2025.12.02 Safari ya Kitume nchini Lebanon-Mkutano na waandishi wa habari katika ndege kutoka Beirut-Roma. 2025.12.02 Safari ya Kitume nchini Lebanon-Mkutano na waandishi wa habari katika ndege kutoka Beirut-Roma.  (@Vatican Media)

Papa Leo:‘Nilikuwa nafikiria kustaafu,badala yake nilijisalimisha kwa Mungu’

Ndani ya ndege ya Papa akirejea Roma kutoka Lebanon,Papa Leo XIV alizungumza na waandishi wa habari kuhusu jukumu la Vatican,ambalo hufanya kazi "nyuma ya pazia" katika mazungumzo ya amani,ili pande zote ziweze kuweka silaha chini.Kuhusu Ukraine,Papa alisisitiza ushiriki wa Ulaya na jukumu muhimu ambalo Italia inaweza kuchukua, na alijibu swali kuhusu jinsi alivyoitikia kuchaguliwa kwake katika Uchaguzi Mkuu na kuhusu hali yake ya kiroho:kutoa maisha ya mtu kwa Mungu na kumruhusu awe mkuu.

Vatican News

"Kwanza kabisa, ninataka kuwashukuru nyote mliofanya kazi kwa bidii; ningependa mpitishe ujumbe huu pia kwa waandishi wengine wa habari, wote huko Türkiye na Lebanon, ambao mmefanya kazi ya kuwasilisha ujumbe muhimu wa safari hii. Ninyi pia mnastahili pongezi kubwa kwa ziara hii." Ndivyo alianza Papa Leo XIV kuwasalimia waandishi wa habari 81 waliokuwa kwenye ndege kutoka Beirut hadi Roma kwa maneno hayo, kabla ya kujibu maswali kadhaa, akizungumza kwa Kiingereza, Kiitaliano na Kihispania.

Alizungumzia kuhusu Ziara yake ya Kitume iliyomalizika hivi punde, kuhusu Mashariki ya Kati, vita nchini Ukraine, uwepo wa Ulaya katika mazungumzo ya amani, na hali nchini Venezuela. Pia alipokea zawadi kutoka kwa mwandishi wa habari wa Lebanon: uchoraji uliotengenezwa kwa mkono, ulioundwa moja kwa moja kwenye televisheni katika siku za hivi karibuni, ukimwonesha yeye na maeneo ya mfano aliyotembelea katika Nchi ya Mierezi. Yafuatayo ni maswali na majibu ya Papa Leo XIV..

Joe Farchakh (LBC International): Wewe ni Papa wa Marekani unayeongoza mchakato wa amani. Swali langu ni kwamba utatumia mawasiliano yako na Rais Donald Trump na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu. Kwenye ndege, ulisema kwamba Vatican ni rafiki wa Israel. Je, utazungumzia suala la kukomesha uchokozi wa Israel dhidi ya Lebanon? Na je, amani endelevu inawezekana katika eneo hilo?

Papa Leo XIV, alijibu kwa Kiingereza: Kwanza kabisa, ndiyo, naamini amani endelevu inawezekana. Nadhani kwamba tunapozungumzia matumaini, tunapozungumzia amani, tunapotazama wakati ujao, tunafanya hivyo kwa sababu naamini inawezekana kwamba amani ije tena katika eneo hilo na kuja nchini mwenu, Lebanon. Kiukweli tayari, kwa njia ndogo sana, nimeanza mazungumzo machache na baadhi ya viongozi wa maeneo ambayo umeyataja, na ningekusudia kuendelea kufanya hivyo, kibinafsi au kupitia Kiti Kitakatifu, kwa sababu ukweli ni kwamba tuna uhusiano wa kidiplomasia na nchi nyingi kupitia eneo hilo, na itakuwa matumaini yetu hakika, kuendelea kutoa wito huo wa amani ambao nilizungumzia mwishoni mwa Misa leo.

