Papa Leo XIV,chakula na Maskini:Bwana uwajalie watu wanaoteseka kwa vurugu,vita na njaa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mama Kanisa akiwa anaadhimisha Dominika ya XXXIII ya Mwaka C wa Kawaida, sanjari na Siku ya Maskini Ulimwenguni 2025 na pia Jubilei ya Maskini, Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro na vile vile sala ya Malaika wa Bwana katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, alikaa mezani na wageni wapatao 1300 kutoka sehemu mbali mbali, wakiwakilisha Ulimwengu na kufurahia chakula cha mchana kilichotolewa na Familia ya Vincent.
Hata hivyo kabla ya kufika katika Ukumbi wa Paulo VI alitoa salamu kwa maskini wengine waliokula chakula katika Bustan za Vatican. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu mbele yao alisema: “Tunataka kuwashukuru waandaaji na wafadhili wote waliowezesha hili kuwezekana. Na tuombe baraka za Bwana juu ya zawadi ambazo mtapokea sasa, juu ya zawadi ya chakula, zawadi ya uzima, zawadi ya udugu, zawadi ya kuweza kushirikishana na kila mmoja.”
Baba Mtakatifu Leo XIV alibariki na kusema: “Tutumie baraka zako, Ee Bwana, na utupe zawadi unayotaka sisi sote tushiriki, zawadi ya uzima na zawadi ya imani, zawadi ya tumaini na zawadi ya upendo, upendo wa kweli, unaomimina mioyoni mwetu Ee Bwana. Ubariki mkutano wetu alasiri ya leo hii, na utufanye tukumbuke kila wakati kwamba yote tunayopokea ni zawadi kutoka kwako. Na tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.” Na hatimaye Papa aliwatakia mlo mwema, na kuondoka.
Baada ya kufika kwenye Ukumbi wa Paulo VI, Baba Mtakatifu Leo XIV, aliwasalimia wote: “Kwa furaha kubwa, tunakusanyika alasiri ya leo hii kwa chakula cha mchana, katika Siku ya Maskini, iliyotamaniwa sana na mtangulizi wetu mpendwa, Papa Francisko.” Papa aliomba apigiwe makofi kwa ajili ya Papa Francisko…”Aliendelea kusema: “Chakula hiki cha mchana tunachopokea sasa kinatolewa na Mpaji na ukarimu mkubwa wa Jumuiya ya MtakatifuVincent, (Wavincentian), ambao tuwashukuru. Na pia ni kumbukumbu ya miaka 400 tangu kuzaliwa kwa mwanzilishi wao.”
Papa alisema kuwa “Watatusindikiza, wakihudumu mezani. Ninawatakia nyote, makuhani, watawa, na walei watu wa kujitolea wanaofanya kazi ulimwenguni kote kuwasaidia watu wengi maskini na wale wanaopitia mahitaji mbalimbali. Kiukweli, tumejawa na roho hii ya shukrani na sifa katika siku hii.” Baada ya kusema hayo, Papa aliomba: “Bwana abariki zawadi tutakazopokea na abariki maisha ya kila mmoja wetu aliyepo hapa, wapendwa wetu, wanafamilia wetu, watu ambao wamefanya mengi ya kutusindikiza. Pia tuwape baraka za Bwana watu wengi wanaoteseka kutokana na vurugu, vita, na njaa; na tusherehekee siku kuu hii leo hii kwa roho ya udugu.”
“Kwa jina la Baba, la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina.”
“Bwana, tubariki na zawadi hizi tunazopokea kutoka katika mapaji yako. Ubariki maisha yetu, udugu wetu. Tusaidie sote kutembea pamoja katika upendo wako. Tunaomba hayo kwa jina la Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.” Baada ya hapo Papa aliwaalika kuanza chakula na mlo mwema...
Mara baada ya chakula
Mwishoni mwa chakula cha mchana na Maskini katika Ukumbi wa Paulo VI, awali ya hayo Papa alishukuru: “Bendi nzima, waimbaji, kila mtu, kwa muziki. Asante!” Aliwaeleza kwamba kabla ya kuondoka wangeweza kuchukua chakula na matunda nyumbani: “kuna matunda kutoka Napoli kwenye kila meza: ni matamu! Mchukue matunda nyumbani pia. Kisha mlangoni, kabla hawajaondoka, Papa alitangaza kuwa “kuna zawadi inayowasubiri kila mmoja wenu. Sawa?
Kwa njia hiyo Papa alishukuru: “Bwana kwa zawadi nyingi tulizopokea, pia kwa furaha ya kuwa hapa na familia yetu, familia nzuri, Dominika hii. Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Bwana, tunakushukuru kwa zawadi zote tulizopokea kutoka katika majaliwa yako, Wewe unayeishi na kutawala daima na milele. Amina.”
Papa aliongezea: “Tunawashukuru tena wafadhili wetu wengi, Jumuiya ya Mtakatifu Vincent, Wavincentian walio hapa, Mkuu wa Shirika, na pia Kardinali Konrad Krajewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo ambaye aliwasindikiza kila wakati.” Papa amemshukuru sana.
Kwa kuhitimisha alisema: Mungu Baba Mwenyezi awabariki nyote na awasindikize kila wakati. Na baraka zake: Kwa jina la Baba na la Mwana, na la Roho Mtakatifu, awajalie na abaki nanyi daima. Amina. Matashi mema. Dominika njema.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here
