Papa Leo XIV:Kanisa litetee maskini,amani,haki,ukweli na kukuza upendo
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV Ijimaa tarehe 21 Novemba 2025, alikutana mjini Vatican na Wajumbe kutoka Caritas Intenatinalis ambapo katika kuanza hotuba yake kwa lugha ya kiingerza alisema “Ni furaha kwangu kuwasalimu asubuhi ya leo, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Caritas Internationalis, na hasa Rais wa Caritas, Kardinali Kikuchi, Askofu Mkuu wa Tokyo. Karibuni!” Akiendelea , Papa aliwashukuru “kwa ziara yenu wakati wa Mwaka huu wa Jubilei ya Matumaini, na kwa huduma thabiti ambayo shirika lenu linaendelea kutoa kwa Kanisa lote, kwa watu kote ulimwenguni.” Papa Leo kadhalika alisema kuwa “Kuanzia kuanzishwa kwa shirika hili, Caritas Internationalis limeelezea tangazo la Kanisa kwamba “upendeleo wa Kristo ni kwa maskini, wadogo, walioachwa na waliotupwa,” (Francisko, Ujumbe kwa Washiriki katika Mkutano Mkuu wa Caritas Internationalis, 11 Mei 2023). Kwa hiyo “Hakika, maono haya yanaweza kuonekana katika Ekaristi yenyewe, ambapo Bwana "akiwa amewapenda walio wake waliokuwa duniani, aliwapenda hadi mwisho," (Yh 13:1).
Akirejea katika Hati yake ya hivi karibuni, Papa alieleza kuwa “Katika Wosia wangu wa Kitume ‘Dilexi Te,’ yaani “Nimekupenda,” Papa aliongeza “nilitafakari fumbo hili hasa: kwamba upendo tunaopokea kutoka kwa Kristo kamwe si hazina ya kibinafsi bali daima ni utume uliokabidhiwa mikononi mwetu. Upendo hututuma; upendo hutufanya watumishi; upendo hutufungua macho yetu kwa majeraha ya wengine.” Kwa njia hiyo “Caritas Internationalis kwa muda mrefu imekuwa ishara angavu ya upendo wa kimama wa Kanisa, na kwa hiyo Papa aliongeza “ ninatiwa moyo kujua kwamba mko tayari kutembea na Mrithi wa Petro katika kumtumikia kila mtu kwa heshima,” Kwa sababau “Utume wenu unarudia maono niliyoshiriki katika hotuba yangu ya kwanza kwa Kikundi cha Kidiplomasia, ambapo nilizungumzia nguzo tatu zinazounga mkono kazi ya Kanisa duniani: amani, haki, na ukweli. Nguzo hizi si maadili ya kufikirika.
Papa alisisitiza kwamba nguzo hizo “ ni kazi yao ya kila siku, kazi ya kila siku ya Caritas. Popote mnaposindikiza na familia iliyohamishwa, au kutetea haki za maskini, au kutoa moyo wa kusikiliza kwa waliosahaulika, ushuhuda wa Kanisa unakuwa wa kuaminika zaidi.” Papa alipta ushauri kwamba “ Kwa roho hii, ninawahimiza kuendelea kusindikizana na Makanisa mahalia, kuimarisha uundaji wa viongozi wa kawaida, na kulinda umoja ndani ya shirika lenu tofauti. Utume wa Kanisa hufunuliwa tu tunapotembea pamoja kama wasaidizi njiani, tukimruhusu Roho Mtakatifu kuunda matendo yetu ya huruma.”
Ni kwa mawazo haya mafupi, Papa Leo XIV alikabidhi kazi yao kwa Maria, Mama wa Maskini. Kupitia maombezi yake, na waendelee kuwa mahujaji wa matumaini na mafundi wa amani. Kwa dhati kabisa, aliwashukuru, kila mmoja wao, na watu wengi wanaowawakilisha, wale wanaofanya kazi pamoja nao. Alishukuru tena na kumuomba Bwana awabariki kwa zawadi za ujasiri, uvumilivu na furaha. Na hatimaye walisali kwa pamoja sala ya ‘Baba Yetu’....
