Huu ni mwaliko kwa Wakristo kutembea kwa pamoja katika hija ya maisha ya kiroho kuelekea Maadhimisho ya Mwaka wa Ukombozi, yaani miaka 2033 ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, huko mjini Yerusalemu Huu ni mwaliko kwa Wakristo kutembea kwa pamoja katika hija ya maisha ya kiroho kuelekea Maadhimisho ya Mwaka wa Ukombozi, yaani miaka 2033 ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, huko mjini Yerusalemu  (@Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Nchini Uturuki na Lebanon 2025

Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru viongozi wote walioshiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso Mkuu wa Nicea uliofanyika Asia Ndogo kunako Mwaka 325.Huu ulikuwa ni Mtaguso wa kwanza wa Kiekumene kufanyika katika Kanisa na hivyo ukaibua imani ambayo ilikamilishwa na Mtaguso wa Kwanza wa Costantinopol ulioadhimishwa Mwaka 381 na hivyo kutoa dira na mwongozo wa imani ya Kanisa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Uturuki kuanzia tarehe 27 hadi tarehe 30 Novemba 2025 imenogeshwa na kauli mbiu: “Bwana mmoja, Imani na Ubatizo Mmoja.” Baba Mtakatifu Leo XIV amekazia pamoja na mambo mengine: Umuhimu wa uinjilishaji, Utangazaji na ushuhuda wa Injili yaani “Kerygma” kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya wokovu. Utengano kati ya Wakristo ni kikwazo cha ushuhuda wa Injili ya Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kutembea kwa pamoja katika hija ya maisha ya kiroho kuelekea Maadhimisho ya Mwaka wa Ukombozi, yaani miaka 2033 ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, huko mjini Yerusalemu. Hapa ni mahali ambapo Kristo Yesu aliadhimisha Karamu ya Mwisho, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, Siku ile ya Pentekoste, ili kujenga na kuimarisha umoja wa Wakristo huku akirejea kwenye kauli mbiu yake: "In illo Uno Unum" yaani "Ingawa Sisi Wakristo ni Wengi, Katika Kristo Mmoja Sisi ni Wamoja.” Hili ni tukio la kihistoria, ambalo litawakusanya Wakristo kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Wakristo wote ni wamoja katika Kristo Yesu
Wakristo wote ni wamoja katika Kristo Yesu   (@Vatican Media)

Hadi sasa hakuna tarehe maalum ambayo imekwisha kupangwa. Lakini Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru viongozi wote walioshiriki katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso Mkuu wa Nicea uliofanyika Asia Ndogo kunako Mwaka 325.Huu ulikuwa ni Mtaguso wa kwanza wa Kiekumene kufanyika katika historia ya Kanisa na hivyo ukaibua imani ambayo ilikamilishwa na Mtaguso wa Kwanza wa Costantinopol ulioadhimishwa Mwaka 381 na hivyo kutoa dira na mwongozo wa imani ya Kanisa kwa Kristo Yesu. Maadhimisho haya yamefanyika ndani ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Kristo Tumaini Letu” na imeambatanishwa na maadhimisho ya Sherehe ya pamoja ya Pasaka ya Bwana kwa Wakristo wa Makanisa ya Mashariki na Magharibi. Hii imekuwa ni fursa ya kupyaisha tena Kanuni ya Imani ya Nicea-Costantinopoli ambayo ni tafakari ya mchakato wa tafsiri rasmi wa imani ya Kanisa kwa Mungu aliye hai. Yaani Mungu Baba Muumbaji; Mungu Mwana Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu anayetakatifuza, kulitegemeza na kulielekeza Kanisa katika ukweli wote, yaani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Wakristo
Umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Wakristo   (ANSA)

“Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima ni kipengele kinachofafanua asili ya Nafsi ya Tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu anayetenda kazi zake kwa njia ya: Imani, Neno, Sakramenti na Sala za Kanisa. Roho Mtakatifu anawakirimia waamini uzima unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Anawapatia waamini maisha mapya kwa kufisha matendo ya mwili yanayoleta kifo! Atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa na Baba na Mwana ni imani inayoonesha Nafsi ya tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kardinali Raniero Cantalamessa, O.F.M. Cap., amekumbushia kwamba, sehemu hii ya Kanuni ya Imani yaani: “Filioque” ndicho chanzo cha mpasuko kati ya Kanisa la Mashariki na Kanisa la Magharibi. Hii ni imani ya Kanisa katika Umungu Mmoja wenye Nafsi tatu. Roho Mtakatifu hata katika kujificha kwake bado anapendwa katika Fumbo zima la Utatu Mtakatifu na kutambulika kwa alama ya: Mwanga, Moto, Upepo, Maji na Njiwa.

Majadiliano ya kidini na kiekumene
Majadiliano ya kidini na kiekumene   (ANSA)

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Lebanon kuanzia tarehe 30 Novemba hadi tarehe 2 Desemba 2025 imenogeshwa na kauli mbiu “Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Mt. 5:9. Baba Mtakatifu amewataka watu wa Mungu nchini Lebanon kujikita kikamilifu katika kutafuta na kudumisha haki na amani hata katikati ya mtutu wa bunduki na kwamba, hii ni changamoto endelevu dhidi ya: chuki, kiburi, utawala wa mabavu, utengano na uhasama! Amewataka wawe wajenzi, watangazaji na mashuhuda wa amani! Huu ni wakati wa kuasha ile ndoto ya Lebanon inayosimikwa katika umoja, ili haki na amani iweze kutamalaki. Ikumbukwe kwamba, amani ni tunda la haki Rej Yak 3:18; kazi ya haki ni kuleta amani Rej. Isa 32:17 na kwamba, pasipo haki hakuna amani.

Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya Kanisa
Majadiliano ya kidini ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya Kanisa   (@Vatican Media)

Huu ni mwaliko kwa kudumisha umoja na mshikamano, kwa wananchi wakiwa wameungana, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, katika majadiliano yanayokita mizizi yake katika upendo; msingi wa haki, amani na upatanisho, unaowaambata na kuwakumbatia watu wote pasi na ubaguzi au maamuzi mbele, kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, mwaliko kwa waamini wote kukita maisha yao katika imani ya kweli, upendo na unyenyekevu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wahakikishe kwamba, amani inatamalaki dhidi ya hofu na woga usiokuwa na mvuto wala mashiko. Baba Mtakatifu Leo XIV amewataka watu wa Mungu nchini Lebanon kuvunjilia mbali: mitazamo ya kikabila, kidini na kisiasa, ili kuamsha tena ile ndoto ya Lebanon iliyoungana katika umoja, mahali ambapo haki na amani vinatawala na kwamba wananchi wote wanatambuana kuwa ni ndugu wamoja. Rej Isa 11:6.

Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa NICEA
Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso wa NICEA   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Diplomasia inayotekelezwa na Vatican sehemu mbalimbali za dunia inajikita kwa namna ya pekee, katika msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Ni diplomasia inayojipambanua kwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Baba Mtakatifu ameyasema hayo wakati wa mahojiano maalum na waandishi wa habari wapatao 80 waliokuwa kwenye msafara wake nchini Uturuki na Lebanon. Baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa, sasa maisha yake yote yako mikononi mwa Mungu. Vijana wana hamu na kiu ya haki, amani na maridhiano. Baba Mtakatifu Leo XIV ametia nia ya kutembelea Barani Afrika na hususan nchini Algeria ili kutembelea maisha na utume wa Mtakatifu Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa, sanjari na kuendeleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, kuendeleza ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha Waislam na Wakristo. Huu ni mwaliko wa kuwa ni vyombo na wajenzi wa umoja na urafiki wa kijamii; pamoja na kuendeleza majadiliano na walimwengu ili kudumisha haki na amani.

Papa Leo XIV Uturuki na Lebanon
03 Desemba 2025, 14:07