“Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo” (Yn 14:27). Hii ndiyo amani tunayoiomba kwake kwa maombi yetu yenye uchaji. “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo” (Yn 14:27). Hii ndiyo amani tunayoiomba kwake kwa maombi yetu yenye uchaji.  

Papa Leo XIV: Jengeni na Kudumisha Haki na Amani

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Lebanon kuanzia tarehe 30 Novemba hadi tarehe 2 Desemba 2025 imeongozwa na kauli mbiu “Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Mt. 5:9. Baba Mtakatifu amewataka watu wa Mungu nchini Lebanon kujikita kikamilifu katika kutafuta na kudumisha haki na amani hata kati kati ya mtutu wa bunduki na kwamba, hii ni changamoto endelevuu dhidi ya: chuki, kiburi, utawala wa mabavu, utengano na uhasama

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Amani inasimikwa katika misingi ya ukweli, haki, upendo na uhuru kamili mambo yanayofafanuliwa katika Waraka wa Kitume wa “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” uliochapishwa na Mtakatifu Yohane XXIII. Anasema, kuna kazi kubwa sana juu ya watu wote wenye mapenzi mema: kazi ya kurudisha mahusiano ya maisha ya kawaida ya wanadamu katika ukweli, katika haki, katika upendo, katika uhuru: mahusiano ya maisha ya kawaida ya wanadamu kati ya watu binafsi; kati ya raia na jumuiya zao za kisiasa; kati ya jumuiya zenyewe za kisiasa kati yao; kati ya watu binafsi, familia, taasisi za kati na jumuiya za kisiasa, kwa upande mmoja, na jumuiya ya dunia nzima, kwa upande mwingine. Hii ni kazi nzuri sana, sawa na ile ya kutekeleza amani ya kweli katika utaratibu uliowekwa na Mungu. Ni amri katika kuwajibika; ni dai katika upendo. Kila mwamini, katika dunia yetu hii, anatakiwa kuwa cheche ya nuru, mahali pa upendo, chachu inayoleta uhai katika umati wa watu: na atakuwa hivyo kweli, akizidi, rohoni mwake, kuishi katika ushirika na Mungu. Maana, hakuna amani kati ya wanadamu kama amani haimo ndani ya kila mmoja wao, yaani kama kila mmoja hazitii ndani yake taratibu zinazotakwa na Mungu. “Nafsi yako – anajiuliza Mtakatifu Augustino – inataka kushinda tamaa zako mbaya? Imtii yule aliye juu na itakishinda kilicho chini. Na ndani yako mtakuwa na amani: ya kweli, ya uhakika, iliyoratibika vizuri sana. Ni upi utaratibu wa amani hiyo? Mungu huiamuru nafsi, nafsi huuamuru mwili; hakuna kitu kilichoratibika vizuri zaidi.”

Papa leo XIV: Jengeni na kudumisha haki na amani
Papa leo XIV: Jengeni na kudumisha haki na amani   (AFP or licensors)

Kristo Yesu ni Mfalme wa amani inayosimikwa katika: haki, inayopata uhai kutoka katika upendo na utekelezwao katika uhuru. Ili jamii ya wanadamu iweze kuwa ni kioo safi inayoakisi vizuri Ufalme wa Mungu, msaada kutoka juu unahitajika. Kwa sababu hiyo, dua zetu, siku hizi takatifu, zinapanda kwa ari zaidi kwa yule aliyeshinda dhambi katika mateso na kifo chake; dhambi ambayo inasambaratisha watu na kuleta misiba, fitina na kukosa usawa; kwake Yeye ambaye amewapatanisha wanadamu na Baba wa mbinguni katika damu yake: “Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja… Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu” (Efe 2:14.17.) “Bwana wetu Yesu Kristo baada ya kufufuka akakaa katikati ya wanafunzi wake na kusema: Amani iwe kwenu. Na wanafunzi walifurahi walipomwona Bwana.” Yeye anatupa amani, yeye analeta amani: “Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo” (Yn 14:27). Hii ndiyo amani tunayoiomba kwake kwa maombi yetu yenye uchaji. Aweke mbali na moyo wa watu yale yanayoihatarisha; na awageuze watu, wawe mashuhuda wa ukweli, haki, na upendo wa kindugu. Awaangaze viongozi wa Mataifa, ili pamoja na kujali: utu, heshima, haki msingi, ustawi wa raia wao walinde na kutetea tunu kubwa ya amani; auchochee utashi wa wote ili kuvuka mipaka inayotenganisha, ili kukuza vifungo vya upendano, ili kuwaelewa wengine, ili kuwasamehe wale waliotenda maovu; kwa sababu ya nguvu ya amani Mataifa yote ya dunia yawe kama ndugu na ndani yao ikue na itawale daima amani inayotamaniwa sana.

Heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu
Heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu   (ANSA)

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Lebanon kuanzia tarehe 30 Novemba hadi tarehe 2 Desemba 2025 imeongozwa na kauli mbiu “Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.” Mt. 5:9. Baba Mtakatifu amewataka watu wa Mungu nchini Lebanon kujikita kikamilifu katika kutafuta na kudumisha haki na amani hata kati kati ya mtutu wa bunduki na kwamba, hii ni changamoto endelevu. Baba Mtakatifu Benedikto XVI wakati wa hija yake ya kitume nchini Lebanon 14 Septemba 2002 aliwataka watu wa Mungu kuadhimisha ushindi wa upendo dhidi ya chuki na uhasama; msamaha dhidi ya kutaka kulipiza kisasi; huduma dhidi ya utawala wa mabavu; unyenyekevu dhidi ya kiburi; umoja dhidi ya utengano; waamini wawe tayari kugeuza mateso na mahangaiko yao kuwa ni kilio cha upendo kwa Mungu na huruma kwa jirani.

Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa Mungu. Mt 5:9
Heri wapatanishi; maana hao wataitwa wana wa Mungu. Mt 5:9   (AFP or Licensors)

Baba Mtakatifu ameendelea kuwahimiza watu wa Mungu kujenga majadiliano katika upendo, ili kurejesha tena umoja kamili kati ya Wakristo. Tajiriba ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1700 ya Mtaguso Mkuu wa Nicea iwe ni chachu ya kutembea kwa pamoja katika ukweli na urafiki, kwa kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu. Kuna haja ya waamini wa dini mbalimbali kuendelea kujikita katika wongofu wa kiikolojia, ili kulinda na kudumisha mazingira bora, kwa kufanya kazi kwa ushirikiano, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Uturuki inayo nafasi ya pekee huko Mashariki ya Kati katika mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha amani na kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwa watu hata katika tofauti zao msingi kuweza kuishi kwa amani na maridhiano.

Papa Leo XIV Haki na Amani
02 Desemba 2025, 14:18