Papa Leo XIV:Kwa Pasaka,Njia ya Msalaba inabadilishwa kuwa Njia ya Mwanga!

Katika nyakati zetu zilizo na alama nyingi ya misalaba,tunahitaji tumaini.Kristo ndiye jibu.Alisema hayo Baba Mtakatifu leo XIV katika tafakari ya Katekesi Jumatano tarehe 5 Novemba 2025 kwa waamini na mahujaji kutoka duniani waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro.Papa alisema kuwa Pasaka ilibadilisha historia kwa sababu Kristo,kwa kufufuka,alishinda kifo na kukidhi hamu yetu ya maana.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika Mzunguko wa Katekesi ya Baba Mtakatifu kwa waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Jumatano tarehe 5 Nvemba 2025, ameendeleza  mada ya Jubilei ya "Yesu Kristo Tumaini Letu.  Ufufuko wa Kristo na Changamoto za Ulimwengu wa Leo. Papa Leo XIV alijikita na mada ya “Pasaka Hutoa Matumaini kwa Maisha ya Kila Siku.” Mara baada ya kuzungukia uwanja uliowakusanya waamini na mahujaji wapata 40,000 kutoka ulimwenguni kote ambapo awali aliwabariki watoto, huku akichukua zawadi mbalimbali kwa haraka.  Baada ya kufika kwenye jukwaa kuu, lilisomwa neno la Mungu kwa lugha mbali mbali kutoka Injili ya Mathayo 28:18-20.

Papa na mahujaji
Papa na mahujaji   (@Vatican Media)

"Yesu , baada ya kufufuka kwake, akaja, akawaambia, "Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu, na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi. Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari."

Baba Mtakatifu alianza katekesi yake kwa kusema, Wapendwa Kaka na dada, habari za Asubuhi. Karibuni nyote. Pasaka ya Yesu ni tukio ambalo si la zamani za kale, ambalo sasa limejikita katika tamaduni kama vipindi vingine vingi katika historia ya mwanadamu. Kanisa linatufundisha kuadhimisha Ufufuko kwa njia ya kisasa kila mwaka Dominika ya Pasaka na kila siku katika maadhimisho ya misa, ambapo ahadi ya Bwana aliyefufuka inatimizwa kikamilifu: "Tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata mwisho wa nyakati" (Mt 28:20). Kwa sababu hii, Fumbo la Pasaka ni jiwe kuu la maisha ya Kikristo, ambalo matukio mengine yote yanazunguka. Tunaweza kusema, basi, bila ujinga wowote au hisia, kwamba kila siku ni Pasaka. Vipi? Tunapata uzoefu mwingi tofauti saa kwa saa: maumivu, mateso, huzuni, yaliyounganishwa na furaha, mshangao, utulivu. Lakini kupitia kila hali, moyo wa mwanadamu unatamani utimilifu, fwa uraha kubwa.

Papa akibariki watoto
Papa akibariki watoto   (@Vatican Media)

Mwanafalsafa mkuu wa karne ya ishirini, Mtakatifu Teresa Benedikta wa Msalaba, kwa jina  Edith Stein, ambaye alizama kwa undani katika fumbo la mwanadamu, anatukumbusha utafutaji huu wa nguvu na wa mara kwa mara wa utimilifu. "Binadamu," anaandika, "siku zote hutamani kuwa na kipawa cha kuwa tena, ili kuweza kutumia kile ambacho wakati hutoa na kuchukua" (Finite and Eternal Being. Toward an Elevation to the Meaning of Being, Rome 1998, 387). Tumezama katika mapungufu, lakini pia tunajitahidi kuyapita. Tangazo la  Pasaka ni habari nzuri zaidi, ya furaha, na ya kushtua kuwahi kutokea katika historia yote. Ni "Injili" bora kabisa, inayothibitisha ushindi wa upendo dhidi ya dhambi na uzima dhidi ya kifo, na kwa hivyo ndiyo pekee inayoweza kukidhi utafutaji wa maana unaosumbua akili na mioyo yetu. Binadamu wanaongozwa na harakati za ndani, wakifikia kilele kinachowavutia kila mara. Hakuna ukweli unaoweza kuwaridhisha.

