Papa Leo XIV: Hotuba Kwa Makleri wa Jimbo Kuu la Roma: Uinjilishaji wa Kina
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Msingi wa utumishi wa Wahudumu wa Daraja Takatifu yaani: Ushemasi, Upadre na Uaskofu ni Kristo Yesu mwenyewe aliyekuja kutumika na kuutoa uhai wake kwa ajili ya wengi. Ekaristi Takatifu wanayoiadhimisha kila siku iwakumbushe kwamba, “chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa hukaa hali iyo peke; bali ikifa, hutoa mazao mengi” (Yn 12:24). Kristo ndiye chembe ya ngano ya Mungu na kutoka kwa Mungu ameshuka katika ulimwengu. Padri anapoadhimisha Ekaristi Takatifu, anagusa kwa mikono yake Mkate wa ngano ya Mungu ambaye ndiye Kristo Yesu mwenyewe, ambaye kutokana na: mateso na kifo chake, chembe ya ngano imekuwa mkate kwa ajili ya ulimwengu mzima. Kwa hiyo, kwa mhudumu wa Daraja Takatifu, Ekaristi Takatifu, licha ya kuwa ishara kuu ya mavuno, furaha ya karamu ya harusi ambako watakuja wengi kutoka mashariki na magharibi, kaskazini na kusini (Rej. Mt 8:11), vile vile ni ishara ya Msalaba, kiwango cha juu kabisa cha utumishi. Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha jinsi kuhani anavyopaswa kuwa chembe ya ngano ya Mungu. Hapaswi tu kuridhika kutoa maneno na matendo ya nje, bali anapaswa kujibidiisha katika maisha yake, akijitoa kwa kutumikia mpaka tone la damu. Wahudumu wa Daraja Takatifu wawajibike, awali ya yote, kuihubiri Injili ya Mungu kwa watu wote wakiushika utume wa Bwana asemapo: “Enendeni ulimwenguni mwote mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe” (Rej Mk 16:15). Watu wote wanayo haki ya kulitafuta Neno la Mungu kutoka midomoni mwa mhudumu wa Daraja Takatifu ambaye anapaswa kulihubiri wakati ufaao na wakati usiofaa (Rej. 2Tim 4:2). Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unasema kwamba, Mapadri wanaitwa na kuwekwa wakfu ili watumikie kwa unyenyekevu katika kazi ya kutakatifuza… na watende kazi kama wahudumu wa Yule anayetekeleza bila kukoma wadhifa wake wa kikuhani kwa ajili yetu kwa njia ya Roho wake. Wahudumu wa Daraja Takatifu wamepewa mamlaka ya kutoa huduma hii bila ya mastahili yao na tena wamepewa bure (Mt 10:8.)
Kwa hiyo, wahudumu wa Daraja Takatifu wanapaswa kutoa huduma yao ya utumishi kwa bidii na kwa nguvu zao zote bila masharti wala ubaguzi. Hata hivyo, kwa namna ya pekee, wamekabidhiwa hasa walio maskini na wanyonge zaidi. Ni vizuri viongozi wa Daraja Takatifu wakatafakari namna na jinsi wanavyotekeleza agizo hilo. Namna wanavyotoa huduma za kichungaji katika Jumuiya, Kigango, Parokia na pengine hata nje ya majimbo yao. Ni aina gani ya watu wanaokuwa nao karibu zaidi? Je? Maskini na wanyonge wanayo nafasi mioyoni mwao? Wahudumu wa Daraja Takatifu, inabidi wawe tayari kila wakati kutafuta siyo mapenzi yao binafsi, bali mapenzi ya yule aliyewatuma (taz. Yn 4:34; 5: 30; 6:38.) Kazi ya Kimungu ambayo walichukuliwa na Roho Mtakatifu kwayo, inapita nguvu na uwezo pia hekima ya wanadamu; kwa sababu: “Mungu alivichagua vitu vidhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu” (1Kor 1:27.) Kwa hiyo, mhudumu wa Daraja Takatifu anapaswa kutambua udhaifu wake na kufanya kazi kwa unyenyekevu, akijihakiki ni nini impendezayo Bwana na, hali amefungwa na Roho, anaongozwa katika yote na mapenzi yake yule anayetaka watu wote waokolewe; nayo mapenzi ya Mungu ataweza kuyagundua na kuyafuata katika mambo ya kila siku akiwatumikia kwa unyenyevu wote waliokabidhiwa kwake na Mungu kutokana na dhima anayotakiwa kutekeleza, na matukio mbalimbali ya maisha yake.
Kimsingi Mapadre ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vya faraja kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu na kwamba, mang’amuzi ya Sakramenti ya Upatanisho yawaonjeshe watu upendo na huruma ya Mungu. Mapadre wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama Baba Mwenye huruma, ili waamini hao, waweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao, Mungu ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo!