Imad Atrach (Sky News Arabia): Katika hotuba yako ya mwisho, kulikuwa na ujumbe wazi kwa mamlaka za Lebanon kujadili. Kujadili, kuzungumza, kujenga. Je, Vatican itafanya jambo dhahiri katika suala hili? Jana usiku ulikutana na mwakilishi wa Shia. Kabla ya ziara yako, Hezbollah ilikutumia ujumbe; Sijui kama uliupokea, kama uliusoma. Unaweza kutuambia nini kuhusu hili? Asante sana kwa kutembelea Lebanon, ambayo ilikuwa ndoto kwetu.

Papa, alijibu kwa Kiitaliano: Kipengele kimoja cha safari hii, ambacho hakikuwa sababu kuu, kwani ziara hiyo ilibuniwa kwa kuzingatia maswali ya kiekumeni, kwa kuzingatia mada ya Nicea, mkutano na Mapatriaki Wakatoliki na Waorthodox, na utafutaji wa umoja katika Kanisa, lakini kiukweli, wakati wa safari hii, pia nilikutana kibinafsi na wawakilishi wa makundi tofauti wanaowakilisha mamlaka ya kisiasa, watu au makundi ambayo yana uhusiano wowote na migogoro ya ndani au hata migogoro ya kimataifa katika eneo hilo.

Kazi yetu si jambo la umma ambalo tunalitangaza mitaani; ni jambo ambalo liko nyuma ya pazia. Ni jambo ambalo tayari tumefanya na tutaendelea kufanya ili kuwashawishi wahusika kuweka silaha zao chini, kuacha vurugu, na kukusanyika pamoja kwenye meza ya mazungumzo: kutafuta majibu na suluhisho ambazo si za vurugu lakini zinaweza kuwa na ufanisi zaidi.

Imad Atrach: Ujumbe kutoka kwa Hezbollah?

Ndiyo, niliuona. Ni wazi kwamba, kwa upande wa Kanisa kuna pendekezo kwamba waweke silaha zao chini na kwamba tutafute mazungumzo. Lakini zaidi ya haya, napendelea kutotoa maoni kwa wakati huu.

Cindy Wooden, CNS: Baba Mtakatifu, ulisema miezi michache iliyopita kwamba kuna njia ya kujifunza kuwa Papa. Ulipofika Harissa jana, kwa ukarimu wa hali ya juu, ilionekana kama ulisema, ‘Woow.’ Je, unaweza kutuambia unachojifunza? Ni jambo gani gumu zaidi kujifunza kwako kuwa Papa? Na hujatuambia chochote kuhusu jinsi ilivyokuwa katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi ilipobainika kilichokuwa kikiendelea. Je, unaweza kutuambia kidogo kuhusu hilo?

Papa, kwa Kiingereza: Naam, maoni yangu ya kwanza yangekuwa kwamba mwaka mmoja au miwili iliyopita mimi pia nilifikiria kustaafu siku moja. Inaonekana umepokea zawadi hiyo; baadhi yetu tutaendelea kufanya kazi. (Utani unaorejea ukweli kwamba Bi. Wooden anastaafu mwezi Desemba, mh.)

Mkutano Mkuu wa uchaguzi  wenyewe, naamini kwa ukali sana kuhusu siri ya Mkutano Mkuu wa Uchaguzi(Conclave,) ingawa ninajua kwamba kumekuwa na mahojiano ya umma ambapo mambo kadhaa yalifichuliwa. Nilimwambia mwandishi wa habari siku moja kabla ya kuchaguliwa kwangu, alinikuta barabarani nikiwa ninakwenda kula chakula cha mchana ng'ambo ya barabara kwa Waagostinian, na akasema, 'Unafikiri nini? Umekuwa mmoja wa wagombea!' Nami nilisema tu, 'Kila kitu kiko mikononi mwa Mungu.' Na ninaamini hilo kwa undani.

Mmoja wenu, kuna mwandishi wa habari wa Ujerumani hapa ambaye aliniambia siku moja, niambie kitabu kimoja, mbali na Mtakatifu Agostino, ambacho tunaweza kusoma ili kuelewa Prevost ni nani. Na kuna vitabu kadhaa nilivyofikiria, lakini moja wapo ni kitabu kinachoitwa, "Utendaji wa uwepo wa Mungu." Ni kitabu rahisi sana, kilichoandikwa na mtu ambaye hata jina lake la mwisho, ni  Ndugu Lawrence, kilichoandikwa miaka mingi iliyopita. Lakini kinaelezea, ukitaka, aina ya sala na mambo ya kiroho ambapo mtu humpa Bwana maisha yake na kumruhusu Bwana akuongoze. Ukitaka kujua jambo kunihusu, hilo limekuwa jambo la kiroho kwangu kwa miaka mingi.

