Papa,makaburi ya Verano:Siku ya kifo chao,walituacha,lakini tunawabeba mioyoni mwetu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika siku ambayo Mama Kanisa anakumbuka Marehemu wote, Dominika tarehe 2 Novemba 2025, Baba Mtakatifu Leo, alasiri alikwenda huko Verano jiji Roma kwenye makaburi, kuadhimisha misa Takatifu kwa ajili ya Marehemu wote, na kama alivyo kuwa tayari amesema mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana. Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake alianza kusema kuwa “wapendwa kaka na dada Tumekusanyika mahali hapa kusherehekea ukumbusho wa waamini wote waliofariki, hasa wale waliozikwa hapa na, kwa upendo maalum, wapendwa wetu. Siku ya kifo chao, walituacha, lakini huwa tunawabeba pamoja katika kumbukumbu ya mioyo yetu. Na kila siku, katika kila kitu tunachopitia, kumbukumbu hii inaendelea kuishi. Mara nyingi kuna kitu kinachotukumbusha, picha zinazorudisha kile tulichoshirikishana nao.
Sehemu nyingi, hata harufu za nyumba zetu, zinatuzungumzia kuhusu wale tuliowapenda na hawapo nasi tena na huweka kumbukumbu zao hai. Hata hivyo, leo hatupo hapa kuwakumbuka wale waliopita kutoka katika ulimwengu huu. Imani ya Kikristo, iliyojengwa juu ya Pasaka ya Kristo, inatusaidia kupata uzoefu wa kumbukumbu si tu kama ukumbusho wa yaliyopita, bali pia, na zaidi ya yote, kama tumaini la wakati ujao. Sio suala la kutazama nyuma sana, bali badala ya kutazama mbele, kuelekea lengo la safari yetu, kuelekea bandari salama ambayo Mungu ametuahidi, kuelekea sherehe isiyoisha inayotusubiri.
Huko, tukiwa tumezungukwa na Bwana Mfufuka na wapendwa wetu, tutafurahia furaha ya karamu ya milele: "Siku hiyo," tulisikia katika usomaji kutoka kwa nabii Isaya, "Bwana wa majeshi atawaandalia watu wote karamu ya chakula kingi katika mlima huu. [...] Atameza mauti milele" (Isaya 25:6, 8). "Tumaini hili la wakati ujao" linahuisha ukumbusho wetu na sala zetu siku hii. Sio udanganyifu unaotumika kutuliza maumivu ya kutengana na wapendwa, wala si matumaini tu ya kibinadamu. Ni tumaini linalotokana na ufufuko wa Yesu, ambaye alishinda kifo na kutufungulia njia ya kufikia ukamilifu wa uzima. Papa aliongeza kusema kwamba kama alivyokumbusha katika katekesi ya hivi karibuni, kuwa ndiye “hatua ya kufika kwa safari yetu. Bila upendo wake, safari ya maisha ingekuwa kutangatanga bila mwisho, kosa la kusikitisha lenye mwisho uliopotea. [...] Aliyefufuka anatuhakikishia kufika kwetu; anatuongoza nyumbani, ambapo tunasubiriwa, tunapendwa, tunaokolewa” (Katekesi Oktoba 15, 2025). Na mwisho huu wa mwisho, karamu ambayo Bwana atatukusanya, itakuwa mkutano wa upendo.
Kwa upendo, Mungu alituumba; katika upendo wa Mwanae, anatuokoa kutoka kifo; katika furaha ya upendo pamoja naye na pamoja na wapendwa wetu, anataka tuishi milele. Kwa sababu hiyo hasa, tunasafiri kuelekea lengo na kulitarajia, katika kifungo kisichoshindika na wale waliotutangulia, tu tunapoishi kwa upendo na kufanya mapenzi kwa kila mmoja wetu, hasa walio dhaifu zaidi na maskini zaidi. Yesu anatualika kwa maneno haya: "Nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula, nilikuwa na kiu nanyi mkanipa kinywaji, nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha, nilikuwa uchi nanyi mkanivika, nilikuwa mgonjwa nanyi mkanitembelea, nilikuwa gerezani nanyi mkanijia" (Mt 25:35-36).
“Upendo hushinda kifo. Katika upendo, Mungu atatukusanya pamoja na wapendwa wetu. Na tukitembea katika upendo, maisha yetu yanakuwa sala inayotuinua na kutuunganisha na marehemu, ikituleta karibu nao, tunaposubiri kukutana nao tena katika furaha ya milele. Papa aliendelea kusema kuwa huku maumivu ya kutokuwepo kwa wale ambao hawako tena miongoni mwetu yakibaki yamechorwa mioyoni mwetu, hebu tujiaminishe kwa tumaini lisilokatisha tamaa (Rm 5:5). Tumtazame Kristo Mfufuka na kuwafikiria wapendwa wetu waliofariki kana kwamba wamefunikwa na nuru yake; hebu turuhusu ahadi ya Bwana ya uzima wa milele iingie ndani yetu.
Papa aliendelea kuse akuwa Ataondoa kifo milele. Amekishinda milele kwa kufungua njia ya uzima wa milele, yaani, kwa kusherehekea Pasaka, katika handaki la kifo, ili, tukiwa tumeungana Naye, tuweze pia kuingia na kupita humo. Anatusubiri, na tutakapokutana naye mwishoni mwa maisha haya ya kidunia, tutafurahi pamoja naye na pamoja na wapendwa wetu waliotutangulia. Ahadi hii itutegemeze, ikaushe machozi yetu, na ielekeze macho yetu mbele, kuelekea tumaini hilo la baadaye ambalo halishindwi kamwe. Misa alihitimisha kwa sala na kuwabariki kwa maji ya baraka na baraka yake.
