Papa,wito kwa Tanzania:Kila mtu aepuke vurugu na kufuata njia ya mazungumzo
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 2 Novemba 2025, ikiwa Mama Kanisa anawakumbuka Marehemu wote, akiwageukia waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, Papa Leo XIV ameonesha wasiwasi wake kuhusu ukatili na ubaguzi dhidi ya wanawake na watoto, na mashmbulizi ya raia wasio na ulinzi nchini Sudan, lakini pia kuombea nchi ya Tanzania kutokana na kuibuka vurugu wakati na baada ya uchguzi.
Baba Mtakatifu alianza kusema:: “Kwa huzuni kubwa ninafuatilia habari za kusikitisha kutoka Sudan, hasa kutoka mji wa El Fasher, katika eneo la Darfur Kaskazini linaloteseka. Ukatili usio na ubaguzi dhidi ya wanawake na watoto, mashambulizi dhidi ya raia wasio na ulinzi, na vikwazo vikali dhidi ya hatua za kibinadamu vinasababisha mateso yasiyokubalika kwa idadi ya watu ambao tayari wamechoka na miezi kadhaa ya migogoro.”
Kwa njia hiyo Papa aliongeza“Tuombe kwamba Bwana awakaribishe marehemu, awasaidie wanaoteseka, na awaguse mioyo ya waliohusika. Ninarudia wito wangu wa dhati kwa pande zinazohusika kwa ajili ya kusitisha mapigano na kufunguliwa kwa haraka kwa njia za kibinadamu. Mwishowe, ninaalika Jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kwa uamuzi na ukarimu, kutoa msaada na kuwasaidia wale wanaofanya kazi bila kuchoka kuleta unafuu.”
Tanzania
Papa Leo XIV aligeukia upande mwingine wa Afrika Mashariki hasa Tanzania na kusema kuwa:“Pia tunaiombea Tanzania, ambapo, kufuatia uchaguzi wa kisiasa wa hivi karibuni, mapigano yalizuka na waathiriwa wengi. Ninawasihi kila mtu kuepuka aina zote za vurugu na kufuata njia ya mazungumzo.”
Papa aliendelea na salamu
Papa aliendelea kuwageukia mahujaji kuwa "Nawasalimu nyote, Warumi na mahujaji kutoka Italia na kutoka sehemu nyingi za dunia, hasa wawakilishi wa kundi la PeaceMed kutoka nchi mbalimbali za Mediterania, Chuo cha Mtakatifu Tomás" cha Lisbon, Watawa Wafanyakazi wa Brescia pamoja na kampuni ya ukumbi wa michezo ya "Uno di noi", waamini wa Manerbio, walimu wa Taasisi ya "Aurora" ya Cernusco huko Naviglio, na vijana wa Rivarolo.
Misa kwa amjili ya Marehemu
Papa alitangaza juu ya kwenda kwenye makaburi kusali: Alasiri ya leo, katika makaburi ya Verano, nitadhimisha Ekaristi kwa ajili ya marehemu wote. Kiroho, nitatembelea makaburi ya wapendwa wangu; pia nitawaombea wafu ambao hakuna anayewakumbuka. Lakini Baba yetu wa mbinguni anatujua na anatupenda kila mmoja wetu na hasahau mtu yeyote! Kwa wote, Dominika njema katika ukumbusho wa Kikristo wa marehemu wetu.
