2025.01.24 Kardinali  Koch,Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo. 2025.01.24 Kardinali Koch,Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo. 

Kardinali Koch:Ziara ya Papa ina nafasi ya kuimarisha imani katika Umungu wa Kristo

Jumuiya ya Wakristo mjini Türkiye-Ituruki inapomsubiri Papa Leo XIV kuadhimisha Mtaguso wa Nicea pamoja na Patriaki wa Kiekumene wa Konstantinopoli,Kardinali Kurt Koch,Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo anatumaini kwamba maadhimisho haya ya pamoja yatatoa ushuhuda wa umoja wa Wakristo.

Na Christine Seuss – Vatican.

Ziara ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV  inapokaribia kwenda Uturuki kuanzia tarehe 27 hadi 30 Novemba na baadaye kuelekea nchini Lebanon kuanzia tarehe 30 Novemba  2 Desemba 2025, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikristo, Kardinali Kurt Koch alikuwa na maoni yake,  akihojiana na mwandishi wa Habari wa Vatican.

Mtaguso wa Kwanza wa Nicea ulifanyika miaka 1,700 iliyopita. Kwa nini bado ni muhimu leo?

Ninaamini kuna sababu mbili. Kwanza, Mtaguso ilifanyika 325, wakati Ukristo ulikuwa bado haujajeruhiwa na migawanyiko mingi. Ndiyo maana Mtaguso unawahusu Wakristo wote na unaweza kuadhimishwa katika ushirika wa kiekumene. Na pili, Mtaguso ulifafanua na kuanzisha imani ya Kikristo katika Yesu Kristo kuwa Mwana wa Mungu, ambayo inashikiliwa na Wakristo wote. Kujikumbusha upya hili na kuimarisha imani yetu pamoja katika urafiki wa kiekumene ni faida kubwa ya tukio hili.

Umungu wa Kristo unabaki kuwa muhimu katika uekumene

Wakati huo, kulikuwa na mabishano juu ya asili ya umungu ya Kristo. Ni maswali gani makubwa katika Uekumene leo hii?

Swali hilo linabaki, bila shaka, kwa sababu ninaamini kwamba, pamoja na diplomasia yetu yote, tunaweza kupata tu umoja katika imani. Tunapata umoja katika imani hiyo ya kitume ambayo inakabidhiwa na kukabidhiwa kila kiungo kipya cha mwili wa Kristo katika ubatizo. Na, bila shaka, Mtaguso wa Nicea ni msingi mkuu ambao juu yake imani imeanzishwa. Na inaweza kuimarishwa upya ,  kwa sababu imani katika Umungu wa Yesu sio tu iliyotolewa, lakini bado inatiliwa shaka leo hii. Na kuiongeza upya inaonekana kwangu kuwa muhimu sana.

Mialiko mingi imetolewa kwa ajili ya kumbukumbu hii kuu, kutoka pande za Kikatoliki na Kiorthodox. Lengo lilikuwa kuwezesha ushiriki mpana iwezekanavyo. Je, unaweza kutuambia tayari ni nani tunayeweza kutarajia kuona huko na ambapo huenda hawakuweza kuthibitisha kuhudhuria kwao?

Bado hatujui ni nani hasa atakuja na nani hataki ... Kwa hivyo, sitaki kusema chochote katika suala hili, ili usieneze ripoti za uwongo. Kusudi lilikuwa kuwa na Wakristo wengi iwezekanavyo wahudhurie. Hayo pia yalikuwa matakwa ya Papa Leo XIV, na ningependa kusisitiza hilo. Tunaweza kujadili baadaye nani alikuwepo na ambaye hakuweza kufika.

'In Illo uno unum:' kauli mbiu ya Papa

Je, ni ujumbe gani ungependa kuona ukitoka katika maadhimisho haya ya Mtaguso?

Ushuhuda kwamba sisi ni wamoja katika kiini cha imani ya Kikristo. Hii pia inalingana na kauli mbiu ya kushangaza ya Papa Leo XIV, iitwayo “In Illo uno unum.” Hii ina maana kwamba sisi ni wengi, tuko tofauti, lakini sisi ni wamoja katika Yesu Kristo. Kauli mbiu hii, ambayo aliichagua kwa ajili ya Kanisa Katoliki, inatumika sawa kwa Uekumene.

Wewe mwenyewe unaweza kutazama nyuma maisha marefu ukiwa Vatican na katika Uekumene. Je, wewe binafsi unahisije kuhusu kushiriki katika maadhimisho haya muhimu?

Kwanza kabisa, ninafurahi sana kuona jinsi ambavyo tukio hili, la miaka 1,700 baada ya Mtaguso wa  Niea, linavyosonga Jumuiya yote ya Wakristo. Kumekuwa na mikutano mingi sana juu ya swala hili ... Nimefurahishwa sana na hili na ninashukuru sana kwamba Jumuiya ya Wakristo inatafakari juu ya Mtaguso huu na kufanya upya imani yake ya pamoja.

Ziara ya "huruma na mshikamano"

Baada ya Türkiye, - Ututuki, pia utatembelea Lebanon. Je, unatarajia kuona matunda gani kutoka katika ziara hii ya kwanza ya kitume ya Papa?

Bila shaka, pia ni ziara ya huruma na mshikamano na hali ngumu katika nchi hizi, katika Türkiye -Ututuki na, hasa, katika Lebanon. Ni faraja kwa Wakristo  huko Türkiye, Wakristo ni wachache. Wakati Nchini Lebanon, kuna jumuiya mbalimbali za Wakristo, na uwepo mkubwa wa Wamaronite, bila shaka, ambao wanaishi katika hali ngumu, kisiasa na kiuchumi. Kuwaimarisha na kuwatia moyo hakika ni jambo la Baba Mtakatifu. Na, bila shaka, mazungumzo ya kiekumene na mazungumzo ya kidini, mazungumzo kati ya Wakristo na Waislamu, ambayo ni muhimu sana nchini Lebanon kwa sababu rais wa huko ni Mmaronite na Waziri Mkuu ni Mwislamu.

Maoni ya Kardinali Koch kuhusu ziara ya kitume ya Papa huko Uturuki na Lebanon
25 Novemba 2025, 16:13