Papa Leo XIV:Wenye nguvu hawasikilizi kilio cha Dunia na Maskini
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika Katekesi ya Mwisho ya Jubilei, iliyoanzishwa Januari iliyopita na Papa Francisko, Baba Mtakatifu Leo XIV anawasihi waamini kukumbuka kwamba wakati Jubilei inakaribia kuisha, "tumaini haliishi", kwamba Mwaka Mtakatifu umetimiza, na hivyo safari ya waamini inaendelea. Kwa njia hiyo Katekesi yake ya Jumamosi tarehe 20 Desemba 2025 akiwageukia waamini na mahujaji waliofika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, alisisitiza kwamba watu wengi wenye nguvu hushindwa kusikiliza kilio cha uumbaji na kwamba matajiri wa dunia wanazidi kujilimbikizia, bila haki, mikononi mwa wachache. Mungu amekusudia mali za uumbaji kwa ajili ya wote ili wote waweze kushiriki katika hizo. Kazi yetu ni kuzalisha, si kuiba. Kinachotishia na kuua si nguvu: ni kiburi, ni hofu kali, ni uovu usiozalisha chochote. Nguvu ya Mungu huzaa.
Hata hivyo kabla ya kuanza katekesi hiyo iliyoongozwa na Mada: kutumaini ni kuzalisha. Maria, Tumaini letu. Papa aliwasili katika Uwanja wa Mtakatifu Petro muda mfupi baada ya saa 4:00 asubuhi na, akiwa juu kigari chake nyeupe, akiwasalimia wale waliofika kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wakipunga bendera na kauli mbiu. Baadhi walitoka Marekani, Argentina, na Hispania; kama ilivyo kawaida, Papa alisimama kuwabariki watoto na kuzungumza na vikundi kadhaa. Kwanza lilisomwa somo kutoka Mtakatifu Paulo kwa Warumi kwa lugha mbali mbali:
"Tunajua kwamba viumbe vyote vimekuwa vikiugua kwa uchungu wa uzazi hadi sasa. Na si hivyo tu, bali sisi wenyewe, tulio na malimbuko ya Roho, tunaugua ndani yetu, tukingojea kwa hamu kufanywa wana, yaani, ukombozi wa miili yetu, kwa maana katika matumaini tuliokolewa,(Rm 8, 22-24)."
Papa alianza kuwasalimia habari za asubuhi na kuwakaribisha. Noeli inapokaribia, tunaweza kusema: Bwana yuko karibu! Bila Yesu, kauli hii, ya Bwana yuko karibu, inaweza kusikika kama tishio. Hata hivyo, katika Yesu, tunagundua kwamba, kama manabii walivyoelewa, Mungu ni tumbo la huruma. Mtoto Yesu anatufunulia kwamba Mungu ana moyo wa huruma, ambao huzalisha kila wakati. Ndani yake hakuna tishio, ila msamaha. Papa akiendelea alisema kuwa “Wapendwa, leo ni Katekesi ya mwisho ya Jubilei ya Jumamosi, iliyoanzishwa mnamo Januari iliyopita na Papa Francisko. Jubilei inakaribia kuisha, lakini tumaini ambalo Mwaka huu umetupatia haliishi: tutabaki kuwa mahujaji wa matumaini!”
Tumesikia kutoka kwa Mtakatifu Paulo: "Kwa maana katika tumaini tuliokolewa" (Rm 8:24). Bila tumaini, tumekufa; kwa tumaini, tunafika kwenye nuru. Tumaini huzalisha. Kiukweli, ni fadhila ya kitaalimungu, yaani, nguvu ya Mungu, na kwa hivyo, huzaa; haiui, bali huzaa na kuzaliwa upya. Hii ni nguvu ya kweli. Kinachotishia na kuua si nguvu: ni kiburi, ni hofu kali, ni uovu usiozalisha chochote. Nguvu ya Mungu huzaa. Hii ndiyo sababu Papa alipenda kuwambia hatimaye kwamba: "kutumaini ni kuzalisha." Papa Leo aliendelea kusema kuwa Mtakatifu Paulo anawaandikia Wakristo wa Roma jambo linalotufanya tufikiri: "Tunajua ya kuwa viumbe vyote vimekuwa vikilia na kuteseka pamoja kwa uchungu wa kuzaa hadi sasa" (Rm 8:22). Ni picha yenye nguvu sana. Inatusaidia kusikia na kupeleka maombi ya kilio cha dunia na kilio cha maskini. "Yote pamoja," uumbaji ni kilio. Lakini watu wengi wenye nguvu hawasikii kilio hiki: utajiri wa dunia uko mikononi mwa wachache, wachache sana, wanaozidi kujilimbikizia, bila haki, mikononi mwa wale ambao mara nyingi hawataki kusikia kilio cha dunia na maskini.”
Papa aliongeza kusema: “Mungu amekusudia mema ya uumbaji kwa wote, ili wote waweze kushiriki katika hayo. Kazi yetu ni kuzalisha, si kuiba. Lakini, kwa imani, maumivu ya dunia na maskini ni ya uzazi. Mungu huzalisha kila wakati, Mungu bado huumba, na tunaweza kuzalisha pamoja Naye, kwa matumaini. Historia iko mikononi mwa Mungu na wale wanaomtumaini. Hakuna wale wanaoiba tu, bali zaidi ya yote wale wanaozalisha.” Askofu wa Roma alieleza: " kaka na dada waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro kuwa “ ikiwa sala ya Kikristo ni ya Maria sana, ni kwa sababu katika Maria wa Nazareti tunaona mmoja wetu anayezalisha. Mungu alimfanya azae na akaja kwetu na sura zake, kama vile kila mtoto anavyofanana na mama yake. Yeye ni Mama wa Mungu na wetu." "Tumaini letu," tunasema katika (Salve Regina) yaani sala ya Salamu Malkia. Anafanana na Mwana, na Mwana anafanana naye. Nasi tunafanana na Mama huyu aliyetoa uso, mwili, na sauti kwa Neno la Mungu.
Tunafanana naye, kwa sababu tunaweza kuzalisha Neno la Mungu hapa chini, tukibadilisha kilio tunachosikia kuwa kuzaliwa. Yesu anataka kuzaliwa mara ya pili: tunaweza kumpa mwili na sauti. Huku ndiko kuzaliwa ambako uumbaji unasubiri. Kutumaini ni kuzalisha. Kutumaini ni kuona ulimwengu huu ukiwa ulimwengu wa Mungu: ulimwengu ambao Mungu, wanadamu, na viumbe vyote vinatembea pamoja tena, katika mji wa bustani, Yerusalemu mpya. Na Maria, tumaini letu, asindikize hija yetu ya imani na matumaini kila wakati.
Asante kwa kusoma makala haya. Ikiwa unataka kuendelea kupata taarifa mpya, tunakualika ujiandikishe kwa jarida kwa kubofya hapa: Just click here
