Papa Leo XIV atazindua Mwaka wa masomo huko Laterano,Novemba 14
Vatican News
Ijumaa tarehe 14 Novemba 2025, asubuhi saa 5 kamili, Baba Mtakatifu Leo XIV anatarajia kuongoza hafla ya Dies Academicus yaani Ufunguzi wa Mwaka wa masomo, katika Ukumbi Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran, ikiashiria mwanzo wa mwaka wa masomo wa 2025-2026 katika "Chuo Kikuu cha Papa."
Katika taarifa kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa inabainisha kwamba "uwepo wa Baba Mtakatifu katika 'Chuo Kikuu chake' ni ishara ya umakini wake maalum kwa jumuiya ya kitaaluma ya Lateran na kujitolea kwake katika malezi jumuishi ya vizazi vipya vya wanafunzi, kwa utafiti wa kitaalimungu, kifalsafa, na kisheria, na kwa mazungumzo kati ya imani na utamaduni."
“Dies Academicus” yaani Mwaka wa masomo, kiukweli, ni fursa ya kutafakari na kukutana kati ya maprofesa, wanafunzi, na mamlaka za kikanisa na za kiraia. Hafla hiyo itafanyika mbele ya Chansela, Kardinali Baldassare Reina, Makamu wa Papa Jimbo Kuu la Roma, na Gambera Monsinyori Alfonso V. Amarante, Mamlaka za kitaaluma, na wageni wengi kutoka ulimwengu wa kikanisa na kiutamaduni.
Mara ya mwisho Papa alipotembelea Chuo Kikuu cha Lateran ilikuwa tarehe 26 Machi 2019, wakati Papa Francisko bila kutarajia aliongoza tafakari ya kiutamaduni ya Kwaresima iliyoandaliwa na Chuo Kikuu, akizingatia tafakari yake kwenye kifungu kutoka katika kitabu cha nabii Danieli.
Katika mwaka wa masomo wa 2023-2024, Chuo Kikuu cha Lateran kilikuwa na wanafunzi 1,137 na maprofesa 139. Muundo wake wa kitaaluma unajumuisha: Kitivo cha Kitaalimungu na Falsafa, Taasisi ya “Institutum Utriusque Iuris,” Kitivo cha Sheria ya Kanoni na cha Sheria za Kiraia, Taasisi ya Kichungaji ya Redemptor Hominis, Mzunguko wa mafunzo ya Sayansi ya Amani na Ushirikiano wa Kimataifa, Mzunguko wa Mafunzo ya Ikolojia na Mazingira. Utunzaji wa Nyumba Yetu ya Pamoja na Ulinzi wa Uumbaji. Zifuatao zimejumuishwa kama Taasisi za Kitivo cha Uongozi, zenye uhuru wao wa usimamizi na utawala wa kitaaluma: Taasisi ya Juu ya Kipapa ya Taalimungu ya Maadili Chuo cha Alphonsian, Taasisi ya Kipapa ya Mababa wa Kanisa Augustinianum, na Taasisi ya Kipapa ya Taalimungu ya Maisha ya Wakfu -Claretianum.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here
