Papa Leo XIV: Kipindi cha Kwaresima ni chemchemi ya furaha inayowakumbusha waamini kwamba, wanaitwa, kama Kanisa, yaani Jumuiya ya waamini kusikiliza Neno la Mungu Papa Leo XIV: Kipindi cha Kwaresima ni chemchemi ya furaha inayowakumbusha waamini kwamba, wanaitwa, kama Kanisa, yaani Jumuiya ya waamini kusikiliza Neno la Mungu   (@Vatican Media)

Papa Leo XIV: Ibada ya Jumatano ya Majivu Mwanzo wa Kipindi Cha Kwaresima 2026

Papa Leo XIV: Kipindi cha Kwaresima ni chemchemi ya furaha inayowakumbusha waamini kwamba, wanaitwa, kama Kanisa, yaani Jumuiya ya waamini kusikiliza Neno la Mungu na kwamba, huu ni mwaliko kwa watu wote katika hali na mazingira yao mbalimbali, ili kumlilia Mwenyezi Mungu, aweze kuwasamehe dhambi zao. Kwaresima ni kipindi muafaka cha watu wa Mungu kuweza kukusanyika, kwa kutambua dhambi na udhaifu wao, tayari kuwajibika kikamilifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu 2026 kinanogeshwa na ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kauli mbiu: “Kusikiliza na kufunga: Kwaresima kama Kipindi cha Wongofu wa ndani.” Kwaresima ni kipindi ambacho Kanisa kama Mama na Mwalimu, anawaalika watoto wake kutoa kipaumbele cha pekee kwa Fumbo la Mungu katikati ya maisha yao, ili imani ipate tena nguvu na mioyo ya waamini isipotee katikati ya mahangaiko na bughudha za maisha ya kila siku. Kila safari ya wongofu wa ndani huanza pale waamini wanaporuhusu Neno la Mungu liwafikie na kulikaribisha kwa moyo wa unyenyekevu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuna uhusiano kati ya karama ya Neno la Mungu, Nafasi ya Ukarimu na mabadiliko ambayo Neno hili linaleta. Kwa sababu hiyo, safari ya Kwaresima inakuwa ni fursa muafaka ya kusikiliza sauti ya Mungu na hivyo kupyaisha tena maamuzi ya kumfuasa Kristo Yesu, kwa kutembea katika njia ile iendayo Yerusalemu ambako Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko vinapata utimilifu wake. Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 18 Februari 2026 amewaambia waamini kwamba, Kwaresima ni muda muafaka wa kukutana na Kristo Yesu katika: Neno, Sala, Sakramenti, hasa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho, Mahakama ya huruma ya Mungu sanjari na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni muda uliokubaliwa wa kukutana na Kristo Yesu katika historia na safari ya maisha ya kila mwamini. Ni muda wa waamini kuzamisha maisha yao katika sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kujenga na kudumisha mshikamano na udugu wa kibinadamu. Moyo wa sala, tafakari ya kina ya Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti katika Kipindi hiki cha Kwaresima ni mambo yanayoweza kuwasaidia waamini kuzama katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuadhimisha Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa wafu uletao maisha na uzima wa milele; ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu.

Maandamano ya toba na wongofu wa ndani
Maandamano ya toba na wongofu wa ndani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Katika maadhimisho ya Jumatano ya Majivu, Baba Mtakatifu Leo XIV ameongoza Ibada na maandamano ya toba na wongofu wa ndani kutoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Anselmi, lililoko kwenye kilima cha Avertino kuelekea kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina. Maandamano haya yamewashirikisha Makardinali, Maaskofu, Mapadre, Watawa na waamini walei, kielelezo cha hija ya toba na wongofu wa ndani tayari kuanza maandalizi ya kushiriki maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Baba Mtakatifu amebariki majivu na watu wa Mungu wakapakwa katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Majivu haya yanatokana na matawi yaliyotumika katika Dominika ya Matawi mwaka 2025. Kupakwa majivu katika paji la uso kuna maana kuu tatu. Kwanza, kama ishara ya unyenyekevu na utayari wa kufanya toba ya kweli na wongofu wa ndani, yaani “Metanoia.” Pili, majivu yanawakumbusha waamini kuwa maisha yao ya hapa duniani yana mwisho, kwa kuwa mwili huu upo katika hali ya uharibifu, hivyo wanapaswa kuwekeza katika maisha ya uzima wa roho zao. Tatu, majivu ni ishara ya mwanzo mpya, upya wa maisha ya kiroho, upya katika mahusiano yao, wao kwa wao; Upya katika mitazamo na fikra zao, lakini zaidi sana, upya katika Imani, matumaini na mapendo. Siku hii inawakumbusha waamini kuwa huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi na udhaifu wa kibinadamu. Mwenyezi Mungu yu tayari kumpokea yeyote aliye na nia ya dhati ya toba, wongofu wa ndani tayari kuanza maisha mapya. Itakumbukwa kwamba, hija hii ya Kipindi cha Kwaresima inafanywa kwenye Makanisa ambayo yanahifadhi masalia ya watakatifu na wafiadini, walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni fursa ya kupyaisha tena imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake, ili hata wakristo wa nyakati hizi, waweze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa.

