Papa Leo XIV,Mkutano wa kiekumeni:Umoja,maridhiano na amani vinawezekana

Katika Mkutano wa Kiekumeni na kidini kwenye Uwanja wa mashahidi huko Beirut,Desemba 1,Papa Leo XIV aliwatia moyo watu Walebanon na kutoa wito ili kukabiliana na kutovumilia,kushinda vurugu na ubaguzi.Akinukuu tamko la Nostra Aetate,alihimiza uvumilivu katika kujenga nchi iliyojengwa juu ya heshima na mazungumzo.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV akiwa katika ziara yake ya Kitume nchini Lebanon na siku yake ya Pili nchini humo, Jumatatu tarehe 1 Desmba 2025 alishiriki alasiri Mkutano wa kiekumeni na kidini katika Uwanja wa Mashahidi huko Beirut. Kwa kufuata nyayo za mapapa waliomtangulia, Baba wa Kanisa la Ulimwengu  akiwa katika Moyo wa Mashariki ya Kati ambayo inatunza dini Tatu za Baba wa Mataifa Ibrahimu, aliwasikiliza kidugu, mmoja baada ya mwingine, waliotangulia kusali na kutoa hotuba zao.

Mkutano wa Kiekumene na Kidini
Mkutano wa Kiekumene na Kidini   (@Vatican Media)

Tukio hilo lilifuatia mara baada ya mkutano katika Ubalozi wa Vatican  wa Baraza la Mapatriaki wa Kanisa Katoliki la Mashariki, ambapo, miongoni mwa mambo mengine yaliyozungumzwa ni tarehe ya kawaida ya Pasaka kwa Wakristo wote na chakula cha mchana katika ukumbi huo huo kilifuatiwa,  kilichohudhuriwa na Aram I, Patriaki wa Kanisa la Mitume la Armenia ya Kilikia; Patriaki wa Antiokia na mkuu wa Kanisa la Kiorthodox la kisyria Ignatius Ephrem II, na Patriaki wa Kiorthodox wa Kigiriki wa Antiokia Yohane  X Yazigi.

Mkutano wa kiekumene na kidini
Mkutano wa kiekumene na kidini   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu katika hotuba yake  alianza kueleza alivyoguswa sana na kushukuru sana kusimama miongoni mwao siku hiyo, katika nchi hiyo iliyobarikiwa, nchi iliyoinuliwa na manabii wa Agano la Kale, ambao waliona katika mierezi yake mirefu alama za roho ya haki inayostawi chini ya macho ya mbinguni; nchi ambapo mwangwi wa Logos haujawahi kunyamaza, lakini unaendelea kuwaita, kutoka karne hadi karne, wale wanaotamani kufungua mioyo yao kwa Mungu aliye hai.

Katika Wosia wake wa Kitume wa Baada ya Sinodi Ecclesia in Medio Oriente, uliosainiwa hapo Beirut mnamo 2012, Papa Benedikto  XVI alisisitiza kwamba “asili ya Kanisa kwa ujumla na wito wake unahitaji kwamba lishiriki katika mazungumzo na washiriki wa dini zingine. Katika Mashariki ya Kati, mazungumzo haya yanategemea vifungo vya kiroho na kihistoria vinavyowaunganisha Wakristo na Wayahudi na Waislamu. Ni mazungumzo ambayo hayaamriwi kimsingi na mambo ya vitendo, kisiasa au kijamii, bali na masuala ya kitaalimungu yanayohusiana na imani” (n. 19).

Incontro ecumenico e interreligioso

Mkutano wa Kiekumeni na kidini(@Vatican Media)

Kwa miaka mingi, na hasa katika siku za hivi karibuni, macho ya ulimwengu yameelekezwa Mashariki ya Kati, chimbuko la dini za Ibrahimu, yakiangalia safari ngumu na utafutaji usiokoma wa zawadi ya thamani ya amani. Wakati mwingine ubinadamu huitazama Mashariki ya Kati kwa hisia ya hofu na kukata tamaa, mbele ya migogoro hiyo migumu na ya muda mrefu. Hata hivyo, katikati ya mapambano haya, hisia ya matumaini na kutiwa moyo inaweza kupatikana tunapozingatia kile kinachotuunganisha: ubinadamu wetu wa kawaida, na imani yetu kwa Mungu wa upendo na huruma. Katika enzi ambayo kuishi pamoja kunaweza kuonekana kama ndoto ya mbali, watu wa Lebanon, huku wakikumbatia dini tofauti, wanasimama kama ukumbusho wenye nguvu kwamba hofu, kutoaminiana na ubaguzi hazina neno la mwisho, na kwamba umoja, maridhiano na amani vinawezekana.

Ni dhamira ambayo haijabadilika katika historia ya nchi hii pendwa: kushuhudia ukweli unaodumu kwamba Wakristo, Waislamu, Druze na wengine wengi wanaweza kuishi pamoja na kujenga nchi iliyounganishwa kwa heshima na mazungumzo. Miaka sitini iliyopita, Mtaguso wa Pili wa Vatican pamoja na kutangazwa kwa Tamko la Nostra Aetate, ulifungua upeo mpya wa kukutana na kuheshimiana kati ya Wakatoliki na watu wa dini tofauti, ukisisitiza kwamba mazungumzo ya kweli na ushirikiano vimejikita katika upendo - msingi pekee wa amani, haki na upatanisho. Mazungumzo haya, yaliyoongozwa na upendo wa kimungu, yanapaswa kuwakumbatia watu wote wenye nia njema, kukataa ubaguzi, ubaguzi na mateso, na kuthibitisha heshima sawa ya kila mwanadamu.