Katikati ya changamoto kubwa, kuishi nchini Peru wakati wa miaka ya ugaidi, kuitwa kutumikia katika maeneo ambayo sikuwahi kufikiria ningeitwa kutumikia. Ninamwamini Mungu, na ujumbe huo ni kitu ambacho ninashirikishana na watu wote. Kwa hivyo ilikuwaje? Nilijisalimisha kwa ukweli nilipoona jinsi mambo yalivyokuwa yakiendelea, na nikasema kwamba hii inaweza kuwa ukweli. Nilipumua kwa kina, nikasema, Bwana, wewe ndiye unayesimamia, unaongoza njia.

Sijui kama nilisema ‘Woow’ jana usiku. Kwa maana kwamba uso wangu unaonekana wazi sana, lakini mara nyingi hufurahishwa na jinsi waandishi wa habari wanavyotafsiri uso wangu. Namaanisha, inavutia; wakati mwingine mnajua mimi hupata, kama mawazo mazuri sana kutoka kwenu nyote, kwa sababu mnafikiri mnaweza kusoma mawazo yangu au uso wangu. Na sivyo, sio kila wakati huwa sahihi. Namaanisha, nilikuwa kwenye Jubilei ya Vijana, ambapo kulikuwa huko na vijana zaidi ya milioni 1. Jana usiku kulikuwa na umati mdogo.

Daima ni ajabu kwangu; ninajiambia, ‘Watu hawa wako hapa kwa sababu wanataka kumuona Papa,’ lakini ninajiambia, ‘Wako hapa kwa sababu wanataka kumuona Yesu Kristo na wanataka kumuona mjumbe wa amani,’ katika hali hii hasa. Kwa hivyo kusikiliza tu shauku yao, na kusikia majibu yao kwa ujumbe huo ni jambo ambalo nadhani ni shauku hiyo inavutia. Natumaini sitachoka kuthamini kila kitu ambacho vijana hawa wote wanaonesha.

Gian Guido Vecchi (Corriere della Sera): Hizi ni saa za mvutano mkubwa kati ya NATO na Urusi; kuna mazungumzo ya vita mseto, matarajio ya mashambulizi ya mtandaoni, na mambo ya aina hii. Je, unaona hatari ya kuongezeka kwa mgogoro, unaoendelezwa kwa njia mpya kama ilivyoripotiwa na viongozi wa NATO? Na, katika hali hii, je, kunaweza kuwa na mazungumzo ya amani ya haki bila Ulaya, ambayo katika miezi ya hivi karibuni imetengwa kimfumo na urais wa Marekani?

Papa, kwa Kiitaliano: Hili ni suala muhimu kwa amani duniani, lakini Vatican haina ushiriki wa moja kwa moja, kwa sababu sisi si wanachama wa NATO wala wa mazungumzo yoyote hadi sasa, na ingawa mara nyingi tumetoa wito wa kusitisha mapigano, kwa njia ya mazungumzo na si vita. Na sasa ni vita yenye vipengele vingi: pamoja na ongezeko la silaha, uzalishaji wote wa silaha unaoendelea, mashambulizi ya mtandaoni, nishati. Sasa kwa kuwa majira ya baridi yanakuja kuna tatizo kubwa hapo. Ni wazi kwamba, kwa upande mmoja, Rais wa Marekani anafikiri anaweza kukuza mpango wa amani ambao angependa kutekeleza na kwamba, angalau mwanzoni, hauna Ulaya.

Lakini uwepo wa Ulaya ni muhimu, na pendekezo hilo la kwanza pia lilibadilishwa kwa sababu ya kile ambacho Ulaya ilikuwa ikisema. Hasa, nadhani jukumu la Italia linaweza kuwa muhimu sana. Kiutamaduni na kihistoria, Italia ina uwezo wa kutenda kama mpatanishi katikati ya mgogoro uliopo kati ya pande tofauti: Ukraine, Urusi, Marekani… Kwa maana hii, naweza kupendekeza kwamba Vatican inaweza kuhimiza aina hii ya upatanishi, na kwamba mtu anapaswa kutafuta, na kwamba tunapaswa kutafuta pamoja, suluhisho ambalo linaweza kutoa amani ya kweli, amani ya haki, katika kesi hii nchini Ukraine.

