Baba Mtakatifu Leo XIV: Kumbukizi ya Kifo cha Papa Francisko 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumatatu ya Oktava ya Pasaka, tarehe 6 Aprili 2026 kwa upendo mkuu na katika mwanga wa Kristo Mfufuka amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, umegota mwaka mmoja sasa tangu Papa Francisko alipofariki dunia, na hivyo kuyatoa maisha yake kwa Mwenyezi Mungu, Jumatatu ya Oktava ya Pasaka, tarehe 21 Aprili 2025. Mama Kanisa anamkumbuka kwa ushuhuda mkuu wa imani na upendo. Baba Mtakatifu Leo XIV ametumia fursa hii kutoa mwaliko kwa waamini kuungana na Bikira Maria, Kikao cha Hekima, ili waweze kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa ukweli daima.
Ikuwa ni tarehe 21 Aprili 2025 Profesa Andrea Arcangeli, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya na Usafi ya Vatican alipotangaza rasmi kwamba, Baba Mtakatifu Francisko “Jorge Mario Bergoglio” aliyezaliwa tarehe 17 Desemba 1936 aliyekuwa anaishi mjini Vatican na Mwenyeji wa Vatican amefariki dunia saa 1:35 Asubuhi ya tarehe 21 Aprili 2025 katika chumba chake cha “Domus Santa Marta” Hosteli ya Mtakatifu Martha kutokana na ugonjwa wa: “Kiharusi, Kwa kupoteza fahamu, Koma pamoja na Ugonjwa wa Shinikizo la juu la damu. Baba Mtakatifu Francisko pia alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa: Mkamba, Kisukari pamoja na Shinikizo la damu. Uamuzi wa kifo hiki umeamriwa na rekodi iliyotolewa na chombo kinachojulikana kama “electrocardiothanatographic” na hivyo akatangaza kwamba, sababu za kifo cha Baba Mtakatifu Francisko kulingana na ufahamu wake na dhamiri nyofu ni hizo zilizotangazwa hapo juu anasema Profesa Andrea Arcangeli, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya na Usafi ya Vatican.
Nembo yake ya Kiaskofu: “Akamwangalia kwa huruma, akamchagua” “Miserando atque eligendo” ni maneno ya kauli mbiu ya yaliko kwenye Nembo la Kiaskofu ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko, kama kumbukumbu endelevu ya maisha ya wito wake alipokuwa kijana, pale Mwenyezi Mungu alipomwangalia kwa huruma na kumchagua. Shughuli za kichungaji kuhusu miito ni mchakato wa kukutana na Kristo Yesu, tayari kumchagua na kumwambata katika maisha. Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa maisha ya kiroho, aliouandika tarehe 29 Juni 2022, kwanza kabisa alijikabidhi kwa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Anasema, kwa kuhisi kwamba, mwisho wa maisha yake ya hapa dunia unakaribia na akiwa na tumaini hai katika uzima wa milele, alipenda kuelezea mapenzi yake kuhusu mahali pa kuzikwa kwake.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema siku zote amekabidhi maisha na huduma yake ya Kipadre na Kiaskofu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Bwana wetu Kristo Yesu pamoja na Bikira Maria Mtakatifu. Anaomba kwamba, maisha yake ya kibinadamu yabaki yakipumzika, katika Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, huku akingojea Siku ya ufufuo wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Alitamani kuona safari yake ya mwisho ya hapa duniani inaishia mahali patakatifu pa Bikira Maria, mahali ambapo alienda kwa ajili ya sala mwanzoni na mwishoni mwa kila hija ya kitume, ili kukabidhi nia yake kwa Bikira Maria pamoja na kumshukuru kwa unyenyekevu, kwa ulinzi na tunza yake ya kimama. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anaomba kaburi lake liwekwe kwenye Kikanisa cha Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani.”
Hayati Baba Mtakatifu Francisko alitaka kaburi lake lichimbwe ardhini, rahisi bila mapambo maalum bali libaki likiwa na maandishi ya pekee “Franciscus.” Gharama ya maandalizi na hatimaye maziko yake, zitagharimiwa na mfadhili ambaye amempanga, safari ya kuhamishiwa kutoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, tayari alikwisha kutoa maagizo kwa Kardinali Rolandas Makrikas, Kamishna Maalum wa Kipapa wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu. Hayati Baba Mtakatifu anawaombea thawabu stahiki kwa Mwenyezi Mungu wale wote waliompenda na watakaoendelea kumwombea. Anasema, alitolea mateso aliyokumbana nayo katika sehemu ya mwisho wa maisha na utume wake kwa Bwana kwa ajili ya amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu kati ya watu!
