Papa Leo XIV:Wakristo wa Uturuki wajenge madaraja ya udugu

Tunataka kutembea pamoja,tukithamini kile kinachotuunganisha,tukibomoa kuta za dhana ya awali na kutoaminiana,tukikuza uelewano na heshima ya pande zote,ili kuwapatia kila mtu ujumbe mkali wa matumaini na mwaliko wa kuwa"wahudumu wa amani."Ni katika mahubiri ya Papa katika Uwanja wa Mpira wa Volkswagen wa Istanbul katika maadhimisho ya Misa katika Mkesha wa Dominika ya Majilio,Novemba 29.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa katika Ziara yake ya Kwanza ya  Kitume Kimataifa katika kituo cha kwanza huko Turkiye -Uturuki, katika  siku yake ya tatu imehitimishwa kwa maadhimisho ya Misa Takatifu, kwenye mkesha wa Dominika ya Kwanza ya Majilio katika Uwanja wa Mpira wa Volkswagen huko Istanbul. Maadhimisho yaliyohudhuriwa na zaidi ya watu 4,000, kutoka Uturuki nzima(Türkiye), Ankara na Bursa,  Smyrna na Konya, Anatolia na Bahari Nyeusi, pamoja na kutoka mataifa mengine sabini. Pamoja na hao,  Patriaki wa Kiekumeni Bartholomew I ambaye alishiriki na Papa katika maandamano ya kuingia, na kujiunga mapatriaki wengine na viongozi wa madhehebu mengine ya Kikristo.

Misa iliudhuriwa na viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali
Misa iliudhuriwa na viongozi wa dini na madhehebu mbali mbali   (@Vatican Media)

Papa, katika mahubiri yake kwa Kiingereza, alisema kuwa, tunasherehekea Misa hii usiku wa kuamkia siku ambayo Kanisa linamkumbuka Mtakatifu Andrea, Mtume na Msimamizi wa nchi hii. Wakati huo huo, tunaanza Majilio, kipindi cha kujiandaa kupata uzoefu mpya wakati wa Noeli, fumbo la Yesu, Mwana wa Mungu, "aliyezaliwa, ambaye hakuumbwa, mwenye umungo mmoja na Baba"(Imani ya Nicea-Constantinopoli), kama ilivyotangazwa kwa dhati kwa miaka 1700 iliyopita na Mababa waliokusanyika katika Mtaguso wa Nicea. Katika muktadha huo, wa somo la kwanza (taz. Is 2:1-5) la Misa  linatoka katika mojawapo ya vifungu vizuri zaidi katika kitabu cha nabii Isaya, ambapo mwaliko unasikika tena, ukiwaita watu wote kupanda mlima wa Bwana (Is 2, 3), mahali pa mwanga na amani.

Papa wakati wa mahubiri
Papa wakati wa mahubiri   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV alipenda kutafakari pamoja maana ya kuwa sehemu ya Kanisa kwa kutafakari baadhi ya picha zilizotolewa katika maandishi hayo. Picha ya kwanza ni ile ya mlima "uliowekwa kama kilele cha milima" (taz. Isaya 2:2). Inatukumbusha kwamba matunda ya kitendo cha Mungu katika maisha yetu ni zawadi si kwetu tu, bali kwa kila mtu. Sayuni ni mji uliojengwa juu ya mlima na ishara ya jumuiya iliyozaliwa upya katika uaminifu. Uzuri wake ni mwanga wa nuru kwa wanaume na wanawake kutoka kila mahali, na hutumika kama ukumbusho kwamba furaha ya wema inaambukiza. Maisha ya watakatifu wengi yanathibitisha hili. Mtakatifu Petro anakutana na Yesu kutokana na shauku ya kaka yake Andrea (taz. Yh 1:40-42), ambaye aliongozwa kwa Bwana, pamoja na Mtume Yohane, na bidii ya Yohane Mbatizaji.

Mtakatifu Agostino, karne nyingi baadaye, anamjia Kristo kutokana na mahubiri ya bidii ya Mtakatifu Ambrosi na kuna mifano mingi kama hiyo. Hapo tunapata mwaliko wa kufufua nguvu ya ushuhuda wetu wa imani. Mtakatifu Yohane Chrysostom, mchungaji mkuu wa Kanisa hilo, alizungumzia mvuto wa utakatifu kama ishara yenye ufasaha zaidi kuliko miujiza mingi. Alisema: “Muujiza hutokea na kupita, lakini maisha ya Kikristo yanabaki na hujenga daima” (Tafakari Injili ya Mtakatifu Mt,43, 5). Kwa kumalizia, alihimiza: “Basi na tujitunze nafsi zetu, ili tupate pia kuwanufaisha wengine.”