Elisabetta Piqué (La Nación): Bendera ya Lebanon ina rangi sawa na bendera ya Peru. Je, hiyo ni ishara kwamba utatembelea Amerika Kusini katika nusu ya pili ya mwaka ujao, ukiichanganya na Argentina na Uruguay? Ukicheka kando, unajiandaa kwa ziara gani kwa mwaka ujao? Na, zaidi ya hayo, tukizungumzia Amerika Kusini, kuna mvutano mkubwa kutokana na kinachoendelea Venezuela. Kuna kauli ya mwisho kutoka kwa Rais Trump hadi Maduro ya kujiuzulu, kuondoka madarakani, na tishio la kumwondoa madarakani kwa operesheni ya kijeshi. Unafikiri nini kuhusu hili?

Papa, kwa Kihispania: Kuhusu ziara, hakuna uhakika kabisa; natumaini kufanya ziara Afrika. Huenda hiyo ikawa safari inayofuata. Bi. Piqué: Wapi? Afrika, Afrika. Binafsi, natumaini kwenda Algeria kutembelea maeneo ya Mtakatifu Agostino, lakini pia ili kuendelea na mazungumzo ya mazungumzo, ya kujenga madaraja kati ya ulimwengu wa Kikristo na ulimwengu wa Kiislamu. Hapo awali, katika jukumu lingine, tayari nilikuwa na fursa ya kuzungumzia mada hii. Inavutia: sura ya Mtakatifu Agostino husaidia sana kama daraja, kwa sababu nchini Algeria anaheshimiwa sana kama mwana wa nchi yake. Hiyo ni moja. Kisha kuna nchi zingine, lakini tunafanyia kazi. Ni wazi, ningependa sana kutembelea Amerika Kusini, Argentina, na Uruguay, ambazo zinasubiri ziara ya Papa. Nadhani Peru pia ingenikaribisha, na nikienda Peru pia kutakuwa na nchi nyingi jirani, lakini mpango bado haujafafanuliwa.

Kuhusu Venezuela, katika ngazi ya Mkutano wa Maaskofu na pamoja na Balozi wa Kitume, tunajaribu kutafuta njia ya kutuliza hali hiyo, tukitafuta zaidi ya mema yote ya watu, kwa sababu katika hali hizi ni watu wanaoteseka, si mamlaka. Ishara zinazotoka Marekani zinabadilika, na kwa hivyo lazima tuone… Kwa upande mmoja, inaonekana kumekuwa na mazungumzo ya simu kati ya marais hao wawili; kwa upande mwingine, kuna hatari hii, uwezekano huu, kwamba kunaweza kuwa na hatua, operesheni, ikiwa ni pamoja na uvamizi wa eneo la Venezuela. Ninaamini tena ni bora kutafuta mazungumzo ndani ya shinikizo hili, ikiwa ni pamoja na shinikizo la kiuchumi, lakini kutafuta njia nyingine ya kuleta mabadiliko, ikiwa ndivyo Marekani inavyoamua kufanya.

Michael Corre, La Croix: Baba Mtakatifu, asante kwa safari hii ya kuvutia sana. Umezungumzia tu kuhusu kuendelea kujenga daraja kati ya walimwengu tofauti? Ningependa kuuliza: baadhi ya Wakatoliki barani Ulaya wanaamini kwamba Uislamu ni tishio kwa utambulisho wa Kikristo wa Magharibi. Je, wako sahihi, na ungewaambia nini?

Papa, kwa Kiingereza: Mazungumzo yote niliyofanya wakati wangu, huko Türkiye na Lebanon, ikiwa ni pamoja na Waislamu wengi, yalijikita hasa kwenye mada ya amani na heshima kwa watu wa dini tofauti. Ninajua kwamba, kiukweli, hilo halijawa hivyo kila wakati. Ninajua kwamba barani Ulaya kuna hofu nyingi zilizopo lakini mara nyingi husababishwa na watu wanaopinga uhamiaji na kujaribu kuwaweka nje watu ambao wanaweza kuwa wanatoka nchi nyingine, dini nyingine, na rangi nyingine.

