Papa Leo XIV alitua Istanbul,kituo cha mwisho katika siku yake ya kwanza nchini Türkiye
Vatican News
Ilikuwa ni saa 1:12usiku masaa ya huko, wakati ndege ya ITA “Airbus A320” iliyombeba Papa Leo XIV ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Istanbul Atatürk. Papa Leo XIV, alikaribishwa tena alipowasili na mamlaka mahalia na watoto waliomkabidhi shada la maua meupe, na ambapo atabaki Uturuki (Türkiye) hadi Dominika Novemba 30, kabla ya kwenda nchini Lebanon hadi tarehe 2 Desemba 2025, katika ziara yake ya Kwanza ya Kitume. katika Siku yake hii ya kwanza katika nchi hii alikuwa na mikutano kadhaa na pia hotuba yake ya kwanza.
Ziara ya Kaburi la Atatürk
Ndege iliondoka saa 12:35 jioni(saa za ndani) kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ankara-Esenboğa. Kwa hiyo siku ya Papa Leo XIV katika mji mkuu wa Uturuki ilianza saa 4:22 Asubuhi (saa za ndani) kwa kutua na kukaribishwa rasmi na Waziri wa Utamaduni na Utalii wa Uturuki, Mehmet Nuri Ersoy, kabla ya kuendelea na ziara ya Kaburi la Atatürk.
Mara tu baada ya sherehe rasmi ya ukaribishwaji katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ankara Alhamisi asubuhi Novemba 27, Papa Leo XIV alitembelea Kaburi la Atatürk la jiji au Anıtkabir (kihalisi, "kaburi la ukumbusho", akiambatana na ujumbe rasmi akiwemo Waziri, Makamu wa Gavana, na Kamanda wa Kaburi hilo. Papa alisaini Kitabu cha Heshima cha Kaburi hilo na kuandika, "Ninamshukuru Mungu kwa kuweza kutembelea Türkiye, na ninaomba nchi hii na watu wake wingi wa amani na ustawi." Papa Leo XIV katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku 6 huko Türkiye na Lebanon, Ziara yake ya kwanza ya Kitume nje ya nchi. Ukumbusho huo una umuhimu mkubwa kwa Waturuki, kwani unamheshimu mwanzilishi wa Türkiye ya kisasa na unaashiria kuzaliwa kwa taifa, usasa, na udini.
Mustafa Kemal Atatürk anaheshimiwa kama "Baba wa Waturuki" kwa kuongoza Harakati ya Kitaifa ya Uturuki, kuanzisha Jamhuri ya Türkiye mnamo 1923, na kuhudumu kama rais wake wa kwanza. Mahali hapa pia ni mahali pa mwisho pa kupumzika kwa İsmet İnönü, Rais wa pili wa Türkiye, ambaye alizikwa hapo baada ya kufariki mnamo 1973. Kaburi lake linaelekea Kaburi la Atatürk, upande wa pili wa Uwanja wa Sherehe. Kuna sehemu kuu nne za Anıtkabir: Barabara ya Simba, Ukumbi wa Sherehe, Ukumbi wa Heshima (eneo la kaburi la Atatürk), na Hifadhi ya Amani inayozunguka mnara.
![]()
Papa akisaini Kitabu cha Heshima katika Kaburi la Atatürk huko AnkaraIl (@Vatican Media)
Mkutano na Rais Erdoğan
Alasiri Papa Leo XIV alikwenda katika Jumba la Urais, mahali alipopokelewa na Rais wa Jamhuri hiyo Bwana Recep Tayyip Erdoğan.
![]()
Papa Leo XIV na Rais wa Jamhuri ya Türkiye(Uturuki)Recep Tayyip Erdoğan (@Vatican Media)
Hotuba kwa Mamlaka ya Uturuki
Baada ya sherehe ya kukaribisha na mkutano wa faragha na Rais, Papa Leo alikwenda kwenye Maktaba ya Taifa, ambapo alikutana na wawakilishi wa mamlaka, asasi za kiraia, na kikundi cha kidiplomasia, na baadaye kutoa hotuba yake ya kwanza.
Papa katika Urais wa Masuala ya Kidini
Kisha Papa alihamia katika jengo la Urais wa Masuala ya Kidini (Diyanet), akikutana na rais wake, Safi Arpaguş, kwa mazungumzo mafupi.
![]()
Papa Leo XIV na Rais wa Masuala ya jumla ya Kidini Safi Arpaguş (@Vatican Media)
Kuondoka kwenda Istanbul
Na hatimaye Kituo cha mwisho kilikuwa ziara ya Ubalozi wa Vatican nchini humo. Kutoka hapo, Papa Leo XIV alisafiri hadi uwanja wa ndege wa mji mkuu. Kulikuwa na ucheleweshaji kidogo ikilinganishwa na muda uliopangwa wa kuondoka, kwa sababu Papa Leo, akitoka kwenye Ubalozi wa vatican, alipunguza mwendo ili kuwasalimia, kutokea kwenye gari lake, watu waliokusanyika mbele ya Kanisa moja la Parokia.
Asante kwa kusoma makala haya. Ukitaka kuendelea kupata taarifa mpya, tafadhali jiandikishe kwa jarida letu: cliccando qui
