Papa Leo XIV: Tarehe 22 Februari 2026: Mt. Faustina Kowalska: Miaka 95 Tangu Alipotokewa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 18 Mei 2020 alisema, Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake, alijitahidi kuwafunulia watu wa Mungu, huruma na upendo wa Mungu, kama Kristo Yesu alivyomfunulia Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska wa Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma. Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska huu ni wakati wake wa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa sababu rehema zake hudumu vizazi hata vizazi kwa hao wanaomcha! Bikira Maria katika utenzi wake wa “Magnificat” anatafakari kazi ya ukombozi iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya binadamu wote na kwamba, kazi hii inatoa mwangwi wake kwenye maisha ya kiroho yanayosimuliwa na Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska, Bikira, ambaye kwa njia ya zawadi kubwa kutoka mbinguni, alibahatika kukutana na Kristo Yesu, ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu Baba na akawa shuhuda na chombo cha kutangaza na kueneza Ibada ya Huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 18 Februari 2026 amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, tarehe 22 Februari 2026, Mama Kanisa anaadhimisha kumbukizi ya Miaka 95 tangu Kristo Yesu wa huruma ya Mungu kwa mara ya kwanza kabisa alipomtokea Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska. Tukio hili likawa ni chemchemi ya Rozari ya Huruma ya Mungu na Sala yake.
Kunako mwaka 1931, Kristo Yesu alimtokea Mtakatifu Sr. Faustina katika maono akamwona Yesu akiwa amevaa vazi jeupe, mkono wake wa kuume umeinuliwa kubariki; mkono wake wa kushoto ulikuwa umegusa vazi lake kifuani kwenye sehemu ya Moyo ambamo miali miwili mikubwa ya mwanga ilitokea: mmoja mwekundu, mwingine kama maji. Alimwangalia Kristo Yesu kwa makini sana akiwa kimya na roho yake ilijawa mshangao, ukichanganyikana na furaha kubwa. Yesu akamwambia: “Chora picha kama unavyoiona hapa na chini yake uandike maneno haya: ‘Yesu, nakutumainia!’ Naahidi kwamba roho yoyote itakayotukuza picha hii haitaangamia kamwe. Naahidi pia ushindi kwa maadui wa roho hiyo walio duniani humu, hasa saa ya kifo chake. Mimi mwenyewe nitailinda kama utukufu wangu.” (47,48) “Nawapatia watu chombo watakachotumia kila mara wajapo kupata neema kwenye chemchemi ya Huruma yangu. Chombo hicho ni picha hii na maneno: “Yesu, nakutumainia!” (327) “Napenda picha hii itukuzwe, kwanza kwenye kikanisa chenu na baadaye duniani kote.” (47).
Baba yake wa kiroho alimwomba Mtakatifu Sr Faustina amuulize Kristo Yesu maana ya miali hiyo kwenye picha. Sr Faustina alijibiwa kwa maneno haya: “Miali hiyo miwili humaanisha Damu na Maji. Miali ya maji ni kwa ajili ya Maji yale yatakasayo roho na kuzifanya zenye haki; miali myekundu humaanisha Damu ambayo ni uzima wa roho. Miali hii miwili ilichomoza toka kwenye Moyo wangu wenye Huruma siku ile nilipochomwa kwa mkuki Moyoni pale Msalabani... Heri atakayefunikwa na miali hiyo, mkono wa Mungu wenye haki hautamgusa.” (299) “Nitazipa roho neema nyingi kwa kutumia picha hii. Iwe ni ukumbusho wa madai ya Huruma yangu, kwani hata imani kali kiasi gani bila matendo haina maana.” (742). Picha hii imeishachorwa na mafundi wengi mbalimbali, lakini Bwana Yesu alisema wazi kuwa usanii au ufundi wa uchoraji si jambo muhimu. Mtakatifu Sr. Faustina alipoona kwa mara ya kwanza ile picha iliyochorwa kwa maelekezo yake alilia na kuduwaa huku akimlilia Yesu: "Ni nani awezaye kukuchora na kuonesha uzuri ule ule ulionao?"(313). Baadaye alisikia maneno haya: "Ukuu wa picha hii hauko katika rangi wala kifaa kilichotumika kuichora, wala ufundi, bali katika Neema yangu" (313).