Wakati wa maadhimisho ya Misa Novemba 29
Wakati wa maadhimisho ya Misa Novemba 29   (@Vatican Media)

Papa alisisitiza kuwa, ikiwa kweli tunataka kuwasaidia watu tunaokutana nao, na “tujilinde” nafsi zetu, kama Injili inavyopendekeza (taz. Mt 24:42) kwa kukuza imani yetu kwa sala, pamoja na sakramenti, kuishi maisha yake kwa upendo, na kuacha,  kama Mtakatifu Paulo anavyotuambia katika somo la pili,  matendo ya giza na kuvaa silaha za nuru (taz. Rm 13:12). Bwana, ambaye tunamngojea katika utukufu mwishoni mwa wakati, huja kila siku kubisha mlangoni petu. Tuwe tayari kwa ajili yake (taz. Mt 24:44), tukiwa tumejitolea kwa dhati kuishi maisha ya wema, kwa mfano wa wanaume na wanawake wengi watakatifu ambao wameishi katika nchi hii kwa vizazi vyote.

Taswira ya pili inayotujia kutoka kwa nabii Isaya ni ile ya ulimwengu ambao amani inatawala. Hivi ndivyo anavyoielezea: “Watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu ya kupogoa; taifa halitainua upanga juu ya taifa, wala hawatajifunza vita tena” (Is 2:4). Jinsi gani wito huu ni wa haraka sana kwetu leo! Jinsi gani hitaji la amani, umoja na maridhiano linalotuzunguka, ndani yetu na miongoni mwetu! Mchango wetu unaweza kuwa nini katika kujibu? Ili kuelewa vyema hili, hebu tutazame  nembo ya ziara hiyo, ambayo moja ya picha zilizochaguliwa ni ile ya daraja. Hiyo inaweza pia kutufanya tufikirie njia kubwa maarufu katika jiji hilo, ambalo huvuka Mlango-Bahari wa Bosporus na kuunganisha mabara mawili: Asia na Ulaya.

Misa katika Uwanja wa Volkswagen
Misa katika Uwanja wa Volkswagen   (@Vatican Media)

Kwa muda, vivuko vingine viwili vimeongezwa, hivi kwamba sasa kuna sehemu tatu za uhusiano kati ya pande hizo mbili. Miundo hii mitatu mikubwa ya mawasiliano, kubadilishana na kukutana inavutia kuona, lakini ni midogo na dhaifu ikilinganishwa na maeneo makubwa yanayounganisha. Umbali wao wa mara tatu kuvuka Mlango-Bahari unatukumbusha umuhimu wa juhudi zetu za pamoja za kujenga madaraja ya umoja katika ngazi tatu: ndani ya jumuiya, katika mahusiano ya kiekumeni na wajumbe wa madhehebu mengine ya Kikristo, na katika kukutana kwetu na kaka na dada wa dini zingine. Kutunza vifungo hivi vitatu, kuviimarisha na kuvipanua kwa kila njia inayowezekana, ni sehemu ya wito wetu wa kuwa mji uliojengwa juu ya kilima (taz. Mt 5:14-16).

Kifungo cha kwanza cha umoja ambacho Papa alikuwa amekitaja ni kile kilicho ndani ya Kanisa hilo, ambalo katika nchi hiyo lina tamaduni  nne tofauti za kiliturujia,  Kilatini, Kiarmenia, Kikaldayo na Kisiria. Kila moja huchangia utajiri wake wa kiroho, kihistoria na kikanisa. Kushiriki kwa tofauti hizi kunaonesha wazi moja ya sifa nzuri zaidi za uso wa Bibi arusi wa Kristo: ukatoliki unaounganisha. Umoja unaotuunganisha pamoja kuzunguka madhabahu ni zawadi kutoka kwa Mungu. Kwa hivyo, ni imara na isiyoshindika, kwa sababu ni kazi ya neema yake. Wakati huo huo, hata hivyo, utambuzi wa umoja huu kwa wakati umekabidhiwa kwetu, kwa juhudi zetu. Kwa sababu hiyo, kama madaraja juu ya Bosporus, umoja unahitaji uangalifu, umakini na "matunzo," ili misingi yake ibaki imara na isidhoofishwe na wakati na mabadiliko.

