Papa Leo XIV:Mateso ya Wakristo hayatokea kwa silaha&unyanyasaji tu,pia kwa maneno ya uongo

Kabla ya Malaika wa Bwana,Dominika Novemba 16,Papa Leo XIV,alisema kuwa Wale wanaomtumaini Yesu wanajua kwamba majanga na mateso yana mwisho na kwamba neema ya Mungu ina uwezo wa kubadilisha hata vurugu kuwa ishara ya ukombozi.Kwa njia hiyo tusishindwe na hofu tunapokabiliana na migogoro,maafa na mateso.Na kwamba mateso ya Wakristo hayatokei kwa silaha na unyanyasaji tu,bali pia kwa maneno,yaani,kupitia uongo na udanganyifu wa kiitikadi.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV mara baada ya Misa ya Jubilei ya Maskini, na Siku ya IX ya Maskini Duniani katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, alikwenda katika Dirisha la Jumba la Kitume mjini Vatican na akatoa tafakari kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana kwa waamini, waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, mjini Vatican, Dominika tarehe 16 Novemba 2025. Papa Leo XIV lianza kuwatakia Dominika Njema kwa  kaka na dada na kwamba “Mwaka wa liturujia unapokaribia kuisha, Injili ya leo (Lk 21:5-19) inatuhimiza kutafakari kuhusu msukosuko wa historia na mwisho wa mambo. Kwa sababu anajua mioyo yetu, Yesu, akiangalia matukio haya, anatualika kwanza kabisa tusishindwe na hofu: "Mtakaposikia habari za vita na maasi," anasema, "msiogope" (Lk 21, 9). Wito wake ni wa wakati unaofaa sana: cha kusikitisha, kiukweli, tunapokea habari za kila siku za migogoro, majanga, na mateso yanayowatesa mamilioni ya wanaume na wanawake.

Papa wakati wa sala ya Malaika wa Bwana Novemba 16
Papa wakati wa sala ya Malaika wa Bwana Novemba 16   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV alisisitiza kwamba “Iwe tunakabiliwa na mateso haya au kwa kutojali kunakojaribu kuyapuuza, maneno ya Yesu yanatangaza kwamba uchokozi wa uovu hauwezi kuharibu tumaini la wale wanaomtumaini. Kadiri saa inavyozidi kuwa nyeusi, ndivyo imani angavu inavyong'aa kama jua. Mara mbili, kiukweli, Kristo anasema kwamba "kwa ajili ya jina lake" wengi watapitia vurugu na usaliti (taz. Lk 21: 12, 17), lakini hapo ndipo watapata fursa ya kutoa ushahidi (taz. mst. 13). Kwa kufuata mfano wa Bwana, ambaye msalabani alifunua ukuu wa upendo wake, faraja hii inatuhusu sote.

Waamini waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Waamini waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro   (@Vatican Media)

Kiukweli, mateso ya Wakristo hutokea si kwa silaha na unyanyasaji tu, bali pia kwa maneno, yaani, kupitia uongo na udanganyifu wa kiitikadi. Hasa tunapokandamizwa na maovu haya, ya kimwili na kiadili, tunaitwa kushuhudia ukweli unaookoa ulimwengu, kwa haki inayowakomboa watu kutoka kwa ukandamizaji, kwa tumaini linaloelekeza njia ya amani kwa wote. Katika mtindo wao wa kinabii, maneno ya Yesu yanathibitisha kwamba majanga na maumivu ya historia yana mwisho, huku furaha ya wale wanaomtambua kama Mwokozi ikikusudiwa kudumu milele. "Kwa uvumilivu wenu mtapata uhai wenu" (Lk 21, 19): Ahadi hii ya Bwana inatutia nguvu ya kupinga matukio ya kutishia ya historia na kila kosa; hatubaki bila nguvu mbele ya maumivu, kwani Yeye Mwenyewe anatupa "maneno na hekima" (mstari wa 15), ili tufanye mema kila wakati kwa moyo unaowaka.

Umati wa waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Umati wa waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro   (@Vatican Media)

 

Papa alibainisha tena kwamba katika historia yote ya Kanisa, ni zaidi ya yote mashahidi wanaotukumbusha kwamba neema ya Mungu ina uwezo wa kubadilisha hata vurugu kuwa ishara ya ukombozi. Kwa hivyo, tukiungana na ndugu na dada zetu wanaoteseka kwa ajili ya jina la Yesu, hebu tutafute kwa ujasiri maombezi ya Mariamu, Msaada wa Wakristo. Katika kila jaribu na ugumu, Bikira Mtakatifu atufariji na kututegemeza.

Tafakari ya Angelus 16 Novemba

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwenye jarida letu la kila siku. Just click here

16 Novemba 2025, 14:22