Papa Leo XIV:Historia yenu ni chanzo cha lishe ya safari ngumu kuelekea mstakabali

Papa Leo kabla ya kuondoka kurudi alitoa hotuba yake ya mwisho akielezea matukio yote aliyofanya akiwa nchini Lebanon.Nyinyi ni wenye nguvu kama mierezi inayojaa milima yenu mizuri, na mna matunda kama miti ya mizeituni inayokua katika nyanda,kusini na karibu na bahari.Tutambue kwamba mapambano ya silaha hayaleti faida yoyote.Ingawa silaha ni hatari,mazungumzo,upatanisho ni ya kujenga.Sote tuchague amani kama njia,na si kama lengo tu.

Na Angella Rwezaula - Vatican.

Baba Mtakatifu aliwahutubia Rais, Spika wa Bunge,wakuu wa Baraza Mawaziri, Patriaki na Maaskofu, Mamlaka za kiraia na kidini, katika Uwanja wa Ndege, Jumanne tarehe 2 Desemba 2025 kabla ya kuanza safari ya kurudi Roma baada ya Ziara yake ya kitume nchini Lebanon. Papa akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Papa alisema:  “Kuondoka mara nyingi ni vigumu zaidi kuliko kufika. Tumetumia muda pamoja, na hapa Lebanon, roho hii ya kukutana inaambukiza.

Papa katika kilele cha kuagwa huko Lebanon
Papa katika kilele cha kuagwa huko Lebanon   (@Vatican Media)

Papa aliendelea kusema kuwa "Hapa, nimegundua kuwa watu hufurahia kukutana pamoja, badala ya kutengwa. Ingawa kufikakatika nchi yenu kulimaanisha kuingia kwa upole katika utamaduni wenu, kuondoka katika nchi hii kunamaanisha kuwabeba moyoni mwangu.” Kwa hivyo, Papa aliongeza "hatuachani; badala yake, baada ya kukutana, tutasonga mbele pamoja. Tunatumaini kuhusisha Mashariki ya Kati nzima katika roho hii ya udugu na kujitolea kwa amani, ikiwa ni pamoja na wale ambao kwa sasa wanajiona kuwa maadui. "

Papa Leo XIV kadhalika alisema kuwa “kwa hivyo, ninashukuru kwa siku nilizotumia nanyi, na ninafurahi kwamba ningeweza kutimiza hamu ya mtangulizi wangu mpendwa, Papa Francisko, ambaye angependa kuwa hapa. Kiukweli, yuko pamoja nasi, akitembea nasi pamoja na mashahidi wengine wa Injili wanaotusubiri katika kumbatio la milele la Mungu."

Nyimbo za kitaifa
Nyimbo za kitaifa   (@Vatican Media)

"Sisi ni warithi wa kile walichoamini, imani, tumaini na upendo uliowatia moyo. Nimeona heshima kubwa ambayo watu wako wanayo kwa Bikira Maria, ambaye anapendwa na Wakristo na Waislamu pia. Nilisali kwenye kaburi la Mtakatifu Charbel na nikahisi mizizi ya kiroho ya nchi hii. Historia yenu ni chanzo muhimu cha lishe kinachoweza kuwategemeza katika safari ngumu kuelekea siku zijazo! Papa kadhalika alisisitiza kuwa “Niliguswa sana na ziara yangu fupi katika Bandari ya Beirut, ambapo mlipuko uliharibu eneo hilo, bila kusahau maisha ya watu wengi.

Rais wa Lebanon akimuaga
Rais wa Lebanon akimuaga   (@Vatican Media)

Papa alisema kuwa "Niliomba kwa ajili ya waathiriwa wote, na ninabeba maumivu, na kiu ya ukweli na haki, ya familia nyingi, ya nchi nzima. Katika siku hizi chache, nimekutana na watu wengi na kupeana mikono na watu wengi, nikipokea hisia ya matumaini kutokana na mikutano hii. Nyinyi ni wenye nguvu kama mierezi inayojaa milima yenu mizuri, na mna matunda kama miti ya mizeituni inayokua katika nyanda, kusini na karibu na bahari."

Katika suala hili,  Papa Leo alisema "ninawasalimu maeneo yote ya Lebanon ambayo sikuweza kutembelea: Tripoli na kaskazini, Beqaa na kusini mwa nchi, Tyro, Sidone, maeneo ya Kibiblia, maeneo yote na hasa kusini ambayo kwa sasa yanakabiliwa na hali ya migogoro na kutokuwa na uhakika. Kwa kuwakumbatia nyote, ninaelezea hamu yangu ya amani, pamoja na wito wa kutoka moyoni: mashambulizi na uadui vikome."

Chenye mwanzo kina mwisho wanaagana na mwenyeji wake
Chenye mwanzo kina mwisho wanaagana na mwenyeji wake   (@Vatican Media)

Hatimaye Papa wa Roma alisema kuwa "Lazima tutambue kwamba mapambano ya silaha hayaleti faida yoyote. Ingawa silaha ni hatari, mazungumzo, upatanisho na mazungumzo ni ya kujenga. Sote tuchague amani kama njia, na si kama lengo tu! Tukumbuke kile ambacho Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alithibitisha tena alipokuwa katikati yenu: Lebanon ni zaidi ya nchi; ni ujumbe! Tujifunze kufanya kazi pamoja na kutumaini pamoja, ili hili liweze kuwa kweli. Mungu awabariki watu wa Lebanon, nyote, Mashariki ya Kati na wanadamu wote! Shukran, ila al-liqa’!"

Papa akiagwa na kuondoka kurudi Roma

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

 

02 Desemba 2025, 13:04