Papa awakumbuka waathirika wa Synedy:"kuna ukatili wa kutosha dhidi ya Wayahudi"
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 15 Desemba 2025 aliwapokea katika Mkutano kwenye Ukumbi wa Paulo VI wafadhili wa mti na mandhari ya Pango la kuzaliwa kwa Yesu, (moja katika Ukumbi wa Paulo VI na jingine katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican), ambalo linazinduliwa alasiri, siku ya Jumatatu Desemba 15. Papa Leo alianza kusema kuwa: “Ninafurahi kuwakaribisha nyote, mliokusanyika hapa kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa mandhari ya Kuzaliwa kwa Yesu na mti wa Noeli unaopamba Uwanja wa Mtakatifu Petro, pamoja na mandhari ya Pango la Kuzaliwa kwa Yesu iliyowekwa katika Ukumbi huu.”
Papa Leo XIV aliendelea “Ninawasalimu wajumbe kutoka Jimbo la Nocera Inferiore-Sarno, ambapo mandhari ya Pango la Kuzaliwa kwa Yesu linaanzia: Askofu Giuseppe Giudice, mamlaka za kiraia, na makundi mbalimbali ya kikanisa. Ninashukuru kwa kazi hii ya kisanii, ambayo inakumbusha vipengele vya kawaida vya eneo lenu, huko Nocera ya Juu, Chemchemi ya Helvius ya Mtakatifu Egidio kwenye Mlima Albino, na ua la kipekee la Agro Nocerino-Sarnese.” Papa Leo alisema kuwa “ Hizi ni sehemu zilizokaliwa na Mtakatifu Alphonsus Maria de' Liguori, Watumishi wa Mungu Padre Enrico Smaldone, na Alfonso Russo. Ninawashukuru makampuni yaliyohusika, mafundi, na wote waliobuni mpango huo na kushirikiana katika utekelezaji wake, wakilenga kuunganisha sanaa na mambo ya kiroho katika mazingira yanayosimulia imani na mizizi ya kiutamaduni ya nchi yenu.”
Papa aliendelea kukazia kuwa "kwa mahujaji kutoka ulimwenguni kote watakaokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, mandhari ya Pango la kuzaliwa kwa Yesu litatukumbusha kwamba Mungu hukaribia ubinadamu, anakuwa mmoja wetu, akiingia katika historia yetu na udogo wa mtoto. Hakika, katika umaskini wa zizi huko Bethlehemu, tunatafakari siri ya unyenyekevu na upendo. Kabla ya kila mandhari ya kuzaliwa kwa Yesu, hata yale yaliyoumbwa katika nyumba zetu, tunakumbuka tukio hilo na kugundua tena hitaji la kutafuta wakati wa ukimya na maombi katika maisha yetu, kujigundua upya na kuingia katika ushirika na Mungu.”
“Bikira Maria ni mfano wa kuabudu ukimya.” Papa akisisitiza kwamba “Tofauti na wachungaji ambao, wakirudi kutoka Bethlehemu, walimtukuza Mungu na kusimulia walichokiona na kusikia, Mama wa Yesu alithamini kila kitu moyoni mwake (Lk, 2:19). Ukimya wake si ukimya tu: ni ajabu na kuabudu. Kando ya mandhari ya Pango la Kuzaliwa kwa Yesu, Mti Mrefu kutoka msitu wa manispaa za Lagundo na Ultimo, katika Jimbo la Bolzano-Bressanone.” Papa aliwaslimu pia “wajumbe kutoka maendeo hayo mazuri: Askofu Ivo Muser, mameya, mamlaka nyingine, na makundi mbalimbali ya kikanisa na kiraia.
Mti huo, pamoja na matawi yake ya kijani kibichi, ni ishara ya uzima na huamsha tumaini ambalo halishindwi kamwe, hata wakati wa baridi kali. Taa zinazoupamba zinaashiria Kristo, nuru ya ulimwengu, ambaye alikuja kuondoa giza la dhambi na kuangazia njia yetu. Mbali na mti mkubwa wa fir, miti mingine midogo iliyokusudiwa kwa ajili ya ofisi, maeneo ya umma na nafasi mbalimbali katika Jiji la Vatican inatoka katika maeneo yale yale ya Tyrol Kusini. Mandhari ya Pango la Kuzaliwa kwa Yesu, ambalo litabaki katika Ukumbi wa Paulo VI katika kipindi chote cha Noeli linatoka huko Costa Rica na likiitwa (Nacimiento Gaudium) “Furaha ya kuzaliwa”.
Baba Mtakatifu Leo aidha alisisitiza kuwa , Mandhari ya Pango la Kuzaliwa kwa Yesu na Mti ni ishara za imani na matumaini; tunapozitafakari katika nyumba zetu, katika parokia, na katika viwanja vya umma, tumwombe Bwana afanye upya ndani yetu zawadi ya amani na udugu. Tuwaombee wale wanaoteseka kwa sababu ya vita na vurugu; hasa, leo ninataka kuwakabidhi kwa Bwana waathiriwa wa shambulio la kigaidi la jana dhidi ya jumuiya ya Wayahudi huko Sydney. Yatosha aina hizi za vurugu za chuki dhidi ya Wayahudi! Lazima tuondoe chuki mioyoni mwetu.
Turuhusu huruma ya Mtoto Yesu iangaze maisha yetu. Turuhusu upendo wa Mungu, kama matawi ya mti wa kijani kibichi, ubaki kuwa wa moto ndani yetu. Ninawashukuru tena nyote, pamoja na Kurugenzi ya Miundombinu na Huduma za Gavana ya mji wa Vatican, kwa kujitolea kwao kwa ukarimu. Kwa kuhitimisha Papa alisisitiza kwamba “Ninapowaombea ulinzi wa mama wa Maria Mtakatifu Zaidi juu yenu na familia zenu, ninawapa Baraka zangu za Kitume kwa uchangamfu. Asante! Kuhusiana na wazo kwa watu wa Sydney, lilitokana na ufyatuaji risasi jana usiku (saa za Australia) katika Ufukwe wa Bondi wakati sherehe za kiyahudi - Hanukkah. "Sikukuu ya taa" ya Kiyahudi imebadilika kuwa wakati wa giza na maumivu kutokana na vifo vya watu 15 (mmoja wa washambuliaji wawili pia aliuawa, akauawa na polisi) na takriban thelathini kujeruhiwa.
