Papa Leo XIV:Kila monasteri iwe shule ya huduma katika dunia yenye ubinafsi!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV, alikutana katika Ukumbi wa Mikutano, Jumatatu tarehe 30 Machi 2026 na Jumuiya Tatu za wamonaki wa kike na kiume kutoka: Monasteri ya Mtakatifu Scolastica huko Subiaco, Monasteri ya Mtakatifu Scolastica huko Cesena na Wabenedikitini wa Mtakatifu Scolastica huko Bari. Papa alianza na salamu zake akionesha furaha ya kuwa na mkutano huo, ambao pia alisema: “unatupatia fursa ya kutafakari pamoja kuhusu thamani ya karama ya Wabenediktini katika maisha yenu, katika maisha ya Kanisa na katika ulimwengu. Kwa kutambua "vyombo vya matendo mema", Mtakatifu Benedikto, katika Sura ya IV ya Kanuni, anatuhimiza "kujilinda na kila tendo la mtu"(48).
Kujua kusali na kusoma Neno la Mungu
Papa Leo XIV aliendelea: Ninyi, watawa wa Benediktini wa ndani, wamonaki wa kiume wa Wabenedikti, mnajua vizuri jinsi maombi, kusali masifu na kusoma Neno la Mungu, hasa katika ‘Lectio divina’, mnavyosaidia katika uangalifu huu, na kuwawezesha wale wanaoufanya kuelewa ukweli kuwahusu, katika kutambua udhaifu na dhambi zao wenyewe na katika kusherehekea neema na baraka za Bwana.” Papa alisisitiza: “ Hivi ndivyo hamu ya kuwa wake inavyofanywa upya ndani yetu na nadhiri ya kujitoa kwetu inavyothibitishwa. Kwa hivyo, Maandiko yanapaswa kuwa "lishe ya maisha yetu na ya tafakari yenu na maisha ya kila siku, ili muweze kushiriki uzoefu huu unaobadilisha"(Francisko Katiba ya Kitume Vultum Dei quaerere, 19).”
Njia ya utakaso wa mtu aliyewekwa wakfu,haijalishi ni ya bidii na msukumo kiasi gani
Hata hivyo, Papa aliendelea, “njia ya utakaso wa mtu aliyewekwa wakfu, ya mtawa, haijalishi ni ya bidii na msukumo kiasi gani, haiwezi kupunguzwa kuwa safari ya kibinafsi tu.” Kwa sababu Papa alisema “ Ina mwelekeo muhimu wa kijumuiya, ambapo kutangazwa kwa ukombozi wa Pasaka kunachukua umbo linaloonekana katika huduma ya kidugu, kielelezo cha upendo wa Kristo kwa Kanisa na kwa wanadamu.” Katika suala hilo, sinodi, iliyohamasishwa na Papa Francisko kama msingi kwa maisha ya Kanisa, inatafsiriwa katika monasteri kuwa utaratibu wa kila siku wa "kutembea pamoja", kusikilizana kwa pamoja, utambuzi wa jumuiya chini ya mwongozo wa Roho Mtakatifu, na ushirika na Kanisa mahalia na familia ya Wabenediktini.”
Maisha ya kimonaki hayaeleweki tu kama kujiondoa Ulimwengu wa nje
“Hili linajidhihirisha katika mkutano wa kidugu, Papa Leo alisema - katika sala ya pamoja na katika maamuzi ya pamoja, ambapo mamlaka na utii hukutana katika mazungumzo, ili kutafuta mapenzi ya Mungu pamoja. Maisha ya kimonaki hayawezi kueleweka tu kama kujiondoa kutoka katika ulimwengu wa nje. Ni njia ambayo upendo sawa na ule wa Bwana, unaweza kukua katika mioyo ya wanafunzi, tayari kushiriki na kusaidia, hata miongoni mwa watawa. Kwa hivyo, Papa alisisitiza kuwa “maisha ya kimonaki yatakuwa kielelezo kwa watu wote wa Mungu, katika ulimwengu ambao mara nyingi una sifa ya kujipenda na ubinafsi, na kutukumbusha kwamba kuwa wamisionari, kabla ya kufanya mambo, kunahitaji njia ya kuwa na kuendesha mahusiano.”
