Papa Leo XIV katika Kanisa Kuu la Kiarmenia:kumechanua mazungumzo ya upendo

Papa Leo XIV alisali katika Kanisa Kuu la Kitume la Armenia huko Istanbul na alimshukuru Mungu kwa ushuhuda wa ujasiri unaotolewa na Waarmenia katika historia na mara nyingi katikati ya hali mbaya.Tunapaswa kupata msukumo kutoka uzoefu wa Kanisa changa ili kurejesha ushirika kamili,ushirika ambao haumaanishi kunyonya au kutawala,bali kubadilishana vipaji ambavyo Makanisa yetu yamepokea kutoka Roho Mtakatifu kwa ajili ya utukufu wa Mungu Baba na ujenzi wa mwili wa Kristo.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika siku yake ya nne na ya mwisho ya Ziara yake ya Kitume nchini Türkiye,- Uturuki, Dominika tarehe 30 Novemba 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV alianza siku hiyo kwa sala katika Kanisa Kuu la Kitume la Armenia huko Istanbul. Katika hotuba yake, Papa alimsalimia Patriaki  Karekin II, Patriaki, Mkuu wa Wakatoliki wa Waarmenia Wote, na jumuiya nzima ya Kitume ya Armenia huko Türkiye,(Uturuki). Alimshukuru Mungu kwa ushuhuda wa Kikristo wa ujasiri wa watu wa Armenia katika historia, mara nyingi katikati ya hali mbaya. Papa Leo XIV alitoa shukrani zake kwa uhusiano unaokua wa kidugu unaounganisha Kanisa la Kitume la Armenia na Kanisa Katoliki.

Papa akiwa katika Kanisa Kuu la Kiarmenia
Papa akiwa katika Kanisa Kuu la Kiarmenia   (@Vatican Media)

Muda mfupi baada ya Mtaguso wa II wa Vaticani mnamo Mei 1967, Patriaki Khoren I alikuwa wa kwanza wa Kanisa la Kirthodox la Mashariki kutembelea na kubadilishana mkumbatio wa amani na Askofu wa Roma. Pia alikumbusha kwamba mnamo Mei 1970, Patriaki Vasken I alisaini na Papa Paulo VI tamko la kwanza la pamoja kati ya Papa na Patriaki wa Kiorthodox wa Mashariki, akiwaalika waamini wao kujigundua upya kama kama kaka na  dada katika Kristo kwa lengo la kukuza umoja. Tangu wakati huo, kwa neema ya Mungu, "mazungumzo ya upendo" kati ya Makanisa yetu yamestawi".

Wakati wa sala katika Kanisa Kuu la Kiarmenia
Wakati wa sala katika Kanisa Kuu la Kiarmenia   (@Vatican Media)

Katika kumbukumbu hii ya miaka 1700 ya Mtaguso wa kwanza wa kiekumeni, ziara yangu inatoa fursa ya kusherehekea Imani ya Nicea. Lazima tujifunze kutoka kwa imani hii ya pamoja ya kitume ili kurejesha umoja uliokuwepo katika karne za mwanzo kati ya Kanisa la Roma na Makanisa ya kale ya Mashariki. Pia tunapaswa kupata msukumo kutoka kwa uzoefu wa Kanisa la kwanza ili kurejesha ushirika kamili, ushirika ambao haumaanishi kunyonya au kutawala, bali badala yake ni kubadilishana zawadi zilizopokelewa na Makanisa yetu kutoka kwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya utukufu wa Mungu Baba na ujenzi wa mwili wa Kristo (taz. Efe 4:12).

Papa katika Kanisa Kuu la Kiarmenia
Papa katika Kanisa Kuu la Kiarmenia   (@Vatican Media)

"Ni matumaini yangu kwamba Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Mazungumzo ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Orthodox ya Mashariki itaweza kuanza tena kazi yake yenye matunda haraka, ikitafuta mfano wa ushirika kamili pamoja, bila shaka, kama Papa  Yohane Paulo II alivyotaka katika Waraka wake wa  Unum sint. "Katika safari hii kuelekea umoja, tunatanguliwa na kuzungukwa na "wingu kubwa la mashahidi" (Ebr 12:1). Miongoni mwa watakatifu wa tamaduni ya Kiarmenia, Baba Mtakatifu alipenda  kumkumbuka  Patriaki  na mshairi mkuu wa karne ya 12, Nerses IV Shnorhali, ambaye tuliadhimisha kumbukumbu ya miaka 850 ya kifo chake hivi karibuni, na ambaye alifanya kazi bila kuchoka kupatanisha makanisa ili kutimiza sala ya Kristo kwamba "wote wawe wamoja" (Yh 17:21). Mfano wa Mtakatifu Nerses ututie moyo na sala yake ituimarishe katika njia ya ushirika kamili!"

Papa akionja Mkate kutoka katika sahani iliyoshikwa na watoto
Papa akionja Mkate kutoka katika sahani iliyoshikwa na watoto   (@Vatican Media)

Watoto kadhaa walijipanga kwenye njia ya Kanisa Kuu huku Papa Leo XIV akiingia katika maandamano pamoja na Patriaki Sahak II na makuhani wa Kanisa la Kitume la Armenia, huku kwaya ikiimbwa, vyombo vya muziki vikilia na uvumba ukijaa hewani. Juu ya mlango wa kuingia Kanisani, waliokuwepo waliweza kumuona mwanamume amesimama kwenye ukingo kupitia dirishani, akipiga kengele za Kanisa Kuu. Mwanamke mmoja katika umati alifuta machozi kutoka mashavuni mwake maandamano yalipopita. Watoto walisimama kwa msisimko karibu na kila mmoja wao wakiwa na mitandio iliyofunikwa shingoni mwao ikiwa na nembo ya ziara ya Papa.

Kanisa Kuu la Kiarmenia
Kanisa Kuu la Kiarmenia   (@Vatican Media)

“Sisi ndio jumuiya kubwa zaidi ya Kikristo huko Türkiye, kwa hivyo kumkaribisha Papa katika Kanisa letu ni muhimu sana kwetu," alisema Dkt. Drtad Uzunyan, Kuhani na Mjumbe wa baraza la kidini. "Natumaini hili litaleta uhusiano wa kiekumeni wa karibu zaidi kati ya Makanisa hayo mawili. Tayari ni mzuri sana, lakini natumaini kwamba litaongezeka katika siku zijazo." Alikumbuka kwamba, ingawa Papa Leo XIV ndiye Papa wa nne kuja Kanisa Kuu—baada ya Paulo VI, Yohane Paulo II, na Benedict XIV—mwaka 2014, Papa Francis alimtembelea Patriaki wa Armenia wakati huo, ambaye alikuwa mgonjwa hospitalini huko Istanbul. Kwa hivyo Papa Leo ndiye Papa wa nne katika Kanisa Kuu lakini Papa wa tano katika jumuiya ya Waarmenia,” Mkuu wa Kanisa Uzunyan alisema, akitabasamu.

Asante kwa kusoma makala haya. Ukitaka kuendelea kupata taarifa mpya, tafadhali jiandikishe kwa jarida letu:cliccando qui

 

30 Novemba 2025, 11:34