Papa Leo XIV Awasalimia Mahujaji Kutoka Tanzania: Toba, Wongofu na Utakatifu wa Maisha
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa wafungwa, maaskari magereza pamoja na wahudumu mbalimbali magerezani, Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 14 Desemba 2025, maarufu kama “Dominica Gaudete” Yaani “Dominika ya Furaha”; kama antifona ya mwanzo inavyohimiza kwa kusema: furahini katika Bwana siku zote; tena nasema furahini. Bwana yu karibu. Rej Flp 4:4,5 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya hitimisho la Jubilei ya wafungwa, askari magereza na wahudumu mbalimbali magerezani, iliyozinduliwa tarehe 12 Desemba 2025. Hii ni Dominika inayosimikwa katika imani, matumaini na furaha ya kungojea. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amekazia kuhusu: Umuhimu wa Jubilei, Changamoto za magereza, wajibu wa kinabii magerezani, msamaha na matumaini kwa wafungwa. Katika maadhimisho haya, Mahujaji 49 kutoka Tanzania wameshiriki katika Ibada hii ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakiwa wamesindikizana na Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita, Askofu Lazarus Vitalis Msimbe wa Jimbo Katoliki Morogoro; Askofu Eusebio Samwel Kyando wa Jimbo Katoliki la Njombe pamoja na Askofu Anthony Gaspar Lagwen wa jimbo Katoliki Mbulu. Katika msafara huu kuna Mapadre 12, waamini walei 33 pamoja na mtawa mmoja.
Lengo kuu ni kuweza kujichotea neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa katika Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa kupitia katika Malango ya Makanisa Makuu ya Hija, Mjini Roma. Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kukumbatia toba, wongofu na utakatifu wa maisha. Huu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, haki na amani, daima wakimwangalia Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji toba, msamaha, amani na utulivu wa ndani. Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Katika hija hii, Mahujaji kutoka Tanzania wanatembelea Makanisa Makuu ya hija yaliyoko mjini Roma, na Assisi kwa Mtakatifu Francisko. Mahujaji hawa watamtembelea Mtakatifu Rita wa Cascia aliyezaliwa kunako mwaka 1381 huko Roccaporena. Akafariki dunia tarehe 22 Mei 1457 na kutangazwa kuwa Mtakatifu hapo tarehe 24 Mei 1900 na Baba Mtakatifu Leo XIII. Ni mwanamke wa shoka, aliyeweza kuvumilia ndoa shuruti kwa muda wa miaka 18, akiwa anamwombea mumewe ili aweze kutubu na kuongoka!
Katika kumbukumbu ya miaka 18 ya ndoa yao, mumewe akauwawa kikatili katika ugomvi! Kifo hiki kiliacha machungu katika familia ya Mtakatifu Rita, ambaye, watoto wake walitaka kulipiza kisasi, ili “kumwonesha cha mtema kuni” yule aliyesababisha kifo cha baba yao! Mawazo haya yakeleta majonzi makubwa tena katika maisha ya Mtakatifu Rita wa Cascia, akawaombea watoto wake ili wasilipize kisasi, akafanikiwa na watoto hawa wakawa ni mashuhuda wa huruma na msamaha katika maisha yao, kiasi hata cha kuitupa mkono dunia wakiwa katika hali ya neema!Katika hali ya upweke na majonzi makuu, Rita wa Cascia akajiunga na maisha ya kitawa, akawa kweli ni chemchemi ya huruma na upendo kwa jirani pamoja na watawa wenzake. Mkazo kwa waamini ni kuhusu: Umuhimu wa kusamehe na kusahau pamoja na kupenda Msalaba, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa: Hekima, huruma, upendo na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Mtakatifu Rita wa Cascia anakumbukwa na wengi kama mwombezi wa mambo yaliyoshindikana. Katika maisha na wito wake, daima alijiaminisha katika ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu! Baba Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, utakatifu wa Mtakatifu Rita wa Cascia unafumbatwa katika maisha yake ya kila siku, kama: Mama wa familia; mjane na hatimaye kama mtawa mmonaki wa Shirika la Mtakatifu Augustino. Mahujaji kutoka Tanzania wanahitimisha hija yao ya maisha ya kiroho tarehe 19 Desemba 2025.