ROZARI YA HURUMA YA MUNGU: Chombo cha pili cha kuwaunganisha waamini na Huruma ya Mungu na zana maalum aliyowakabidhi Kristo Yesu mwenyewe kupitia kwa Mtakatifu Sr. Faustina ni Rozari ya Huruma. Mnamo mwaka 1935, Mtakatifu Sr Faustina alipata maono ya Malaika wa Bwana aliyetumwa kuangamiza mji fulani. Sista Faustina akaanza kuomba huruma, lakini sala zake hazikuwa na nguvu yoyote. Ghafula, akaona Utatu Mtakatifu na nguvu ya neema ya Kristo Yesu ikamjia. Wakati huo huo alijikuta anamwomba Mungu Huruma yake kwa maneno aliyoyasikia ndani ya moyo wake: “Baba wa milele, ninakutolea Mwili na Damu, Roho na Umungu wa Mwanao Mpenzi, Bwana wetu Yesu Kristo, kwa kulipia dhambi zetu na dhambi za dunia nzima; kwa ajili ya Mateso makali ya Yesu, utuhurumie sisi na dunia nzima (476). Alipokuwa anaendelea kusali sala hii, Malaika alionekana kushindwa kutimiza adhabu hiyo (taz. Shajara, nn. 474 na 475). Ni kutokana na muktadha huu, Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa kusikiliza maombi yaliyowasilishwa na watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia na baada ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu amana na utajiri wa maisha ya Mtakatifu Faustina, ameridhia na kutamka kwamba: Mtakatifu Maria Faustina (Helena) Kowalska, Bikira aingizwe kwenye Kalenda ya Kirumi na atakuwa anakumbukwa na waamini wote tarehe 5 Oktoba ya kila mwaka, kama Kumbukumbu ya Hiyari. Maagizo haya yanapaswa kuingizwa kwenye Kalenda na Vitabu vya Liturujia kwa ajili ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu na Sala ya Kanisa kwa kuzingatia maelelezo yaliyotolewa kwenye Tamko hili. Kumbe, nyaraka hizi zinapaswa kutafsiriwa, kuthibitishwa na hatimaye kupitishwa na Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa na mwishoni, kuchapishwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki.
Mtakatifu Sr. Faustina alibahatika kuishi katika Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma kwa muda mfupi. Alionesha moyo wa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa wito na zawadi mbali mbali za maisha ya kiroho, akajitahidi kuishi kwa uaminifu mkubwa kwa zawadi zote hizi. Katika Shajara ya moyo wake, Madhabahu ambayo aliyatumia kukutana na Kristo Yesu, mwenyewe anasimulia jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyomwezesha kwa ajili ya faida ya watu wengi zaidi. Kwa kumsikiliza Kristo Yesu ambaye ni Upendo na Huruma aliweza kutambua kwamba, hakuna dhambi yoyote ya binadamu ambayo ingeweza kushinda huruma ya Kristo Yesu inayobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu. Na tangu wakati huo, akawa ni muasisi wa Ibada ya Huruma ya Mungu ambayo leo hii imeenea sehemu mbali mbali za dunia. Alitangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Mtakatifu, wakati wa Maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Tangu sasa, Mtakatifu Faustina Bikira, atakuwa anaadhimishwa katika Kumbukumbu ya Hiyari na Kanisa zima, kila mwaka ifikapo tarehe 5 Oktoba!
Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa katika tamko lililotolewa tarehe 18 Mei 2020 lilitangaza kwamba kuanzia sasa waamini wataweza kuadhimisha Kumbukumbu ya Hiyari kwa Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska, Bikira, baada ya jina lake kuingizwa kwenye Kalenda ya Kirumi. Mtakatifu Faustina Kowalska alizaliwa tarehe 25 Agosti 1905. Mwaka 1925 akajaribu kuanza maisha ya kitawa ndani ya Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa huruma. Tarehe 3 Aprili 1927 anatokewa na muujiza, Mwaka 1931 akaanza utume wake katika tasaufi ya huruma ya Mungu. Mwaka 1933 akaweka nadhiri za daima. Mwaka 1938 akafariki dunia. Mwaka 1993 akatangazwa kuwa ni Mwenyeheri na mwaka 2000 akatangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni Mtakatifu. Ni mtakatifu anayependwa na wengi kutokana na jitihada zake za kukuza na kueneza: Tasaufi na Ibada ya Huruma ya Mungu, chemchemi ya upendo wa Mungu kwa waja wake. Tangu hapo, Jina la Mtakatifu Faustina likapata umaarufu wa ajabu kutoka sehemu mbalimbali za dunia mwitikio wa kutangaza na kushuhudia Ibada ya Huruma ya Mungu ambayo imeleta mageuzi makubwa katika maisha ya waamini.