Misa huko uwanja wa Volkswagen
Misa huko uwanja wa Volkswagen   (@Vatican Media)

Tukiwa tumegeukia mlima ulioahidiwa, mfano wa Yerusalemu ya Mbinguni, ambayo ndiyo mwisho wetu na mama yetu (taz. Gal 4:26), basi, tufanye kila juhudi kukuza na kuimarisha vifungo vinavyotuunganisha, ili tuweze kutajirishana na kuwa ishara ya kuaminika mbele ya ulimwengu wa upendo wa Bwana wa ulimwengu wote na usio na kikomo. Kwa njia hiyo Papa alisisitiza kwamba tufanye kila juhudi kukuza na kuimarisha vifungo vinavyotuunganisha, ili tuweze kutajirishana na kuwa ishara ya kuaminika mbele ya ulimwengu ya upendo wa Bwana wa ulimwengu wote na usio na kikomo.

Kifungo cha pili cha umoja ambacho liturujia hii inakipendekeza ni umoja wa kiekumeni. Hili pia linathibitishwa na uwepo wa Wawakilishi wa Madhehebu mengine ya Kikristo, ambao aliwasalimu kwa upendo. Hakika, imani ile ile katika Yesu Mwokozi wetu inaunganisha si, sisi tu ndani ya Kanisa Katoliki, bali pia kaka na dada zetu wote wa Makanisa mengine ya Kikristo. Papa alisema hjinis ambavyo walihuhudia tarehe 28 Novemba katika sala huko İznik. “Hii pia ni njia ambayo tumekuwa tukitembea pamoja kwa muda. Mtakatifu Yohane XXIII, ambaye aliunganishwa na nchi hii kwa uhusiano mkubwa wa upendo wa pande zote, alikuwa mhamasishaji mkuu wa, na shahidi wa, ushirika wa kiekumeni.

Misa takatifu 29 Novemba
Misa takatifu 29 Novemba   (@Vatican Media)

Kwa hivyo, tunapoomba kwa maneno ya Papa Yohane kwamba "fumbo kuu la umoja huo ambalo Kristo Yesu alimwomba Baba wa Mbinguni kwa sala za dhati usiku wa kuamkia sadaka yake liweze kutimizwa"(Mtaguso wa Kiekumeni wa Vatican, Oktoba 11, 1962, 8.2), tunasasisha leo "ndiyo" yetu kwa umoja, "ili wote wawe kitu kimoja" (Yh 17:21), ut unum sint. Kifungo cha tatu cha umoja, ambacho neno la Mungu linatuita, ni kile kinachohusiana na washiriki wa jumuiya zisizo za Kikristo. Tunaishi katika ulimwengu ambapo dini hutumika mara nyingi sana kuhalalisha vita na ukatili. Hata hivyo, kama Mtaguso wa Pili wa Vatican ulivyotangaza, "mtazamo wa wanadamu kuelekea Mungu Baba na ule wa mwanadamu kuelekea wanaume na wanawake wenzake umeunganishwa kwa karibu sana kiasi kwamba Maandiko yanasema: 'Yeyote asiyependa hamjui Mungu' (1 Yh 4:8)" (Tamko Nostra Aetate, 5).

Kwa hivyo, Papa Leo alisema kwamba tunataka kutembea pamoja kwa kuthamini kile kinachotuunganisha, kuvunja kuta za chuki na kutoaminiana, kukuza ujuzi na heshima ya pande zote ili kuwapa wote ujumbe wenye nguvu wa matumaini na mwaliko wa kuwa "wapatanishi"(Mt 5:9). Papa Leo XIV kwa kuhitimisha alisema kwamba “tufanye maadili haya kuwa maazimio yetu kwa ajili ya kipindi cha Majilio na zaidi kwa maisha yetu binafsi na ya pamoja. Tunasafiri kana kwamba tuko kwenye daraja linalounganisha dunia na Mbingu, daraja ambalo Bwana ametujengea.” Kwa hiyo  tuendelee kutazama pwani zote mbili, ili tuweze kumpenda Mungu na kaka na dada zetu kwa mioyo yetu yote ili tuweze kusafiri pamoja na kujikuta siku moja tumeungana katika nyumba ya Baba.

Papa Leo akimsalimia mzee
Papa Leo akimsalimia mzee   (@Vatican Media)
29 Novemba 2025, 17:30