Papa Leo XIV amemtumia salam za rambirambi Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania kufuatia kifo cha Kardinali Polycarp Pengo, Papa Leo XIV amemtumia salam za rambirambi Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania kufuatia kifo cha Kardinali Polycarp Pengo,  

Papa Leo XIV: Kardinali Pengo: Utume wa Kiaskofu; Malezi ya Kipadre na SECAM

Baba Mtakatifu Leo XIV anamshukuru Mungu kwa huduma ya Kiaskofu aliyoitekeleza Kardinali Polycarp Pengo katika majimbo kadhaa nchini Tanzania. Anamkumbuka hasa kwa sadaka na majitoleo yake katika malezi na majiundo ya awali na endelevu ya Makleri, Jimbo kuu la Dar es Salaam, bila kusahau huduma yake iliyotukuka kama Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar iliyosaidia kuwaunganisha Maaskofu wa Afrika kuwa wamoja tena.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Mzaburi anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima.” Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo!  Kristo Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini.

Hayati Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar.
Hayati Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar.

Ni katika muktadha wa Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu, Baba Mtakatifu Leo XIV amemtumia salam za rambirambi Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania kufuatia kifo cha Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam kilichotokea tarehe 19 Februari 2026 majira ya Saa 4:00 Usiku, akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar es Salaam. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kutoa salama zake za rambirambi kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam. Anamshukuru Mungu kwa huduma ya Kiaskofu aliyoitekeleza katika majimbo kadhaa nchini Tanzania. Anamkumbuka hasa kwa sadaka na majitoleo yake katika malezi na majiundo ya awali na endelevu ya Makleri, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kati ya Mwaka 2007 hadi mwaka 2009 alichaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, akafanikiwa kuwaunganisha Maaskofu wa Kusini mwa Afrika na Kaskazini, kwa kukazia moyo wa SECAM kujitegemea kwa rasilimali watu na vitu. Na katika maisha na utume wake kama Kardinali, aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Mabaraza mbalimbali ya Kipapa kwa ajili ya huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu Leo XIV anapenda kuiweka roho ya Kardinali Polycarp Pengo, Mchungaji mnyenyekevu, katika huruma ya Kristo Yesu, Mchungaji Mwema. Kwa waombolezaji na wote walioguswa na msiba huu mzito, huku wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele, anapenda kuwapatia faraja na baraka zake za kitume!

Kardinali Pengo alijisadaka kwa ajili ya malezi na majiundo ya Kipadre.
Kardinali Pengo alijisadaka kwa ajili ya malezi na majiundo ya Kipadre.

Familia ya Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania na Afrika katika ujumla wake, inamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam kwa maisha na utume wake kwa watu wa Mungu. Amelitumikia Kanisa kama Padre kwa miaka 54.66, kama Askofu kwa miaka 42.12 na kama Kardinali-Padre kwa miaka 27. Na tarehe 19 Februari 2026 majira ya Saa 4:00 Usiku, akaitwa nyumbani kwa Baba wa Milele akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar es Salaam, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Ijumaa tarehe 27 Februari 2026 mwili wa Hayati Kardinali Polycarp Pengo utawasili kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Dar es Salaam ili kutoa nafasi kwa waamini kutoa heshima zao za mwisho. Jioni saa 10: 00 kutaadhimishwa Ibada ya Misa Takatifu na baadaye kufuatiwa na kipindi cha sala na maombolezo. Jumamosi tarehe 28 Februari 2026 kuanzia saa 1:00 hadi Saa 3:45 waamini watapata fursa ya kutoa heshima zao za mwisho na hatimaye, Saa 4: 00 Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya mazishi ya Kardinali Pengo itaanza. Kardinali Pengo alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 20 Juni 1971, mikononi mwa Hayati Askofu Charles Msakila wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga (1958 – 1994), siku ambayo anasema Kardinali Pengo mwenyewe kwamba, kamwe hataweza kuisahau kwani tangu mwanzo kabisa alimwambia Mama yake kwamba, angetamani kuwa Padre na shuhuda wa imani kama alivyokuwa Mtakatifu Polycarp.

Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa SECAM: 2007-2009
Kardinali Polycarp Pengo, Rais wa SECAM: 2007-2009

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, wakati huo, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, Kardinali Pengo katika maisha na utume wake kama Padre na Askofu kuanzia: Nachingwea na Tunduru-Masasi, Kardinali Pengo ameweza kusimama imara bila kuteteleka katika masuala ya imani, maadili na utu wema. Na kwa njia ya msimamo wake, akaweza kuiepusha Tanzania katika dhoruba na mawimbi makali yaliyokuwa yanaisonga nchi kwa nyakati mbalimbali. Kardinali Pengo katika maisha na utume wake, amekuwa ni chombo na shuhuda wa majadiliano ya kiekumene, kidini, kisiasa na kitamaduni; mambo yaliyosaidia kujenga na kuimarisha maridhiano, umoja na mshikamano wa kitaifa; daima ni kiongozi aliyesimamia: ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi! Ni kiongozi aliyebahatika kuwa na kipaji cha unyenyekevu na usikivu, kiasi kwamba, alikuwa tayari kupokea watu, kuwasikiliza, kung’amua pamoja na kuwapatia ushauri. Kwa wale ambao wametekeleza kikamilifu ushauri wake, wamefanikiwa kupata suluhu ya changamoto zilizokuwa zinawaandama. Kardinali Polycarp Pengo ni kiongozi aliyebahatika kuwa na ushauri chanya katika changamoto za maisha. Katika maisha na utume wake, hasa kwa Jimbo kuu la Dar es Salaam, mafanikio makubwa yameonekana chini ya uongozi wake. Idadi kubwa ya Maaskofu walioko nchini Tanzania, wengi wao wamepitia mikononi mwake, kama wanafunzi na hata akawaweka wakfu kuwa Maaskofu, ili waweze kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Kardinali Pengo alijisadaka sana katika maisha na utume wake wa Kiaskofu
Kardinali Pengo alijisadaka sana katika maisha na utume wake wa Kiaskofu

Ni kiongozi ambaye amewathamini sana vijana, akawawekeza amana, utajiri, uzoefu na mang’amuzi yake katika malezi na makuzi yao, leo hii, Jimbo kuu la Dar es Salaam linaendelea kuwa na idadi kubwa ya miito mitakatifu si tu kwa watawa na watu wa ndoa, bali hata kwa wingi wa Mapadre. Ameimarisha malezi, makuzi na majiundo endelevu na fungamani kwa Mapadre wa Jimbo kuu la Dar es Salaam kama kielelezo cha ukomavu wa imani na mwanzo wa mchakato wa kujitegemea kwa rasimali watu, bila kusahau pia rasimali fedha. Jimbo kuu la Dar es Salaam ni kati ya Majimbo ambayo yana mwamko mkubwa katika kulitegemeza Jimbo kwa rasilimali fedha na vitu. Hizi ni juhudi za Kardinali Polycarp Pengo katika utume wake. Askofu Mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga anaendelea kufafanua kwamba, Kardinali Pengo ni mtu mwenye msimamo na malengo katika maisha na amejitahidi kuhakikisha kwamba, anatekeleza malengo yake kwa wakati. Kabla ya kung’atuka kutoka madarakani, alijipangia kwamba, Jimbo kuu la Dar es Salaam liwe limefikia Parokia 100, lakini hadi kufikia tarehe 15 Agosti 2019, Parokia za Jimbo kuu la Dar es Salaam ziliongezeka zaidi ya namba aliyokuwa amekusudia. Nia ilikuwa ni njema, kuhakikisha kwamba, waamini wa Jimbo kuu la Dar es Salaam wanapata huduma ya kichungaji kwa karibu zaidi. Askofu mkuu Nyaisonga anasema, shukrani hizi kwa Kardinali Polycarp Pengo ni kwa niaba ya familia yote ya Mungu, nchini Tanzania. Kwa sadaka na majitoleo yake, yaliyowawezesha watu wa Mungu nchini Tanzania licha ya mawimbi mazito katika medani mbalimbali za maisha, kuendelea kusimama na kushikamana kama ndugu wamoja. Bado familia ya Mungu nchini Tanzania inahitaji kutumia hekima, busara na mapaji aliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania.