Na kwa maana hiyo, ningesema kwamba sote tunahitaji kufanya kazi pamoja, moja ya maadili ya ziara hii ni kuinua umakini wa ulimwengu kwa uwezekano kwamba mazungumzo na urafiki kati ya Waislamu na Wakristo inawezekana. Nadhani moja ya mafunzo makubwa ambayo Lebanon inaweza kufundisha ulimwengu ni kuonesha hasa nchi ambapo Uislamu na Ukristo vipo na vinaheshimiwa na kwamba kuna uwezekano wa kuishi pamoja ili kuwa marafiki.

Historia, ushuhuda, mashahidi ambao tulisikia hata katika siku mbili zilizopita za watu wakisaidiana; Wakristo walio na Waislamu, ambao wote wawili walikuwa wameharibiwa vijiji vyao, kwa mfano, walikuwa wakisema tunaweza kuungana na kufanya kazi pamoja. Nadhani hayo ni mafunzo ambayo yangekuwa muhimu pia kusikilizwa Ulaya au Amerika Kaskazini. Labda tunapaswa kupunguza woga kidogo na kutafuta njia za kukuza mazungumzo na heshima halisi.

Anna Giordano (Ard Radio): Kanisa nchini Lebanon linaungwa mkono pia na Kanisa la Ujerumani. Kwa mfano, kuna baadhi ya mashirika ya misaada ya Ujerumani yanayofanya kazi sana nchini Lebanon. Kwa hivyo pia kutokana na mtazamo huo, ni muhimu kwamba Kanisa la Ujerumani liendelee kuwa Kanisa imara. Kwa hivyo labda unajua, kwamba kuna hii (Synodal Weg), Njia ya Sinodi, mchakato wa mabadiliko katika Kanisa la Ujerumani unaoendelea. Je, unafikiri mchakato huu unaweza kuwa njia ya kuimarisha Kanisa? Au ni kinyume chake? Na kwa nini?

Papa, kwa Kiingereza: Njia ya Sinodi si ya kipekee kwa Ujerumani; Kanisa zima limeadhimisha Sinodi na sinodi katika miaka kadhaa iliyopita. Kuna kufanana pakubwa, lakini pia kuna tofauti kubwa kati ya jinsi ya Njia ya Sinodi nchini Ujerumani ilivyoendelezwa na jinsi inavyoweza kuendelea katika Kanisa la ulimwengu wote. Kwa upande mmoja, ningesema hakika kuna nafasi ya kuheshimu utamaduni. Ukweli kwamba katika sehemu moja sinodi huishi kwa njia fulani, na katika sehemu nyingine huishi tofauti, haimaanishi kwamba kutakuwa na mpasuko au mipasuko. Nadhani hilo ni muhimu sana kukumbuka.

Wakati huo huo, ninajua kwamba Wakatoliki wengi nchini Ujerumani wanaamini kwamba vipengele fulani vya Njia ya Sinodi ambavyo vimeadhimishwa nchini Ujerumani hadi sasa, haviwakilishi tumaini lao kwa Kanisa au jinsi wanavyoishi Kanisa. Kwa hivyo, kuna haja ya mazungumzo zaidi na kusikiliza ndani ya Ujerumani yenyewe, ili sauti ya mtu yeyote isiondolewe, ili sauti ya wale walio na nguvu zaidi isinyamazishe au kuzima sauti ya wale ambao wanaweza kuwa wengi sana lakini hawana mahali pa kuzungumza na kuruhusu sauti zao na maneno yao ya ushiriki wa Kanisa kusikilizwa.