Jumatano ya Majivu Mwanzo wa Kwaresima
Jumatano ya Majivu Mwanzo wa Kwaresima   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake, Jumatano ya Majivu 2026 amesema kwamba, Kipindi cha Kwaresima ni chemchemi ya furaha inayowakumbusha waamini kwamba, wanaitwa, kama Kanisa, yaani Jumuiya ya waamini kusikiliza Neno la Mungu na kwamba, huu ni mwaliko kwa watu wote katika hali na mazingira yao mbalimbali, ili kumlilia Mwenyezi Mungu, aweze kuwasamehe dhambi zao. Kwaresima ni kipindi muafaka cha watu wa Mungu kuweza kukusanyika, kwa kutambua dhambi na udhaifu wao, tayari kuwajibika kikamilifu mbele ya Mwenyezi Mungu! Hiki ni kitendo cha uaminifu na uujasiri na kwamba, Kanisa linaishi na kudumu katika Unabii kwa kutambua dhambi na makosa yake sanjari na miundo mbinu ya dhambi inayosimikwa katika masuala ya kiuchumi, kijamii, kitamaduni, kisiasa na hata kidini, kiasi hata cha waamini kuthubutu kuabudu miungu mingine. Mwenyezi Mungu aliye hai anawafunda waja wake kwamba, uhuru wa kweli unawawezesha watu wa Mungu kukusanyika, tayari kutubu na kumwongokea Mungu, kwani wanatambua kwamba, katika safari ya maisha yao wametenda dhambi. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika vijana wa kizazi kipya, kutambua dhamana na wajibu wao katika Kanisa: “Tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa.” 2 Kor 6:2. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani wa maisha, ili kuanza kuwa na mwelekeo mpya kuhusu Ufalme wa Mungu na haki zake. Kwaresima ni muda muafaka wa toba na wongofu wa ndani, ili mchakato wa uinjilishaji na ushuhuda wa tunu msingi za Injili uweze kuwa na mvuto na mashiko. Toba na wongofu wa ndani ni dai endelevu hata kwa watu wa Mungu katika Ulimwengu mamboleo, kwa kujikita katika ukweli na tunu msingi za Kiinjili kama alivyowahi kusema Mtakatifu Paulo VI na kwamba, maisha ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo ni kama “majivu.” Leo hii dunia inaendelea kuwaka moto wa vita, sheria za Kimataifa zinasiginwa; haki msingi za binadamu zinaendelea kutoweka “kama ndoto ya mchana”; zawadi ya uhai kutoka kwa Mwenyezi Mungu inakumbana na utamaduni wa kifo!

Jumatano ya Majivu Mwanzo wa Kwaresima.
Jumatano ya Majivu Mwanzo wa Kwaresima.   (@Vatican Media)

Hiki ni kifo katika maana yake ya ndani na kwamba, waamini wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa mateso, kifo na ufufuko wa wafu uletao uzima wa milele. Waamini watambue dhambi zinazowatafuna, wawe na ujasiri wa kufanya toba na wongofu wa ndani na kamwe wasibaki wakiwa wamegalagazwa kwenye majivu, bali wawe na ujasiri wa kusimama tena na kuendelea na safari ya ujenzi wa maisha mapya, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Maadhimisho ya Alhamisi, Kuu, Ijumaa Kuu na Jumamosi Kuu, ni Siku muhimu sana za maandalizi ya Sherehe ya Fumbo la Pasaka, lakini ziku hizi zitakuwa na manufaa, ikiwa kama waamini katika Kipindi hiki cha Kwaresima kwa njia ya toba na wongofu wa ndani wameweza kuvuka kutoka katika kifo na kuibukia maisha mapya kutokana na neema na baraka za Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kuendeleza Mapokeo ya Kale katika Kipindi hiki cha Kwaresima, kuzingatia Vituo vya Kwaresima: “Stationes”, kielelezo makini cha waamini kwamba, wao ni mahujaji. Vituo hivi vifufue ndani mwao kumbukumbu za mashuhuda wa imani, yaani wafiadini walioyamimina maisha yao kama mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. Huu ni mwaliko wa kutambua na kuthamini: maeneo, historia na majina ya wale walioyamimina maisha yao kwa kujitahidi kumwilisha Heri za Mlimani, Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Wao wamekuwa ni mbegu ya Ukristo na sasa imezaa matunda mengi na ajaa, zamu ya waamini katika Ulimwengu mamboleo kuvuna matunda haya. Kwaresima inapata maana yake kuwa ni wakati muafaka wa kumwilisha Injili katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni muda wa waamini kuzama katika maisha ya sala, toba na kufunga. Rej. Mt 6: 2.5.16. Kwaresima ni kipindi cha matendo ya huruma; Ni kipindi cha kufunga na kusali ili kuimarisha mahusiano na mafungamano na Mwenyezi Mungu, chemchemi ya furaha ya kweli kwa kujiaminisha kwake!

Papa Jumatano ya Majivu

 

 

 

19 Februari 2026, 15:26