Papa atuma ujumbe kwa Makanisa wanaoshiriki COP30:Kazi imefanyika lakini haitoshi!
Na Angella rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV alituma Ujumbe tarehe 17 Novemba 2025, jioni masaa ya Ualaya kwa njia ya video na kwa lugha ya Kiingereza, ikiwa ni mchana nchini Brazili, kwa Makanisa maalum ya Kusini mwa Dunia, waliokusanyika katika Jumba la Makumbusho la Amazonai huko Belém katika mkutano wa kilele wa mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa COP30 ukiendelea katika jiji la Brazil katikati mwa Amazon. Papa alianza kwa kwa salama kwa Makanisa hayo huku akiungana na “sauti ya kinabii ya kaka zangu Makardinali ambao wameshiriki katika COP 30, wakiuambia ulimwengu kwa maneno na ishara kwamba eneo la Amazonia linabaki kuwa ishara hai ya uumbaji yenye hitaji la dharura la utunzaji.”
“Mlichagua matumaini na vitendo badala ya kukata tamaa, alisema Papa, “kujenga jumuiya ya kimataifa inayofanya kazi pamoja. Hii imeleta maendeleo, lakini haitoshi. Matumaini na dhamira lazima vifanyiwe upya, si kwa maneno na matarajio tu, bali pia kwa vitendo halisi.”
"Uumbaji unalia katika mafuriko, dhoruba, ukame na joto"
Papa wa Roma alisisitiza kwamba “Uumbaji unalia katika mafuriko, ukame, dhoruba na joto kali. Mtu mmoja kati ya watatu anaishi katika udhaifu mkubwa kwa sababu ya mabadiliko haya ya hali ya hewa. Kwao, mabadiliko ya hali ya hewa si tishio la mbali, na kuwapuuza watu hawa ni kukataa ubinadamu wetu wa pamoja. Bado kuna wakati wa kudumisha ongezeko la joto duniani chini ya ya Nyuzi joto 1.5°C, lakini dirisha limefungwa. Kama wasimamizi wa uumbaji wa Mungu, tumeitwa kutenda haraka, kwa imani na unabii, ili kulinda zawadi aliyotukabidhi.”
Makubaliano ya Paris chini ya Nyuzi joto 1.5°C
Papa amekumbusha jambo jengine kuwa “Makubaliano ya Paris yamesababisha maendeleo ya kweli na yanabaki kuwa chombo chetu chenye nguvu zaidi cha kuwalinda watu na sayari. Lakini lazima tuwe waaminifu: si Mkataba unaoshindwa, tunashindwa katika mwitikio wetu. Kinachoshindwa ni utashi wa kisiasa wa baadhi ya watu. Uongozi wa kweli unamaanisha huduma, na usaidizi kwa kiwango ambacho kitaleta mabadiliko makubwa. Vitendo imara vya hali ya Tabianchi, vitaunda mifumo ya kiuchumi yenye nguvu na haki. Vitendo na sera imara za Tabianchi, zote mbili ni uwekezaji katika ulimwengu wenye haki na utulivu zaidi.”
"Sisi ni walinzi wa Uumbaji
“Tunatembea pamoja na wanasayansi, viongozi na wachungaji wa kila taifa na imani. Sisi ni walinzi wa uumbaji, si wapinzani wa nyara zake. Tutume ishara wazi ya kimataifa pamoja: mataifa yamesimama katika mshikamano usioyumba nyuma ya Mkataba wa Paris na nyuma ya ushirikiano wa hali ya Tabianchi.” Kwa kuhitimisha Papa Leo XIV alisema kuwa “Jumba hili la Makumbusho la Amazonia likumbukwe kama nafasi ambapo wanadamu walichagua ushirikiano badala ya mgawanyiko na kukataa.” Na Mungu awabariki nyote katika juhudi zenu za kuendelea kutunza uumbaji wa Mungu. Kwa jina la Baba, mwana, na Roho Mtakatifu. Amina
