kwa ajili ya amani
Sala kwa ajili ya amani   (@Vatican Media)

Papa alisisitiza kwamba leo, inaonekana kwamba ulimwengu umeelekea upande tofauti, lakini tunakumbatia changamoto ya Assisi na ufahamu wa kazi na wajibu wetu wa pamoja kwa amani. Ni katika hilo ambapo anaishuru Jumuiya ya Mtakatifu Egidio na mashirika yote ya Kikatoliki na yasiyo ya Kikatoliki, ambayo huifanya roho hii iendelee kuwa hai, hata ikipingana na wimbi. Kwa Kanisa Katoliki, sala katika "roho ya Assisi" inategemea msingi imara uliowekwa katika Tamko  la Nostra Aetate, la Mtaguso wa Pili wa Vatican yaani, upya wa uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na dini zingine zisizo za Kikristo. Papa Leo XIV aidha alisema kuwa “leo tunasherehekea kumbukumbu ya miaka 60 ya kutangazwa kwa Tamko hili, lililofanyika tarehe 28 Oktoba 1965. Kwa pamoja tunathibitisha tena kujitolea kwetu kwa mazungumzo na udugu, ahadi inayotamaniwa na Mababa wa Mtaguso ambayo imezaa matunda mengi. Kwa maneno ya Mtaguso: "Hatuwezi kumwomba Mungu kama Baba wa wote ikiwa tunawatendea watu wengine kama wengine isipokuwa dada na kaka, kwani wote wameumbwa kwa mfano wa Mungu" (Tamko la Uhusiano wa Kanisa na Dini Zisizo za Kikristo Nostra Aetate, 5).

Waamini wote ni kaka  na dada. Na dini, kama "mama," lazima ziwatie moyo watu kutendeana kama familia, si kama maadui. Kwa maana "ubinadamu huunda lakini jumuiya moja. Hii ni kwa sababu wote hutokana na ukoo mmoja" (n. 1). Papa leo akikumbuka tukio jingine akasema kuwa “Mwaka jana(2024) mlipokutana huko Paris, Papa Francisko aliwaandikia, akisema: "Lazima tuzuie dini zisikubali kushindwa na kishawishi cha kuwa njia ya kuchochea aina za utaifa, ukabila na ufuasi. Vita huongezeka tu. Ole wao wanaojaribu kumvuta Mungu katika upande wa vita!" na kwa njia hiyo “Ningependa kuyafanya maneno haya kuwa yangu na kuyarudia kwa uthabiti: vita si takatifu kamwe; amani pekee ndiyo takatifu, kwa sababu inakusudiwa na Mungu! Kwa nguvu ya maombi, huku mikono ikiwa imeinuliwa mbinguni na wazi kwa wengine, lazima tuhakikishe kwamba kipindi hiki cha historia, kilicho na alama ya vita na kiburi cha mamlaka, kinafikia mwisho hivi karibuni, na kusababisha enzi mpya. Hatuwezi kuruhusu kipindi hiki kuendelea. Kinaunda akili za watu wanaozoea vita kama sehemu ya kawaida ya historia ya mwanadamu. Inatosha! Hiki ni kilio cha maskini na kilio cha dunia. Inatosha! Bwana, sikia kilio chetu!”

Sala kwa ajili ya amani
Sala kwa ajili ya amani   (@Vatican Media)

Giorgio La Pira, shahidi wa amani, alimwandikia Mtakatifu Paulo VI alipokuwa akihudumu katika siasa wakati wa changamoto kwamba: "Tunatamani enzi tofauti ya historia ya dunia: enzi ya mazungumzo, enzi ya ulimwengu mpya bila vita." Leo, zaidi ya hapo awali, maneno haya yanaweza kutumika kama mwongozo kwa ubinadamu. Utamaduni wa upatanisho utashinda utandawazi wa sasa wa ukosefu wa nguvu, ambao unaonekana kutuambia kwamba enzi nyingine haiwezekani. Ndiyo, mazungumzo na ushirikiano vina uwezo wa kushughulikia na kutatua mivutano inayojitokeza katika hali za migogoro. Lazima wafanye hivyo! Mabaraza na watu muhimu wapo. "Kukomesha vita ni wajibu mzito mbele za Mungu unaowahusu wote wanaoshikilia majukumu ya kisiasa. Amani ndiyo kipaumbele cha siasa zote. Mungu atawawajibisha wale walioshindwa kutafuta amani, au waliochochea mvutano na migogoro. Atawauliza wawajibishwe kwa siku zote, miezi na miaka ya vita." Kama viongozi wa kidini, huu ndio wito wa dhati tunaotoa kwa wale walio katika nafasi za serikali. Tunashiriki hamu ya amani kwa watu wote. Sisi ni sauti ya wale ambao hawasikilizwi na wasio na sauti.

