Papa kwa Jubilei ya Ulimwengu wa Kazi:“Kazi lazima iwe chanzo cha matumaini na maisha”
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jumamosi tarehe 8 Novemba 2025 , mara baada ya Katekesi ya Jubilei katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Leo XIV aliwakaribisha kwa washiriki wa Jubilei ya Ulimwengu wa Kazi, miongoni mwa waamini waliohudhuria. Kwa hiyo aliwahutubia wakati akizungumza lugha ya Kiitaliano na kusisitiza umuhimu wa ajira kwa kila mtu.“Kazi lazima iwe chanzo cha matumaini na maisha, ikiruhusu usemi wa ubunifu wa mtu binafsi na uwezo wake wa kufanya mema.”
“Ninawakaribisha kwa furaha washiriki katika Jubilei ya Ulimwengu wa Kazi, Shirikisho la Wataalamu wa Kujitegemea la Italia, Chama cha Ushirika cha Dedalo cha Como, na Chama cha Brindisi na Barabara za Kale. “Kwa kuongezea alisema:
“Wapendwa, kazi lazima iwe chanzo cha matumaini na maisha, ikiruhusu watu binafsi kuelezea ubunifu wao na uwezo wao wa kufanya mema.” Kwa hivyo, “ni matumaini ya kujitolea kwa pamoja kutoka katika taasisi na asasi za kiraia kuunda fursa halali za ajira zinazotoa utulivu na heshima, kuhakikisha hasa kwamba vijana wanaweza kutimiza ndoto zao na kuchangia kwa manufaa ya wote."
Hali kadhalika Papa aliendelea kuwasalimia mahujaji kutoka Majimbo makuu: Gaeta, wakifuatana na Askofu Mkuu Luigi Vari, na Brindisi-Ostuni, pamoja na Askofu Mkuu Giovanni Intini.
“Wapendwa, jumuiya zenu za majimbo zina urithi imara wa kiroho, uliojikita katika imani katika Kristo. Daima jifunzeni kutoka katika chanzo hiki kizuri na kutoka humo jifunzeni ujasiri na nguvu zinazohitajika ili kukabiliana na changamoto za jamii ya leo kwa ujasiri."
Papa aliendelea na salamu kwa washiriki katika Jubilei ya maigizo ya kihistoria ya Italia, akiwasihi kuzingatia jinsi maadili makuu ya imani ya Kikristo yanavyounda msingi wa utamaduni, sanaa, na utamaduni wa kiraia na kidini wa taifa. Pia aliwasalimu wawakilishi wa Vituo vya Italia vya Mbinu za Asili, na waamini wa Canaro, Cupello, Firenze, na Viterbo. Pia mawazo ya Papa yaliwageukia vijana, wagonjwa, na wenye ndoa wapya.
"Ni matumaini ya dhati kwamba kila mtu atarudi majumbani mwake akiwa ameimarishwa na uzoefu huu wa Jubilei na kuimarishwa katika hamu ya kufuata Injili na kutoa ushuhuda wa ujasiri".
Papa aliwakaribisha na kuwasalimu mahujaji na wageni wanaozungumza Kiingereza wanaoshiriki katika katekesi hiyo, hasa wale wanaotoka Marekani. "Salamu maalum kwa nyote mnaoshiriki katika Jubilei ya Ulimwengu wa Kazi. Katika kuomba kwamba mpate kupata ongezeko la fadhila ya matumaini wakati wa Mwaka huu wa Jubilei, ninawaomba nyote, na familia zenu zote, furaha na amani ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mungu awabariki!"
Wapoland ambao wamefika Hija za Ulimwengu wa Kazi na kwamba wana desturi ndefu nchini Poland. Msukumo wao "unatokana na mafundisho ya Mtakatifu Yohane Paulo II na Waraka wake wa Laborem Exercens, na pia kutoka kwa kazi ya Padre Mtakatifu Popiełuszko.
"Mrudi kwenye vyanzo hivi ili kukumbatia "mambo mapya," kukuza maono ya Kikristo ya kazi ya mwanadamu. Ninawabariki kwa moyo wote!"
Asante kwa kusoma makala haya. Ikiwa ungependa kuendelea kupata taarifa mpya, tafadhali jiandikishe kwa jarida letu kwa kubofya hapa: cliccando qui