Kanisa limempoteza Kardinali Pengo, Jabali la Maadili na utu wema
Kanisa limempoteza Kardinali Pengo, Jabali la Maadili na utu wema

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Polycarp Pengo, alizaliwa tarehe 5 Agosti 1944 huko Mwazye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 20 Juni 1971 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Na kwa kipindi cha miaka miwili yaani kuanzia mwaka 1971 hadi mwaka 1973 aliteuliwa kuwa Katibu wa Askofu Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Kati ya mwaka 1973 hadi mwaka 1977 alitumwa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga kuendelea na masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa la Lateran, Kitivo cha Taalimungu Maadili cha Alfonsianum, kilichoko mjini Roma. Aliporejea nchini Tanzania baada ya kuhitimu masomo yake, alitumwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwenda kufundisha taalimungu maadili, Seminari kuu ya Kipalapala, iliyoko Jimbo kuu la Tabora.Kuanzia mwaka 1978 hadi mwaka 1983 aliteuliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuwa Gambera na muasisi wa Seminari kuu ya Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kwa hakika, Kanisa la Tanzania linajivunia Seminari ya Segerea, matunda ya jasho na ubunifu wa Kardinali Polycarp Pengo. Tarehe 11 Novemba 1983 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Nachingwea na kuwekwa wakfu wakati wa Sherehe ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 1984 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na Mtakatifu Yohane Paulo II. Akasimikwa rasmi kuwa Askofu wa Nachingwea hapo tarehe 19 Februari 1984. Tarehe 17 Oktoba 1986, akatangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi, lengo likiwa ni kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kidini katika kukuza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Akasimikwa rasmi tarehe 12 Februari 1987. Tarehe 22 Januari 1990, Mtakatifu Yohane Paulo II, akamteuwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuingia Jimboni tarehe 24 Mei 1990.

Papa Leo XIV: Kardinali Pengo: Askofu, Malezi na SECAM
Papa Leo XIV: Kardinali Pengo: Askofu, Malezi na SECAM   (@Vatican Media)

Akasimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam tarehe 12 Februari 1992. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali na kumsimika rasmi tarehe 21 Februari 1999. Tanzania ikaweka historia ya kupata Kardinali mpya miezi michache tu baada ya kufariki dunia, Kardinali Laurian Rugambwa. Tarehe 2 Septemba 1990 wakati Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Tanzania, Kardinali Polycarp Pengo, aliyekuwa Askofu mkuu mwandamizi, ndiye aliyetoa hotuba, wakati Mtakatifu Yohane Paulo II alipokuwa anazungumza na wakleri pamoja na watawa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Alikazia kwa namna ya pekee uaminifu na upendo kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ari na mwamko wa uinjilishaji wa kina nchini Tanzania unaozingatia mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili. Tarehe 12 Aprili 1994, Kardinali Pengo alishiriki katika maadhimisho ya Sinodi ya Kwanza ya Maaskofu Barani Afrika na kukazia umuhimu wa waamini kumwilisha imani yao kila siku ya maisha kama ushuhuda wao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kati ya Mwaka 2007 hadi mwaka 2009 alichaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, akafanikiwa kuwaunganisha Maaskofu wa Kusini mwa Afrika na Kaskazini, kwa kukazia moyo wa SECAM kujitegemea kwa rasilimali watu na vitu! Kardinali Pengo alishiriki katika mkutano wa Baraza la Makardinali kwa ajili ya kumchagua Baba Mtakatifu Benedikto XVI na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko mwezi Machi 2013. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2019, Kardinali Polycarp Pengo, akang’atuka kutoka shughuli za uongozi Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kwa ufupi, hii ndiyo historia ya Kardinali Polycarp Pengo ambayo imeandikwa kwa jasho, uvumilivu na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo!

Papa Leo XIV Kifo Kardinali Pengo
21 Februari 2026, 13:16