Wito wa Papa Leo XIV:viongozi wa kisiasa wasikilize kilio cha watu
Na Angella rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, mara baada ya Misa Takatifu katika Ufukwe wa Beirut Nchini Lebanon, Jumanne tarehe 2 Desemba 2025, akiwa katika Ziara yake ya Kitume na ya kwanza kimataifa alianza kusema kuwa: "Katika siku hizi, katika Safari yangu ya kwanza ya Kitume, iliyofanywa wakati wa Mwaka wa Jubilei, nimetamani kuwa mhujaji wa matumaini katika Mashariki ya Kati, nikimwomba Mungu zawadi ya amani kwa nchi hii pendwa, iliyojaa ukosefu wa utulivu, vita, na maumivu.
Papa Leo alisema Wapendwa Wakristo wa Mashariki ya Kati, “wakati matokeo ya juhudi zenu za amani yanapochelewa kufika, ninawaalika kuinua macho yenu kwa Bwana anayekuja! Tumtazame kwa matumaini na ujasiri, tukiwaalika kila mtu kuanza njia ya kuishi pamoja, udugu, na amani. Kuwa wajenzi wa amani, watangazaji wa amani, na mashuhuda wa amani!”
“Mashariki ya Kati inahitaji mitazamo mipya, kukataa mantiki ya kisasi na vurugu, kushinda mgawanyiko wa kisiasa, kijamii, na kidini, na kufungua sura mpya kwa jina la upatanisho na amani. Njia ya uadui wa pande zote mbili na uharibifu katika hofu ya vita imesafiri kwa muda mrefu sana, na matokeo mabaya ambayo yapo yanaonwa na wote. Tunahitaji kubadilisha mwelekeo, tunahitaji kuelimisha moyo wa amani.
“Kutoka uwanja huu, nawaombea Mashariki ya Kati na watu wote wanaoteseka kwa sababu ya vita. Pia ninatoa sala, nikitumaini suluhishi la amani kwa migogoro ya kisiasa inayoendelea nchini Guinea-Bissau. Na siwasahau waathiriwa wa moto huko Hong Kong na familia zao. Nawaombea hasa Lebanon pendwa! Naomba jumuiya ya kimataifa tena ifanye juhudi zozote katika kukuza michakato ya mazungumzo na maridhiano.
Ninatoa wito wa dhati kwa wale wote waliowekeza katika mamlaka ya kisiasa na kijamii, hapa na katika nchi zote zilizoathiriwa na vita na vurugu: sikieni kilio cha watu wenu wanaoita amani! Sote tujitoe katika huduma ya maisha, ya manufaa ya wote, ya maendeleo kamilifu ya watu wote. Na kwenu, Wakristo wa LMashariki ya Kati, raia kamili wa nchi hizi, ninarudia: ujasiri! Kanisa zima linawatazama kwa upendo na pongezi. Bikira Maria, Mama yetu wa Harissa, awalinde daima!
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here
