Papa:Uturuki ina jukumu muhimu katika amani Mashariki ya Kati na Ukraine
Vatican News
Katika safari ya ndege kutoka Istanbul hadi Beirut, nchini Lebanon ikiwa ni awamu ya pili ya Ziara yake ya kwanza ya kitume ya kimataifa, Baba Mtakatifu Leo XIV aliwasalimia waandishi wa habari 81 waliokuwa ndani ya ndege hiyo. Papa alianza: “Good afternoon! Habari za mchana kwa wote! "Ninafurahi kuwasalimu. Ninatumaini mlikuwa na wakati mzuri nchini Uturuki, kama mimi nilivyofanya. Nadhani ilikuwa uzoefu mzuri." Kisha Papa aliishukuru nchi iliyomkaribisha yeye na wote waliowezesha ziara hiyo ya siku tatu, na akajibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari wawili wa Uturuki(Türkiye). Swali moja hasa lilihusu matarajio ya amani huko Gaza, ambalo alithibitisha tena suluhisho la mataifa mawili. Kuhusu Ukraine, alitoa wito wa mazungumzo na kusitisha mapigano, akisisitiza jukumu la upatanishi la Uturuki(Türkiye).
“Kama mnavyojua sababu za kwenda nchini Uturuki(Türkiye) ilikuwa ni maadhimisho ya miaka 1700 ya Mtaguso wa Nicea. Tulikuwa na sherehe nzuri sana, rahisi sana lakini yenye kina, katika eneo la moja la makanisa ya kale ya Nicea ili kuadhimisha tukio kubwa la makubaliano ya jumuiya nzima ya Kikristo na ungamo la kanuni ya imani, yaani Imani ya Nicea-Constantinopoli. Zaidi ya hayo, tulisherehekea matukio mengine kadhaa. Ningependa kutoa shukrani zangu kwa kila mtu kwa kazi iliyofanywa kuandaa ziara hiyo, kuanzia na Balozi, wafanyakazi, timu nzima huko Roma iliyoshughulikia maandalizi hayo, lakini ninawashukuru sana Serikali ya Uturuki(Türkiye,) Rais Erdogan na watu wengi aliowapa mamlaka ili kuhakikisha safari hiyo inafanikiwa kikamilifu: helikopta yake binafsi, njia zote za usafiri, maandalizi, uwepo wa wahudumu katika nyakati mbalimbali za maisha. Nadhani ilikuwa mafanikio makubwa. Nilifurahi sana kupata nyakati tofauti na Makanisa tofauti, na jumuiya tofauti za Kikristo, na makanisa ya Kiorthodox, ikifikia kilele asubuhi ya leo na Liturujia Takatifu na Patriaki Bartholomew, ambayo ilikuwa sherehe nzuri sana. Natumaini nyote mlipata uzoefu sawa na mimi.
Baris Seçkin (Anadolu Ajansi): Mwanzoni mwa safari yako ya Papa, ulirejea amani ya kimataifa na kikanda. Katika suala hili, maoni yako ni yapi kuhusu jukumu la Uturuki katika kufikia na kudumisha amani ya kikanda na kimataifa, na mazungumzo yako na Rais Erdogan yamekuwaje kuhusu mada hii?
Kuja Uturuki(Türkiye) na sasa nchini Lebanon, kwa dhati kulikuwa na mada maalum: kuwa mjumbe wa amani, kutaka kukuza amani katika eneo lote. Uturuki (Turkiye) ina sifa nyingi katika suala hili: ni nchi yenye Waislamu wengi na pia ina uwepo wa jumuiya nyingi za Kikristo,ni wachache, na hata watu wa dini zingine wanaweza kuishi kwa amani. Ningesema, ni mfano wa kile tunachotafuta sote ulimwenguni. Zaidi ya tofauti za kidini, zaidi ya tofauti za kikabila, zaidi ya tofauti zingine nyingi, watu wanaweza kuishi kwa amani. Uturuki ( Türkiye) yenyewe imekuwa na nyakati mbalimbali katika historia yake ambapo haijaweza kufanya hivyo kila wakati, na baada ya kuishi tu uzoefu huu na kuweza kuzungumza na Rais Erdogan kuhusu amani, nadhani, ni kipengele muhimu, kipengele muhimu cha ziara yangu.
Seyda Canepa (NTV):Baba Mtakatifu zaidi ya taarifa rasmi, je, umejadili hali ya Gaza na Rais Erdogan, ikizingatiwa kwamba Vatican na Uturuki zinashiriki maono sawa ya suluhisho la mataifa mawili, watu wawili? Kuhusu Ukraine, Vatican imesisitiza mara kwa mara jukumu la Uturuki, kuanzia na ufunguzi wa njia ya kupeleka nafaka mwanzoni mwa mzozo. Kwa hivyo, unaona matumaini yoyote ya suluhisho nchini Ukraine na mchakato wa amani wa haraka huko Gaza kwa wakati huu?
Kwa hakika tumejadili hali zote mbili. Vatican imeunga mkono hadharani pendekezo la suluhisho la mataifa mawili kwa miaka kadhaa. Sote tunajua kwamba Israeli bado haikubali suluhisho hili, lakini tunaliona kama suluhisho pekee linaloweza kutatua mgogoro unaoendelea. Sisi pia ni marafiki wa Israeli na tunatafuta kupatanisha pande zote mbili, kutusaidia kusogea karibu na suluhisho lenye haki kwa wote. Nimezungumza kuhusu hili na Rais Erdogan, na hakika anakubaliana na pendekezo hili. Uturuki ina jukumu muhimu la kuchukua katika hili. Vile vile kwa Ukraine. Miezi michache iliyopita, kwa uwezekano wa mazungumzo kati ya Ukraine na Urusi, rais alikuwa muhimu katika kuzikutanisha pande hizo mbili. Kwa bahati mbaya, hatujaona suluhisho bado, lakini leo kuna mapendekezo thabiti tena ya amani. Na tunatumaini kwamba Rais Erdogan, pamoja na uhusiano wake na marais wa Ukraine, Urusi, na Marekani, anaweza kusaidia katika suala hili, kukuza mazungumzo, kusitisha mapigano, na kuona jinsi ya kutatua mgogoro huu, vita hivi nchini Ukraine.
Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa, Matteo Bruni (dokezo kutoka kwa Bruni, ambaye ni Msemaji wa Vyombo vya habari vya Vatican) alipendekeza niseme neno baada ya mkutano muhimu wa kiekumeni huko Nicea, na kisha, jana asubuhi, tulijadili mikutano inayowezekana ya siku zijazo. Moja itakuwa mwaka 2033, wa maadhimisho ya miaka elfu mbili ya Ukombozi, Ufufuko wa Yesu Kristo, ambayo ni wazi kuwa ni tukio ambalo Wakristo wote wanataka kusherehekea. Wazo limekubaliwa; bado hatujatoa mwaliko, lakini uwezekano ni kusherehekea, kwa mfano, tukio hili kubwa la Ufufuko huko Yerusalemu mwaka 2033. Bado kuna miaka ya kujiandaa kwa ajili yake. Lakini ulikuwa mkutano mzuri sana, kwa sababu Wakristo kutoka tamaduni tofauti walikuwepo na waliweza kushiriki wakati huu.
Asante. Salamu kwa kila mtu, na safari njema!
