Papa Leo,Misa:Kuvua silaha mioyoni ndiyo njia pekee ya kuleta umoja Lebanon

Katika Misa kwenye Ufukwe wa Beirut,Papa Leo XIV alitoa shukrani kwa siku za ziara yake ya kwanza ya kitume,ambapo alikutana na mateso na matumaini ya watu aliokutana nao."Ninafikiria imani yenu ya dhati na ya kweli,familia zenu na kulishwa na shule za Kikristo,kazi ya parokia,mashirika na harakati ili kukidhi maswali na mahitaji ya watu,Mapadre wengi na watawa wanaojitolea kwa utume wao katikati ya matatizo mengi na watu wa kawaida waliojitolea kwa kazi za upendo na kukuza Injili katika Jamii.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa katika Ziara yake ya Kitume nchini Lebanon, aliongoza ibada ya Misa iliyofanyika katika Fukwe ya Beirut, Jumatano tarehe 2 Desemba 2025 kabla ya kuhitimisha Ziara yake ya Kwanza nchini humo. Misa ilikuwa na mguso kuona waamini wapatao 120,000 wakisherehekea na kupeperusha bendera za nchi yao lakini pia ya Vatican. Miongoni mwa waliohudhuria alikuwa Rais wa Lebanon Joseph Aoun na mkewe, Nehmat na viongozi wengine wengi wa Taifa. Kabla ya Misa Papa aliwazungukia akiwasalimia. Ilifuatiwa misa na masomo. Na akianza mahubiri Papa alisema Mwishoni mwa siku hizi kali, ambazo tumeshiriki pamoja kwa furaha, tunamshukuru Bwana kwa zawadi nyingi za wema wake, uwepo wake kati yetu, Neno analotupatia kwa wingi na kwa kuturuhusu kuwa pamoja. Kama tulivyosikia tu katika Injili, Yesu pia alikuwa na maneno ya shukrani kwa Baba na, akimgeukia, akaomba: “Ninakusifu, Baba, Bwana wa mbingu na dunia” (Lk 10:21).

Papa Leo akitoa Baraka
Papa Leo akitoa Baraka   (@Vatican Media)

Hata hivyo, sifa hazipati nafasi kila wakati ndani yetu. Wakati mwingine, tukiwa tumelemewa na mapambano ya maisha, tukiwa na wasiwasi kuhusu matatizo mengi yanayotuzunguka, tukiwa tumedhoofika kwa kutokuwa na nguvu mbele ya uovu na kukandamizwa na hali nyingi ngumu, tuna mwelekeo zaidi wa kujisalimisha na kuomboleza kuliko kushangaa na kushukuru.“Wapendwa watu wa Lebanon, ninawaalika kukuza tabia ya sifa na shukrani kila wakati. Ninyi ni wapokeaji wa uzuri adimu ambao Bwana ameupamba nchi yenu. Wakati huo huo, ninyi ni mashahidi na waathiriwa wa jinsi uovu, katika aina zake mbalimbali, unavyoweza kuficha fahari hii. Kutoka kwenye Uwanja huu mkubwa wa ufukwe unaoelekea bahari, mimi pia ninaweza kutafakari uzuri wa Lebanon unaoimbwa katika Maandiko. Bwana alipanda mierezi yake mirefu hapa, akiilisha na kuinywesha (taz. Zab 104:16).

Misa Takatifu katika fukwe za Beiruti
Misa Takatifu katika fukwe za Beiruti   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa aliyafanya mavazi ya bibi arusi katika Wimbo Ulio Bora kuwa na harufu nzuri ya manukato ya nchi hii (taz. 4:11), na katika Yerusalemu, mji mtakatifu uliovaa nuru kwa ajili ya kuja kwa Masihi, alitangaza: “Utukufu wa Lebanoni utakujia, mti wa mvinje, mti wa pine, ili kupamba mahali pangu patakatifu, nami nitapatukuza mahali pa miguu yangu” (Isaya 60:13). Hata hivyo, uzuri huu umefunikwa na umaskini na mateso, majeraha ambayo yameashiria historia yako. Katika suala hili, nimetembelea bandari ili kuomba mahali pa mlipuko. Uzuri wa nchi yako pia umefunikwa na matatizo mengi yanayokusumbua, muktadha dhaifu na mara nyingi usio imara wa kisiasa, mgogoro mkubwa wa kiuchumi unaokulemea na vurugu na migogoro ambayo imeamsha hofu za kale.

