Papa na timu ya Sinodi:Awapongeza vikundi vyote kwa juhudi za kutembea pamoja
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV aliwakaribisha takriban wanachama elfu mbili wa timu za sinodi na vyombo shirikishi kama vile mabaraza ya wazee, mabaraza ya wachungaji, mabaraza ya kifedha, na miongoni mwa mengine wanaowakilisha tawala za kijimbo/kiaskofu, kitaifa,kikanda kwa Kanisa kutoka ulimwenguni, waliokusanyika katika Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican, Ijumaa tarehe 24 Oktoba 2025. Kwa hiyo siku hiyo iliashiria mwanzo wa hija yao ya Jubilei ya siku tatu. Mkutano wa pamoja na Papa Leo XIV uliadhimisha tukio katika wakati muhimu wa awamu ya utekelezaji wa maelekezo yaliyojitokeza katika Hati ya Mwisho wa Mkutano Mkuu wa Kawaida wa XVI wa Sinodi ya Maaskofu.
Jubilei pia ilionesha wakati wa kwanza wa pamoja wa awamu ya utekelezaji, uliolenga kutafsiri mwelekeo wa Hati ya Mwisho katika chaguzi za kichungaji na kimuundo zinazoendana na asili ya sinodi ya Kanisa. Wakati huo huo, Mkutano na Papa ulibainisha mara moja kutambua huduma ya thamani inayofanywa na makundi haya na watu wanaohudumu ndani yake, yote yakilenga kujenga Kanisa la kisinodi zaidi ndani ya upeo wa matumaini ya Jubilei.
Papa Leo XIV ambaye alikuwa kama Askofu wa Chiclayo, nchini Peru, na kisha kama Mwenyekiti wa Baraza la kipapa la Maaskofu, alihusika sana katika Sinodi kuhusu Sinodi, na alisikiliza kwa makini uwakilishi wa washiriki, waliopangwa kulingana na mabara yote. Kabla ya Papa kufika, walifanya mfululizo wa majadiliano wakiangalia kazi yao katika kukuza Kanisa la kisinodi zaidi kwa kuzingatia Jubilei inatazama kwa undani fadhila ya matumaini, kuendeleza mchakato wa utambuzi wa kiroho na kufanya maamuzi kwa kumsikiliza Roho Mtakatifu na kila mmoja.
Mchakato wa Sinodi umejikita katika "kutembea pamoja" kupitia mikusanyiko ya mara kwa mara, mazungumzo, na mashauriano ya pamoja ili kubaini maamuzi ya kichungaji na kushughulikia masuala yanayokabili jumuiya za kanisa kwa njia zinazoitikia ipasavyo miktadha ya mahali. Papa Leo alisikiliza mawasilisho kuhusu mchakato wa sinodi kutoka kwa uhalisia wa Kanisa wa mabara ya dunia. Kuhusu Afrika, alikumbuka jinsi utume ulivyo muhimu kwa kanisa la sinodi - kuwa Kanisa linalosikiliza, la kimisionari linalomshuhudia Kristo na kujenga madaraja katika tamaduni na dini mbalimbali.
Alisifu vipawa vya Afrika vya ujana, familia, na nguvu, na akahimiza Kanisa kukumbatia utofauti na kukuza amani, umoja, na utunzaji wa uumbaji, akibainisha pia kwamba kila uhalisia wa mahali lazima ueleweke, uheshimiwe, na kwamba kuna njia nyingi za kuwa Kanisa na bila kuweka mfano mmoja wa maisha ya Kanisa:
"Hasa katika tamaduni ambapo sisi Wakristo si wengi, mara nyingi tukiwa na waamini wa dini zingine, za kikanda na za kimataifa, kama vile Uislamu, changamoto zilizopo pia ni fursa nzuri. Na nadhani kile ambacho wengi wetu tumepitia katika miaka ya hivi karibuni katika maandalizi ya Sinodi na mwanzoni mwa mchakato huu mpya wa utekelezaji ni kwamba sinodi, kwa maneno yako, si kampeni. Ni njia ya kuwa kuwa Kanisa. Ni njia ya kukuza mtazamo unaoanza na kujifunza kusikilizana. Na kipaji cha kusikiliza ni kitu ambacho nadhani sote tunatambua, lakini ambacho mara nyingi kimepotea katika baadhi ya sekta za Kanisa, na kitu ambacho thamani yake naamini ni lazima tuendelee kugundua, kuanzia na kusikiliza Neno la Mungu, kusikilizana, kusikiliza hekima tunayopata kwa wanaume na wanawake, kwa wamini wa Kanisa na kwa wale wanaotafuta lakini ambao labda bado hawajawa wajume wa Kanisa na labda hawatakuwa kamwe wajumbe wa Kanisa, lakini ambao wanatafuta ukweli kikweli."
Baada ya kusikia ripoti kuhusu Oceania, Papa alielezea matumaini yake kwamba Kanisa litaendelea kukua katika ushirika kupitia roho ya sinodi. Alisisitiza hitaji la haraka la hatua madhubuti kushughulikia masuala ya kimataifa kama vile mabadiliko ya tabia nchi, umaskini, na ukosefu wa haki, akitoa wito kwa Kanisa kupaza sauti yake kwa ujasiri na kutekeleza wito wa Papa Francisko uliotolewa katika Laudato Si’ wa kujali kikamilifu uumbaji na ubinadamu.
Kuhusu Bara la Amerika, Papa Leo XIV alitambua mgawanyiko kati ya nchi na ndani ya jamii na hitaji la kisinodi, kusikiliza, na mazungumzo katika Kanisa na jamii. Kuendelea kwa malezi ya mapadre, maaskofu na walei, ni muhimu kwa mchakato huu, alibainisha, ili kudumisha maelewano na ushirika ndani ya Kanisa. Papa alisema kuwa "mara kadhaa nilipata msukumo kutokana na mchakato; nahisi msukumo kutoka katika watu wanaoishi imani yao kwa shauku. Na kuishi roho hii na tunazungumzia kuhusu hiki cha kiroho cha sinodi, lakini ni kiroho cha Injili, cha ushirika, cha kutaka kuwa Kanisa. Hivi ni vipengele vinavyoweza kututia moyo kweli kuendelea kuwa Kanisa na kujenga njia za ujumuishi, tukiwaalika wengine wengi—kila mtu—kusindikizana nasi, kutembea nasi.”
Kuhusu Mashariki ya Kati, Papa Leo XIV alibainisha jinsi eneo hilo linavyohitaji matumaini, akisifu imani, ujasiri, na uvumilivu wa Wakristo wake, wale waliobaki katika nchi zao za asili na wale walio nje ya nchi, kama ishara za kweli za uwepo wa Roho Mtakatifu. Pia alielezea shukrani zake za kina na pongezi kwa Kanisa huko Asia, akitambua uvumilivu wake katika kuishi sinodi katikati ya changamoto za lugha, kitamaduni, na kiuchumi, na ushuhuda wake wa imani katika miktadha isiyo ya Kikristo kwa kiasi kikubwa.
