Papa Leo XIV:Njia Njia mpya za kupeleka Neno la Mungu lilipofichwa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 17 Novemba 2025 akikutana na Wajumbe wa Bodi ya Shirikisho la Biblia Kikatoliki wakiwa katika Ukumbi wa Mapapa, mjini Vatican aliwakaribisha na kutoa salamu, akianza kumshukuru Kardinali Kurt Koch, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya kuhamasisha Umoja wa Wakristo, kwa uwepo wake na Kardinali Luis Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Papa wa Baraza la Kipapa kwa Uinjilishaji na Rais wa Shirikisho la Biblia Katoliki. Pia aliwakaribisha wajumbe wa Kamati ya Uongozi, Waratibu wa Kanda, Sekretarieti Kuu na Marafiki wa Shirikisho la Biblia Katoliki. Kwa kila mmoja wao na kwa wote wanaowawakilisha, alitoa shukrani zake za dhati kwa huduma yao kwa Neno la Mungu.
Ufunuo wa Kimungu katika Dei Verbum
Katiba ya Dogmatic kuhusu Ufunuo wa Kimungu, Dei Verbum, ambayo tunaadhimisha miaka yake sitini mwaka huu 2025, inahitimisha kwa maneno yafuatayo: “Tuombeeni ili neno la Bwana lienee haraka na kutukuzwa kila mahali, kama vile lilivyo kwenu”(2 Thes 3:1). Ombi hili la Mtume Paulo kwa Wathesalonike linaonesha hamu kubwa, imani thabiti na mbinu ya kichungaji ambayo inaweza kuongoza tafakari yetu pamoja. Mafundisho ya Dei Verbum hayana shaka; Tumeitwa “kusikia Neno la Mungu kwa heshima na kulitangaza kwa imani”(taz. DV 1), na “upatikanaji rahisi wa Maandiko Matakatifu unapaswa kutolewa kwa waamini wote Wakristo” (DV 22).
Maono haya haya yanaonekana katika Katiba yao, Papa alisema ambayo inathibitisha kwamba Shirikisho la Biblia la Kikatoliki "linakuza na kuendeleza Huduma ya Kichungaji ya Kibiblia kwa njia ambayo inaruhusu Neno la Mungu kama lilivyo katika Maandiko Matakatifu, kuwa chanzo chenye nguvu cha msukumo kwa maeneo yote ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu wa leo" (Katiba ya Shirikisho la Biblia la Kikatoliki, Kifungu cha 9). Katika siku hizi za majadiliano, Papa aliwahimiza kuchunguza upya uaminifu wao binafsi na wa kikanisa kwa agizo hilo, ambalo si kitu kingine ila tangazo la kerygma, fumbo la wokovu la Bwana wetu Yesu Kristo.
Utume na maono yanapaswa kuongozwa na imani
Hakika, Papa Leo XIV alisema utume na maono yenu yanapaswa kuongozwa na imani kwamba Kanisa halichomoi uhai kutoka kwake bali kutoka kwa Injili. Kutoka kwa Injili, hugundua tena mwelekeo wa safari yake, chini ya mwongozo wa Roho Mtakatifu, anayefundisha mambo yote na kutukumbusha kila kitu ambacho Mwana alisema (taz. Yh 14:26). Kwa hivyo, kusikia Neno la Mungu na kulitangaza ni matendo ya kikanisa ipasavyo: Bibi arusi akisikiliza kwa upendo mwingi sauti ya Bwana arusi(taz. Wimbo 2:8–10).
Papa aliongeza kuwa wakati huo huo, kuhakikisha upatikanaji rahisi wa Maandiko Matakatifu kwa waamini wote ni muhimu, ili kila mtu aweze kukutana na Mungu anayesema, anayeshiriki upendo wake, na kutuvuta katika utimilifu wa uzima (taz. Yh 10:10). Katika suala hili, tafsiri za Maandiko Matakatifu zinabaki kuwa muhimu sana, na Papa aliwashukuru kwa kujitolea kwao kukuza Mafundisho ya Kimungu na kila mpango unaohimiza usomaji wa Biblia mara kwa mara. Lakini leo hii, vizazi vipya hukaa katika mazingira mapya ya kidijitali ambapo Neno la Mungu hufunikwa kwa urahisi. Jamii mpya mara nyingi hujikuta katika maeneo ya kiutamaduni ambapo Injili haijulikani au imepotoshwa na mambo yanayovutia. Kwa hivyo, lazima tujiulize: "Ufikiaji rahisi wa Maandiko Matakatifu" unamaanisha nini katika wakati wetu? Tunawezaje kurahisisha mkutano huu kwa wale ambao hawajawahi kusikia Neno la Mungu au ambao tamaduni zao hazijaguswa na Injili?
Neno la Mungu litoe mizizi
Baba Mtakatifu leo anayo matumaini kwamba masuala haya yatawatia moyo katika aina mpya za kuhubiri kibiblia, yenye uwezo wa kufungua njia za Maandiko Matakatifu, ili Neno la Mungu liweze kuota mizizi katika mioyo ya watu na kuwaongoza wote kuishi katika neema yake. Hatimaye, dhamira yao ni kuwa “barua zilizo hai… zilizoandikwa si kwa wino bali kwa Roho wa Mungu aliye hai”(2 Kor 3:1-6), zikishuhudia ukuu wa Neno la Mungu juu ya sauti nyingi zinazojaza ulimwengu wetu. Bikira Maria, Mama wa Mungu na tumbo ambalo Neno lilifanyika mwili, atufundishe ujuzi wa kusikiliza, atuimarishe katika utii kwa Neno lake, na atuongoze kumtukuza Bwana (taz. Lk 1:46). Kwa hisia hizi, amewapatia wao Baraza zake za Kitume na wapendwa wao.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here