Lazima "tuthubutu amani"! Hata kama ulimwengu utapuuza wito huu, tuna uhakika kwamba Mungu atasikia maombi yetu na kilio cha wengi wanaoteseka. Mungu anataka ulimwengu usio na vita. Atatuweka huru kutokana na uovu huu! Alihitimisha. Kuhusiana na Mkutano huu wa kuombea amani, tmwaka 2020 uliokumbwa na Uviko, tukio hilo limehama kutoka mji wa Umbrian hadi Mji wa Milele, kisha katika miaka miwili iliyopita hadi Berlin, Ujerumani  na Paris, Ufaransa. Sasa wamerudi Roma, huku ushiriki wa kwanza wa Papa Leo XIV, ambaye akiwasili katika Colosseum muda mfupi kabla ya saa 10:20 jioni masaa ya Ulaya, alikaribishwa na viongozi sita wa makanisa na jumuiya za Kikristo ambao aliingia nao katika maandamanona kujiunga na "ujumbe wa upatanisho" uliozinduliwa na washiriki wa Mkutano wa siku hizo tatu. Ombi kwa Roho Mtakatifu linafungua mkutano, huku Papa akirudia maneno yaliyosemwa kutoka katika Dirisha la Baraka siku ya kuchaguliwa kwake kuwa Kharifa wa Mtume  Petro, kuhusu hitaji la "amani isiyo na silaha, na kuponywa kwa silaha.”

Papa Leo katika sala ya Amani
Papa Leo katika sala ya Amani   (@Vatican Media)

Nyimbo, ushuhuda, na maombi vilifuatiwa kwa ajili ya nchi zilizo vitani au zilizoathiriwa na vurugu, mateso, na umaskini: Mashariki ya Kati na Ukraine, lakini pia Afghanistan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Ethiopia na Somalia, Haiti, Libya, Mexico, Myanmar, Msumbiji, Nigeria, na Yemen, ndani ya kuta za travertine za Uwanja wa Maonyesho ya Flavian wa kale, ambapo jua lisilo la kawaida la Oktoba liliaki dhahabu ya msalaba wa maandamano. Watu walitawanyika katika nafasi za kijani za uwanja wa Colosseum na kufuatilia tukio hilo kwenye skrini kubwa zilizooneshwa kwa picha za drone zenye hisia kali na nzuri sana. Kupitia picha walionekana walio vaa vilemba, kovia majoho na kanzu za rangi na mitindo mbalimbali.

Sala katika Colosseum

Maneno hayo yanatiririka mfululizo, lakini mazingira ni ya ukimya, kutafakari, na kukumbuka. Miongoni mwa miti ya misonobari na mialoni ya holm ya njia ya Mtakatifu  Gregori, milio ya ndege na sauti ya mlio wa radio za tafsiri ziliweza  kusikika. Papa alibaki ameinamisha kichwa chake katika awamu hii ya kwanza ya tukio hilo. Kisha aliinuka kufanya ishara ya amani na wawakilishi Wakristo. Pamoja nao, akiwa amezungukwa na Andrea Riccardi na Marco Impagliazzo, mwanzilishi na rais wa wa sasa wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, ambaye baadaye alimtambulisha Papa Wageni.

Sala ya Amani na Hotuba ya Papa
Sala ya Amani na Hotuba ya Papa   (@Vatican Media)

Huku kukiwa na makofi ya umati, aliwasalimia waliohudhuria mmoja baada ya mwingine; Miongoni mwao walikuwa Makardinali Matteo Zuppi, Baldo Reina, Gualtiero Bassetti, Louis Raphael Sako, Fridolin Ambongo, Antoine Kambanda, Jean-Marc Aveline, Askofu Mkuu Vincenzo Paglia, na Askofu Kilatini wa Kyiv, Vitalii Kryvytskyi. Wawakilishi wengine wa  Mageuzi na Makanisa ya Kiorthodox walikuwepo, akiwemo Antonij, mkuu wa mahusiano ya nje wa Upatriaki wa Moscow, Urusi. Pia alikuwepo Imam Mkuu wa Msikiti wa Istiqlal huko Jakarta, Nasaruddin Umar, ambaye mazungumzo yake ya upendo na Papa Francisko wakati wa ziara yake ya Septemba 2024 yanakumbukwa. Leo pia, Imam Mkuu alimkumbatia Papa na kuweka busu kwenye paji la uso wake.

Papa alitoa hotuba yake
Papa alitoa hotuba yake   (@Vatican Media)

Kusalimiana kwa kugusana kulifanyika na Koko Kondo mwenye umri wa miaka 80, ambaye alinusurika na bomu la nyuklia la Hiroshima akiwa na umri wa zaidi ya miezi sita na sasa ni shahidi wa hofu hiyo lakini pia nguvu ya amani. Kisha Papa anapanda ngazi za jukwaa la bluu na kutoka hapo, baada ya salamu ya Impagliazzo, ushuhuda wa mkimbizi wa Sudan, na sala kwa ajili ya waathiriwa wa migogoro na ugaidi, anatoa hotuba yake. Maneno yake ya kwanza ni shukrani kwa wale waliokuja Roma kuomba amani, akionyesha ulimwengu "jinsi sala ilivyo muhimu."

Papa Sala ya Amani
28 Oktoba 2025, 19:13