Walioudhuria mkutano wa kiekumeni na kidini
Walioudhuria mkutano wa kiekumeni na kidini   (@Vatican Media)

Ingawa huduma ya umma ya Yesu ilijitokeza hasa Galilaya na Yudea, Injili pia zinasimulia matukio ambapo alitembelea eneo la Dekapoli, hasa katika mazingira ya Tiro na Sidoni - ambapo alikutana na mwanamke Msiria-Foinike ambaye imani yake isiyoyumba ilimsukuma kumponya binti yake(taz. Mk 7:24-30). Hapa, nchi yenyewe inakuwa zaidi ya mahali pa kukutana tu kati ya Yesu na mama anayeomba; inakuwa mahali ambapo unyenyekevu, uaminifu, na uvumilivu hushinda vizuizi vyote na kukutana na upendo usio na mipaka wa Mungu unaokumbatia kila moyo wa mwanadamu. Hakika, huu ndio "msingi wa mazungumzo ya kidini yenyewe: ugunduzi wa uwepo wa Mungu zaidi ya mipaka yote na mwaliko wa kumtafuta pamoja kwa heshima na unyenyekevu."

Ikiwa Lebanon inajulikana kwa mierezi yake mizuri, mti wa mzeituni pia unasimama kama jiwe la msingi la urithi wake. Mzeituni haupambi tu nafasi hii tunayokusanyika leo, lakini pia unaheshimiwa katika maandishi matakatifu ya Ukristo, Uyahudi na Uislamu, ukitumika kama ishara isiyo na kikomo ya upatanisho na amani. Maisha yake marefu na uwezo wake wa ajabu wa kustawi hata katika mazingira magumu zaidi yanaashiria uvumilivu na matumaini, yakionyesha kujitolea kwa dhati kunakohitajika ili kukuza kuishi pamoja kwa amani. Kutoka kwenye mti huu hutiririka mafuta yanayoponya - dawa ya maumivu ya kimwili na kiroho - yanayoonesha huruma isiyo na kikomo ya Mungu kwa wote wanaoteseka. Mafuta yake pia hutoa mwanga, yakitumika kama ukumbusho wa wito wa kuangazia mioyo yetu kupitia imani, upendo na unyenyekevu.

Nella tenda in piazza dei Martiri

Viongozi wa Kiekuemeni na kidini katika Hema kwenye Uwanja wa Mashahidi(@Vatican Media)

Kama mizizi ya mierezi na mizeituni inavyozama ndani na kuenea kote duniani, ndivyo pia watu wa Lebanon wanavyotawanyika kote ulimwenguni, lakini wamefungwa pamoja na nguvu ya kudumu na urithi usio na mwisho wa nchi yenu. Uwepo wenu hapa na kote ulimwenguni unaimarisha ulimwengu na urithi wenu wa milenia nyingi, lakini pia unawakilisha wito. Katika ulimwengu unaozidi kuunganishwa, mmeitwa kuwa wajenzi wa amani: kukabiliana na kutovumiliana, kushinda vurugu na kuondoa kutengwa, kuakisi njia ya haki na maelewano kwa wote, kupitia ushuhuda wa imani yenu.

Papa Leo XIV aidha alisema kuwa tarehe 25 Machi kila mwaka, ikiadhimishwa kama siku kuu ya kitaifa nchini mwao  wanakusanyika pamoja kumsifu Maria, Mama Yetu wa Lebanon, anayeheshimiwa katika madhabahu huko Harissa, ambayo imepambwa kwa sanamu ya kuvutia ya Bikira kwa mikono iliyonyooshwa, ikiwakumbatia watu wote wa Lebanon. Kumbatio hilo la upendo na la kimama la Bikira Maria, Mama wa Yesu na Malkia wa Amani, liwaongoze kila mmoja wao, ili katika nchi yao na  Mashariki ya Kati  yote na ulimwenguni kote, zawadi ya upatanisho na kuishi pamoja kwa amani ipate kutiririka “kama vijito vinavyotiririka kutoka Lebanon” (tazama Wimbo 4:15). Walete matumaini na umoja kwa wote. Shukran.

La piantumazione dell'olivo

Kupanda Mti wa Mzeituni pamoja viongozi watatu wa dini za Ibarahimu(@Vatican Media)

Mkutano ulihitimishwa na watoto wakiimba, ambao walihuisha sherehe hiyo kwa muziki wao mtamu. Papa aliendelea kupanda na kumwagilia mzeituni, ishara nyingine ya kutamani amani na utunzaji wa nyumba yetu ya pamoja. Pembeni mwake alikuwa Sheikh Al-Aql wa jumuiya ya Druze, Sami Abi Al-Muna, na Patriaki wa Kiorthodox wa Ugiriki wa Antiokia, Yohanna X Yazigi. Ikumbukwe tarehe 30 Novemba Papa alitarajiwa kushiriki katika upandaji wa "mwerezi wa urafiki" katika bustani za Ikulu ya Rais. Hata hivyo, hali mbaya ya hewa ililazimisha sherehe hiyo kufanyika ndani ya nyumba, huku mti mchanga ukimwagiliwa maji. Ishara hiyo ilidumisha thamani yake ya mfano, ikikumbusha hitaji la kulinda urithi wa asili uliodumu kwa karne nyingi.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here

 

01 Desemba 2025, 18:27