Katika hilo, Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa “Hapa tunaweza kutaja kipengele maalum cha maisha ya kimisionari yaliyofungwa: kile cha maombezi, ambapo Neno lililofanywa sala hutuunganisha na Kristo Mpatanishi, anayetuombea (taz. Ebr 7:25). Maombezi ni haki ya mioyo inayodunda kwa upatanisho na huruma ya Mungu(taz.Catechism of the Catholic Church, 2635),tayari kukusanyika na kumkabidhi Bwana furaha na huzuni, matumaini na wasiwasi wa watu wa leo na wa kila kizazi (taz. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican , Katiba ya Kichungaji ya Gaudium et spes, 1-KKK), na hii ni sehemu muhimu na ya msingi wa kazi waliyokabidhiwa.
Mfano wa Anna,alifanya nyumba ya Mungu kuwa makao yake
Papa Leo XIV aliendelea kusema kuwa “Mfano wa hili ni nabii wa kike Ana, ambaye “hakuondoka hekaluni, akiabudu kwa kufunga na kuomba usiku na mchana” (Lk 2:37). Akiwa mjane na sasa mzee, alikuwa ameifanya nyumba ya Mungu kuwa makao yake. Maombi na kujinyima chakula vilimpelekea kumtambua Masiha katika mtoto maskini na asiyejulikana aliyetolewa na Maria na Yosefu: vilimwezesha kutambua, ndani ya historia, uingiliaji kati wa Mungu na kuufanya kuwa tangazo la kinabii la furaha na tumaini kwa watu wote wa Israeli.”
Umuhimu wa malezi endelevu:Jumuiya inakuwa wakala hai
Unabii na utambuzi unatuongoza kwenye mada ya mwisho ambayo Papa Leo XIV alipenda kuzungumzia ambayo ni: malezi endelevu, hasa muhimu katika enzi kama yetu, alisitiza. Kwanza kabisa inajumuisha "kujua upendo wa Kristo unaopita maarifa yote"(Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Vyama vya Maisha ya Kitume, Maelekezo Cor Orans, 223) na ni msingi ili maisha yaliyowekwa wakfu “yaweze kutekeleza huduma yake, kwa monasteri, kwa Kanisa na kwa ulimwengu kwa njia inayofaa zaidi”(Cor Oran 236). Kwa njia hiyo Jumuiya nzima ndiyo wakala hai katika hili, kupitia sala, Neno, nyakati za sherehe na kufanya maamuzi, za majadiliano na ufufuko, zilizoishi na kushiriki katika ukuu wa upendo. Papa Leo XIV alisema kwamba hiyo ina maana ya kujitolea, kwao wote, kwa hekima na busara, kuhimiza kila nia njema na kuelekeza kila juhudi kuelekea ukuaji wa pamoja katika uwezo wa kutoa, ili kila monasteri iweze kuwa, kama Mtakatifu Benedikto alivyotaka, zaidi na zaidi "shule ya huduma ya Bwana" (taz. Dibaji ya Kanuni, 45).
Ushuhuda wa maisha yenu
Kwa kuhitimisha Baba Mtakatifu alisema “kaka na dada wapendwa, asanteni kwa wema mkubwa na uliofichwa mnaoufanyia Kanisa, kupitia sadaka yenu, sala yenu isiyokoma, huduma yenu, na ushuhuda wa maisha yenu. Endeleeni na kazi hiyo, ambayo ni "kazi ya Mungu" (taz Mtakatifu Benedikto, Kanuni, 43, 3).” Papa aliwakabidhi kwa Maria Mtakatifu sana, Mama wa Ukimya, Mwanamke wa Kusikiliza, kwa Mtakatifu Benedikto, Mtakatifu Scholastica, na kwa watakatifu wengi wa Kibenediktini na aliwabariki kutoka moyoni mwake.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.