Papa akizungukia umati wa mahujaji
Papa akizungukia umati wa mahujaji   (@Vatican Media)

Tunajitahidi kwa ajili ya usio na mwisho na wa milele. Hii inapingana na uzoefu wa kifo, unaotarajiwa na mateso, hasara, na kushindwa. “Binadamu hawezi kukwepa kifo - "Dalla morte nullu homo vivente po skampare"aliimba Mtakatifu Francis (rej. Cantico di frate sole) wimbo wa Ndugu Jua. Kila kitu kilibadilika asubuhi hiyo wakati wanawake, waliokuwa wamekwenda kaburini kupaka mafuta mwili wa Bwana, walikuta kaburi tupu. Swali lililoulizwa na Mamajusi kutoka Mashariki waliokuja Yerusalemu: "Yuko wapi mfalme mpya wa Wayahudi?" (Mt 2:1-2) swali hili linapata jibu lake la uhakika katika maneno ya kijana wa ajabu aliyevaa nguo nyeupe ambaye anazungumza na wanawake alfajiri ya Pasaka: "Mnamtafuta Yesu wa Nazareti, aliyesulubiwa. Hayupo hapa; amefufuka" (Mk 16:6).

Kuanzia asubuhi hiyo hadi leo, kila siku, Yesu pia atakuwa na jina hili: Aliye Hai, kama anavyojionesha katika Ufunuo: "Mimi ni wa Kwanza na wa Mwisho, na Aliye Hai. Nilikuwa nimekufa, na tazama, ni hai milele na milele" (Ufu 1:17-18). Na ndani Yake tuna uhakika wa kupata Nyota ya Kaskazini kila wakati ambayo tutaelekeza maisha yetu yanayoonekana kuwa ya machafuko, yenye alama na matukio ambayo mara nyingi yanaonekana kutatanisha, yasiyokubalika, na yasiyoeleweka: uovu, katika pande zake nyingi, mateso, kifo, matukio yanayoathiri kila mmoja wetu. Kwa kutafakari fumbo la Ufufuo, tunapata jibu la kiu yetu ya maana.

Umati wa waamini katika uwanja wa Mtakatifu Petro
Umati wa waamini katika uwanja wa Mtakatifu Petro   (@Vatican Media)

Kwa kukabiliwa na ubinadamu wetu dhaifu, ujumbe wa Pasaka unakuwa utunzaji na uponyaji, tumaini linalolisha licha ya changamoto kubwa ambazo maisha hutupatia kila siku, kibinafsi na kimataifa. Kwa mtazamo wa Pasaka, Njia ya Msalaba  inabadilishwa kuwa Njia ya Mwanga. Tunahitaji kufurahia na kutafakari furaha baada ya maumivu, ili kupitia tena katika mwanga mpya hatua zote zilizotangulia Ufufuko.

Pasaka haiondoi msalaba, bali inaushinda katika pambano la ajabu lililobadilisha historia ya mwanadamu. Wakati wetu pia, uliowekwa alama na misalaba mingi, unahitaji mapambazuko ya tumaini la Pasaka. Ufufuko wa Kristo si wazo, nadharia, bali Tukio ambalo ni msingi wa imani. Yeye, Aliyefufuka, anaendelea kutukumbusha hili kupitia Roho Mtakatifu, ili tuweze kuwa mashahidi wake hata pale ambapo historia ya mwanadamu haioni mwangaza wowote. Tumaini la Pasaka halikatishi tamaa. Kuamini Pasaka kweli kupitia safari yetu ya kila siku kunamaanisha kuleta mapinduzi katika maisha yetu, kubadilishwa ili kubadilisha ulimwengu kwa nguvu ya upole na ujasiri ya tumaini la Kikristo.

Katekesi ya Papa Novemba 5
05 Novemba 2025, 11:51