Baba Mtakatifu Leo XIV, Alhamisi tarehe 19 Februari 2026 amekutana na kuzungumza na Makleri wa Jimbo kuu la Roma. Ametumia fursa hii kuwashukuru kwa kuchakarika katika shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Roma: fursa, magumu na changamoto za shughuli za kichungaji; kwa kuendelea kuchochea karama ya Mungu iliyomo ndani mwao sanjari na kuwasha moto kwa ajili ya watu wa Mungu, Jimbo kuu la Roma. Huu ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu. Makleri wajenge utamaduni na kujifunza kufanya kazi kwa ushirikiano katika umoja; wajitahidi kuwa karibu na vijana wa kizazi kipya na Mapadre vijana wajiangalie wasitumbukie katika upweke hasi na kwamba, Makleri wanayo dhamana na wajibu wa kulinda, kutunza na kukuza miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XIV Aametumia fursa hii kuwashukuru kwa kuchakarika katika shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Roma: fursa, magumu na changamoto za shughuli za kichungaji; kwa kuendelea kuchochea karama ya Mungu iliyomo ndani mwao sanjari na kuwasha moto kwa ajili ya watu wa Mungu, Jimbo kuu la Roma. Katika utekelezaji wa majukumu yao, hapana shaka kwamba, wanakutana na uchovu, wakati mwingine hali ya kuchanganyikiwa; kuteteleka na hatimaye kuanguka chini katika maisha ya kiroho, maadili na utu wema. Katika hali na mazingira kama haya, Makleri wanahimizwa kuchochea karama ya Mungu iliyoko ndani mwao, kwa kuwasha moto katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Roma. Ikumbukwe kwamba, Moto ni alama ya Roho Mtakatifu anayeliwezesha Kanisa kutembea kwa kuzingatia historia na Mapokeo yanayoendelezwa katika Jumuiya za waamini. Moto wa Roho Mtakatifu ni muhimu katika maisha na utekelezaji wa shughuli za kichungaji, katika hali ya kuchoka na kukata tamaa; imani haba “kama kiatu cha raba” sanjari na kupungua kwa uchaji wa Mungu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anawashukuru na kuwapongeza Makleri wa Jimbo kuu la Roma kwa huduma yao kwa watu wa Mungu kutokana na: fursa, kinzani na changamoto za maisha na kwamba, hizi zinaweza kuwa ni fursa ya kutafakari jinsi ya kukabiliana na changamoto hizi kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji unaojikita hasa katika Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, ili kweli imani iweze kurithishwa na kukita mizizi yake katika tunu msingi za maisha ya familia, lakini kwa sasa kuna mmong’onyoko wa tunu msingi za maisha na hivyo urithishaji wa imani, inakuwa ni changamoto pevu! Kumbe, kipaumbele cha kwanza kwa sasa ni kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mungu, Jimbo kuu la Roma, kwa moyo wa unyenyekevu na ari kuu. Kuna waamini waliobatizwa katika Kanisa Katoliki, lakini wanakosa kujitambua kuwa wao ni sehemu muhimu sana ya Kanisa. Pengine hali hii inatokana na ukosefu wa ukarimu, ukiritimba, maisha magumu na kwamba, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji imepewa nafasi ndogo sana ikilinganishwa na shughuli za kiutawala. Mkazo hapa ni kutoa Sakramenti tofauti na namna nyingine za uinjilishaji. Rej. Evangelii gaudium, 63. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hapa kuna haja ya kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili, kwa kuwasaidia waamini kupata tena fursa ya kukutana na Kristo Yesu kwa kuwashirikisha watoto, vijana na familia katika kurithishana imani.
Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka Makleri wa Jimbo kuu la Roma kujifunza ili hatimaye, kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa kushirikiana na katika umoja, kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu; kufanya kazi kipeke peke ni hatari kwa maisha na utume wa Mapadre. Ushirikiano kati ya Parokia jirani ni jambo muhimu sana linalowawezesha waamini kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Mapadre washirikishane karama, mapaji na mang’amuzi ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu, kielelezo cha ushirika na umoja wa Mapadre. Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka Makleri wa Jimbo kuu la Roma kujenga ukaribu na vijana wa kizazi kipya kwani kuna baadhi yao wanaishi bila ya kuwa na rejea ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao; kuna vijana ambao wametopea na kuzama katika malimwengu; matumizi ya mitandao ya kijamii; vitendo vya jinai bila kusahau kwamba, kuna baadhi yao wamejitumbukiza katika utumwa mamboleo unaosigina utu, heshima na haki zao msingi. Kumbe, Mapadre wa Jimbo kuu la Roma, wajenge utamaduni wa kuwasikiliza na kuwahusisha vijana katika maisha na utume wa Kanisa; Kwa kujaribu kushiriki maisha ya ujana wao; Kwa kujenga na kudumisha majadiliano na shule zilizopo katika maeneo ya Parokia; Kwa kuwashirikisha wataalamu katika sekta ya elimu, sayansi ya binadamu pamoja na wale wote wanaojitosa kusaidia ustawi, maendeleo na mafao ya vijana wa kizazi kipya.
Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwatia shime Mapadre vijana na amewatahadharisha kwamba, katika ujana wao wanaweza kutumbukia na kumezwa na malimwengu sanjari na upweke hasi. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka Mapadre vijana kujenga na kudumisha urafiki, mahusiano na mafungamano ya karibu zaidi na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Neno la Mungu pamoja na Sakramenti za Kanisa. Wawe wazi na tayari kushirikisha hali zao za maisha na utume. Mapadre katika Jumuiya zao, wajenge na kudumisha utamaduni wa kusikilizana; mshikamano na kusaidiana kwa hali na mali. Mapadre watambua kwamba, dhamana na wajibu wao wa kwanza ni kulinda na kudumisha miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba, hii ni changamoto inayosimikwa katika hija ya toba na wongofu wa ndani; upyaisho wa uaminifu na shirikishi. Na kwa njia hii, anasema Baba Mtakatifu Makleri wa Roma wataweza kuhudumia watu wa Mungu kwa ubora zaidi huku wakiwa wamesheheni moyo wa Mungu.