Katika hali kama hiyo, shukrani huacha njia kwa urahisi ya kukata tamaa, nyimbo za sifa hazipati nafasi katika ukiwa wa moyo na tumaini hukaushwa na kutokuwa na uhakika na mkanganyiko. Hata hivyo, neno la Bwana linatualika kutafuta taa ndogo zinazong'aa katikati ya usiku, ili kujifungua kwa shukrani na kututia moyo katika ahadi ya pamoja kwa ajili ya nchi hii. Kama tulivyosikia, sababu ya Yesu kumshukuru Baba si kwa kazi zake za ajabu, bali ni kwa sababu anafunua ukuu wake haswa kwa wadogo na kwa wanyenyekevu, kwa wale ambao hawavutii umakini na wanaonekana kuhesabiwa kwa kidogo au chochote na hawana sauti.

Waamini katika misa
Waamini katika misa   (@Vatican Media)

Ufalme ambao Yesu anakuja kuuzindua unaoneshwa, kiukweli, na sifa ile ile iliyoelezwa na nabii Isaya: ni chipukizi, tawi dogo linalochipuka kutoka kwenye shina (taz. Isaya 11:1). Ni ishara ndogo ya tumaini inayoahidi kuzaliwa upya wakati kila kitu kingine kinaonekana kufa. Hakika, kuja kwa Masiha kulitangazwa kwa udogo wa chipukizi, kwa sababu anaweza kutambuliwa tu na wadogo, na wale ambao kwa unyenyekevu wanajua jinsi ya kutambua maelezo na alama zilizofichwa za Mungu katika historia inayoonekana kupotea. Pia ni ishara kwetu, ili tuwe na macho yenye uwezo wa kutambua udogo wa chipukizi unaoibuka na kukua hata katikati ya kipindi kigumu.

Hata hapa na sasa, tunaweza kuona taa ndogo zinazong'aa usiku, machipukizi madogo yanayochipuka na mbegu ndogo zilizopandwa katika bustani kame katika enzi hii ya historia. Papa Leo alieleza kuwa “Ninafikiria imani yenu ya dhati na ya kweli, iliyojikita katika familia zenu na kulishwa na shule za Kikristo. Ninafikiria kazi ya mara kwa mara ya parokia, makutaniko na harakati ili kukidhi maswali na mahitaji ya watu. Ninafikiria mapadre wengi na watawa wanaojitolea kwa utume wao katikati ya matatizo mengi, na watu wa kawaida waliojitolea kwa kazi za upendo na kukuza Injili katika jamii. Kwa ajili ya taa hizi zinazojitahidi kuangazia giza la usiku, na kwa ajili ya chipukizi hizi ndogo na zisizoonekana ambazo hata hivyo hufungua matumaini kwa ajili ya wakati ujao, leo tunaungana na Yesu kusema: “Tunakusifu, Baba!”

Misa huko Beirut
Misa huko Beirut   (@Vatican Media)

Tunakushukuru kwa sababu uko pamoja nasi na usituache tufe moyo. Wakati huo huo, shukrani hii haipaswi kubaki kama faraja ya kujitafakari na ya udanganyifu. Lazima ituongoze kwenye mabadiliko ya moyo, uongofu wa maisha na utambuzi kwamba Mungu ametufanya tuishi katika nuru ya imani, ahadi ya matumaini na furaha ya upendo. Kwa hivyo, sote tumeitwa kukuza chipukizi hizi, tusikate tamaa, tusianguke katika mantiki ya vurugu na ibada ya sanamu ya pesa, na tusiache kujisalimisha mbele ya uovu unaoenea. Kila mtu lazima afanye sehemu yake, na lazima tuunganishe juhudi zetu ili nchi hii iweze kurudi kwenye utukufu wake wa zamani. Kuvua silaha mioyoni mwetu ndiyo njia pekee ya kufanya hivi.

Tutupilie mbali silaha za mgawanyiko wetu wa kikabila na kisiasa, tufungue madhehebu yetu ya kidini ili tukutane pamoja na kuamsha mioyoni mwetu ndoto ya Lebanon iliyoungana. Lebanon ambapo amani na haki hutawala, ambapo sote tunatambuana kama kaka na dada, na, hatimaye, ambapo maneno ya nabii Isaya yanaweza kutimizwa: "Mbwa mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, chui atalala pamoja na mwana-mbuzi, ndama na simba watalisha pamoja"(Is 11:6). Hii ndiyo ndoto uliyokabidhiwa; ndiyo Mungu wa amani anayoweka mikononi mwako. Lebanon, simama! Kuwa makao ya haki na udugu! Kuwa ishara ya kinabii ya amani kwa Walawi wote! Kaka na dada, mimi pia ningependa kurudia maneno ya Yesu: "Ninakusifu, Baba." Ninamshukuru Bwana kwa kushiriki siku hizi nanyi. Ninapobeba mateso na matumaini yenu moyoni mwangu, naomba kwamba nchi hii ya Levanti iangazwe kila wakati na imani katika Yesu Kristo, jua la haki. Vile vile naomba kwamba kupitia neema ya Kristo, Lebanon idumu katika tumaini hilo ambalo halikatishi tamaa.

Misa huko Beirut
02 Desemba 2025, 12:38