2026.03.30 Wanachama wa Ligi ya Manispaa ya Illinois,Marekani. 2026.03.30 Wanachama wa Ligi ya Manispaa ya Illinois,Marekani.  (@VATICAN MEDIA)

Papa Leo XIV kwa Mameya wa Illinois:Heshima ya kila mtu lazima itambuliwe na kudumishwa

Papa Leo XIV alikutana na wanachama wa Ligi ya Illinois,Shirika la Mameya wa Mkoa wote linalowakilisha takriban Manispaa 1,300 za Mkoa nchini Marekani.Akikumbuka maneno ya La Pira,Papa Leo XIV aliwasihi kupunguza mateso kwa kila njia na ugumu wa raia wao na kusikiliza sauti za maskini na wahamiaji na kutoa huduma,wakizingatia mahitaji ya walio dhaifu na walio hatarini zaidi.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana na kuwakaribisha Wanachama wa Ligi ya Manispaa ya Illinois, Jumatatu tarehe 30 Machi 2026. Hawa ni Mameya wa miji ambao wanaunda Shirika la Mameya wa Mkoa wote, linalowakilisha takriban Manispaa 1,300 za Mkoa, nchini Marekani. Papa katika hotuba yake  alionesha furaha ya kukutana nao. Papa alisema kuwa wamefika Roma na kutembelea Vatican  wakati wa Juma  Takatifu, “ambapo Wakatoliki wote ulimwenguni, pamoja na Wakristo wengine wengi, wanakumbuka mateso, kifo na ufufuo wa Yesu, ambaye utii wake wa upendo kwa Baba hata kifo umepata zawadi ya ukombozi kwa wanadamu wote (taz. Flp 2:8).”

Mkutano wa Papa na mameya wa Manispaa ya Illinois
Mkutano wa Papa na mameya wa Manispaa ya Illinois   (@Vatican Media)

Kupitia Fumbo la Pasaka,Tumaini kwa wote wanaomwamini Kristo

“Kupitia Fumbo la Pasaka, Papa Leo XIV aliongeza kusema “Bwana anatuonesha kwamba hata hali ngumu na zenye changamoto zaidi zinaweza kubadilishwa kutoka ndani kwa nguvu ya upendo. Labda mateso hayawezi kuepukwa au kuondolewa kila wakati, lakini maana ya ukombozi inaweza kupatikana ambayo sio tu hurejesha heshima iliyopotea, lakini pia hufungua mlango wa maisha mapya. Hakika, ufufuo wa Yesu ndio chanzo kikuu cha tumaini kwa wote wanaomwamini Kristo na kusubiri ahadi ya uzima wa milele.”

Ushindi wa Bwana Mfufuka dhidi ya kifo

Ushindi wa Bwana Mfufuka dhidi ya kifo pia unafunua kwamba moyo wa mamlaka halisi ni utumishi, kwani Yesu hakuja “kutumikiwa, bali kutumikia, na kutoa uhai wake uwe fidia ya wengi” (Mt 20:28). Utumishi wake na utii wake kwa mapenzi ya Baba umesababisha tumaini la uhakika na amani ya kudumu kwa wanadamu wote. Kwa njia hiyo, ushindi uliotokana na kipaji cha Kristo cha nafsi unasimama kama taa na changamoto kwetu sote leo.”

Wanachma wa Ligi ya Manispaa ya Illinois
Wanachma wa Ligi ya Manispaa ya Illinois   (@Vatican Media)

Mfano wa La Pira Meya wa zamani wa Firenze

Kama wanaume na wanawake mwaliopewa jukumu la kutawala, Papa Leo alisisitiza “ninyi pia mnaitwa kugundua na kuonesha kipaji cha utumishi. Kwa njia fulani, mnaitwa kuwa makini na mahitaji ya wanyonge na walio dhaifu zaidi ili kuwasaidia kuelekea maendeleo kamili ya kibinadamu.” Papa alitoa mfano wa Meya wa zamani wa mji wa Italia kwamba “Kama Mtumishi wa Mungu  Giorgio La Pira, ambaye alikuwa meya wa zamani wa jiji la Italia la Firenze,  alivyowahi kusema, “mameya wanaitwa kupunguza mateso na matatizo miongoni mwa raia wao kwa kila njia inayowezekana” - nukuu -, "kwa hatua zote ambazo upendo unapendekeza na sheria hutoa" (Maandishi, VI, uk. 83).

Heshima ya kila mtu lazima itambuliwe na kudumishwa

Papa aliendelea kusema kwamba “li kufanya hivyo, lazima kwanza mjitahidi kujua matarajio ya watu pamoja na changamoto zao. Heshima ya kila mtu lazima itambuliwe na kudumishwa, kwani manispaa zao, si sehemu zisizojulikana, bali zina nyuso na historia zinazopaswa kutunzwa kama hazina za thamani (taz. Hotuba kwa Wanachama wa Chama cha Kitaifa cha Manispaa za Italia, 29 Desemba 2025). Ingawa kuna kazi nyingi zinazoshindania umakini wao kila siku, Papa Leo XIV aliwahimiza kuendelea “ kuwasikiliza maskini, wahamiaji, na walio wadogo kati yao, wakitafuta kusindikizana nao katika kazi yao ya kukuza manufaa ya wote na kwa ajili ya wote. Kwa njia hiyo, kila moja ya manispaa zao inaweza kuwa mahali pa kukutana kweli kati ya raia wote, ikitoa fursa kwa kila mtu kustawi.”

Wanachama wa Ligi ya Manispaa ya Illinois
Wanachama wa Ligi ya Manispaa ya Illinois   (@Vatican Media)

Endelea na kazi hiyo muhimu kila siku kwa furaha,kwa upendo na kwa bidii

Papa Leo XIV alipenda kuwahakikisha  maombi yake na kutoa shukrani kwa huduma ya kujitolea wanayotoa kila siku kwa wale waanaowatawala. Aliwaomba waendelee na kazi hiyo muhimu kila siku kwa furaha, kwa upendo, na kwa bidii, wakikumbuka kila wakati kwamba wale walio katika mamlaka pia ni watumishi wa Mungu (taz. Rum 13:6). Kwa maana hiyo, kuiga unyenyekevu wa Kristo kwa mapenzi ya Baba kutawafungulia zaidi nguvu ya kweli ya huduma na kuwawezesha kuleta amani tuliyopewa na Kristo Mfufuka kwa wapiga kura wenu. Papa aliwakabidhi wao na wapendwa wao  kwa maombezi ya Mtakatifu Francis Xavier Cabrini, ambaye aliwahudumia walio katika mazingira magumu zaidi kwa upendo na kujitolea sana kwa miaka mingi huko Chicago, na aliwabariki kwa furaha kila mmoja wao na wapendwa wao wote kutoka moyoni.

PAPA NA MAMEYA WA ILLINOIS

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.

30 Machi 2026, 13:00