Wakati huo huo, kama mnavyojua nina uhakika, kundi la Maaskofu wa Ujerumani limekuwa likikutana, kwa miaka michache iliyopita, na kundi la Makardinali kutoka Curia Romana. Kuna mchakato unaoendelea huko pia, kujaribu na kuhakikisha kwamba Njia ya Sinodi ya Ujerumani, ikiwa itafanya hivyo, haijitengi na kile kinachohitajika kuchukuliwa kama njia ya Kanisa la ulimwengu wote. Nina uhakika hilo litaendelea. Ninashukuru, kutakuwa na marekebisho kadhaa yaliyofanywa pande zote mbili nchini Ujerumani, lakini ninatumaini hakika kwamba mambo yataenda vizuri.

Rita El-Mounayer (Sat-7 International): Sisi ni chaneli nne tofauti za Kikristo zinazotangaza katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, mbili kwa Kiarabu, moja kwa Kiajemi na moja kwa Kituruki. Kwanza kabisa, ningependa kukushukuru kwa kutoa muda kwa ajili ya watu wa Lebanon. Mimi mwenyewe ni mtoto wa vita, na ninajua jinsi inavyomaanisha kukumbatiwa na Utakatifu wako, kubembelezwa begani, na kusema kila kitu kitakuwa sawa.

Na kilichonigusa ni kauli mbiu yako: ‘Katika mmoja sisi ni wamoja.’ Kauli mbiu hii inazungumzia kujenga madaraja kati ya madhehebu tofauti ya Kikristo, kati ya dini na pia kati ya majirani, ambayo wakati mwingine inaweza kuwa ngumu kidogo. Kwa hivyo swali langu ni, kwa mtazamo wako mwenyewe, ni zawadi gani ya kipekee ambayo Kanisa katika Mashariki ya Kati—pamoja na machozi yake yote, majeraha, changamoto na historia ya zamani, linaweza kuipatia  Kanisa katika Magharibi na Ulimwenguni?

Papa, kwa Kiingereza: Acha nianze jibu langu kwa kusema kwamba leo watu waliokulia katika jamii yenye ubinafsi, vijana waliopita muda mwingi wakati wa janga la Uviko, na ambao mahusiano yao ya kibinafsi mara nyingi huwa yametengwa sana, kiukweli kwa sababu yanafanywa kupitia skrini za kompyuta au simu za mkononi, wakati mwingine huuliza, ‘Kwa nini tunapaswa kutaka kuwa wamoja? Mimi ni mtu binafsi, na sijali wengine.’ Na nadhani kuna ujumbe muhimu sana hapa wa kuwaambia watu wote kwamba umoja, urafiki, mahusiano ya kibinadamu, na ushirika, ni muhimu sana na wenye thamani kubwa. Ikiwa bila sababu nyingine, basi mfano uliotaja kuhusu mtu ambaye ameishi vitani au ameteseka na ana maumivu, kukumbatiana kunaweza kumaanisha nini kwake. Ni kile ambacho usemi huo wa kibinadamu, halisi, na wenye afya wa utunzaji wa kibinafsi unaweza kufanya ili kuponya moyo wa mtu mwingine.

Katika ngazi ya kibinafsi, hiyo inaweza kuwa, ikiwa utafanya, kiwango cha kawaida, kiwango cha jamii kinachotuunganisha sote, na kutusaidia kuelewa, na heshima kwa kila mmoja inazidi ‘Wewe huweka umbali wako; Nitakaa hapa, na wewe ukae pale, na hatutakuwa na mwingiliano.’ Lakini inamaanisha kujenga mahusiano ambayo yatawatajirisha watu wote. Kwa ujumbe huo, hakika, kauli mbiu yangu ni kwa sababu ya Kristo “il illo” ni ‘Katika Kristo ambaye ni mmoja na sisi sote tu wamoja.’ Lakini haijafafanuliwa, ukitaka, kuwa Wakristo pekee. Kiukweli, ni mwaliko kwetu sote na kwa wengine kusema: kadiri tunavyoweza kukuza umoja na uelewa wa kweli, heshima na uhusiano wa kibinadamu wa urafiki na mazungumzo duniani, kuna uwezekano mkubwa zaidi kwamba tutaweka kando silaha za vita, kwamba tutaacha kando kutoaminiana, chuki, uadui ambao umejengwa mara nyingi na kwamba tutapata njia za kuungana na kuweza kukuza amani na haki halisi ulimwenguni kote.

Papa na waandishi wa habari

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

02 Desemba 2025, 18:09