Baraza la Maaskofu Katoliki Italia: Kaburi Tupu Chimbuko la Matumaini ya Kikristo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema, Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha Ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani. Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia watu maisha na uzima wa milele. Kwa ufufuko wake amewajalia waamini maisha mapya. Hiki ndicho kiini cha imani ya Kanisa kwamba, Kristo Yesu ameshinda dhambi na mauti na kuwa kifo hakina tena sauti ya mwisho juu ya maisha ya binadamu. Kuhusu Fumbo la Ufufuko, Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, huu ni ukweli ambao si rahisi kuupokea kwani daima mwanadamu anaandamwa na nguvu ya kifo ndani na nje ya maisha yake kwa njia ya dhambi inayokita mizizi yake katika maisha ya watu na kuwafanya wasiweze kuponyoka na kusonga mbele; wanapoandamwa na hali ya kukata na kujikatia tamaa; upweke hasi unaopekenya Injili ya matumaini; wasiwasi unaposhika kasi na hivyo kuondoa ile furaha ya Injili; pale waamini wanapojisikia kuelemewa na upweke hasi au kuhisi kwamba, wanasalitiwa au kukataliwa; wanapoelemewa na udhaifu wao, mahangaiko pamoja na changamoto za kila siku, hapo waamini wanahisi kuishiwa na matumaini na hivyo kushindwa kuona njia ya kuweza kuwaondoa katika hali kama hiyo!
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI katika ujumbe wake kwa ajili ya Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana kwa mwaka 2026, linarejea kwenye kaburi tupu, chimbuko la matumaini ya Kikristo, kielelezo makini ya kwamba Kristo Yesu amefufuka kwa wafu, ameshinda dhambi na mauti, mwaliko kwa waamini kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka anayeuangazia usiku wa maisha ya waja wake! “Hayupo hapa, amefufuka.” Lk 24: 5-6. Watu wa Mungu wanaendelea kuishi katika ulimwengu unaogubikwa na vita inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu, lakini waathirika wakuu ni maskini na wanyonge katika jamii: Haya ni maafa yanayoendelea kusababisha: Upweke hasi, mateso na mahangaiko makubwa, mchoko na hali ya kukata na kujikatia matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Kilio cha watoto kinasikika kutoka sehemu mbalimbali za dunia; wazee wakiendelea kubaki peke yao, kiasi kwamba, leo hii ubaya wa moyo limekuwa ni jambo la kawaida, kiasi kwamba ugumu wa mioyo ya watu unashinda Injili ya huruma; utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine unachukua nafasi ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Pasaka ya Bwana ni tukio ambalo linawarejesha Wakristo katika msingi wa imani yao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kielelezo kwamba, ubaya wa moyo na kifo ni mambo ambayo hayana usemi wa mwisho na kwamba, Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, bado yanaendelea kuwa wazi; mwanga wa Kristo Mfufuka unageuza alama za mateso kuwa ni chemchemi ya matumaini ya Kikristo yanayowawezesha waamini kusimama kidete bila kutoroka, kwani matumaini ya Kikristo ni nguvu ya upole na ustahimilivu na wala si kimbio lililo mbali na historia, bali huu ni wajibu ndani ya historia.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI., katika ujumbe wake wa Pasaka linakaza kusema, Kristo Mfufuka anawaalika waja wake, kamwe wasibaki kuwa watazamaji, bali wachague nuru, wasimame kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; wajaliane na hivyo kuwa ni ishara ya amani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kwa maana "huyu ndiye Mungu wetu: Yesu, Mfalme wa Amani. Mungu anayekataa vita, ambaye hakuna mtu anayeweza kumtumia kuhalalisha vita, asiyesikiliza maombi ya wale wanaopigana vita na kuwakataa, akisema: 'Ingawa mkizidisha maombi yenu, sitasikia; mikono yenu imejaa damu' (Is 1: 15). [...] Kristo, Mfalme wa Amani, bado anaendelea kukumbusha kuwa rehema ni Msalaba wako! ndugu!" (Leo XIV, Mahubiri, 29 Machi 2026). Kila tendo la wema, kila neno la faraja, kila mkono ulionyooshwa, kila upatanisho unaotafutwa, kila huduma iliyofichwa, kila kukataa vurugu, kila chaguo la haki na amani tayari ni kielelezo na ishara ya Fumbo la Pasaka, kipande cha Ufufuo katika moyo wa ulimwengu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI., linasema katika mwanga wa Pasaka linapenda kutoa mawazo ya pekee kwa wale wanaoteseka, huku wakisubiri ishara ya ukaribu nchini Italia yaani: Wagonjwa, wafungwa, watu wasiokuwa na fursa za ajira, wanaoteseka na kuangaika kuelimisha, wale wanaoelemewa na upweke katika maisha yao; watu ambao hawawezi kuona tena mbele. Watambue kwamba, Kristo Mfufuka anasimama kando ya kila mmoja wao kama mwandani wa safari ya maisha, kama ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wa Emau, kielelezo cha safari ya maisha ya kiroho sanjari na ufunuo wa Kristo Yesu katika kuumega Mkate. Anawasha noyo zao, anayafungua macho yao na kuwarejesha tena njiani. Rej Lk 24:13-35. Kanisa Katoliki nchini Italia linawatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, maadhimisho ya Pasaka ya Mwanga, ili Kristo Mfufuka aweze kuyaangazia macho ya nyoyo zao, awe faraja kwa wale wote wanaoomboleza; awasimamishe tena wale walioteleza na kuanguka; awaimarishe waliovunjika na kupondeka nyoyo kwa udhaifu. Awakirimie ujasiri katika kutenda mema; awajalie uvumilivu katika majaribu ya maisha na waaminifu katika Injili ya upendo. Kristo Mfufuka awakirimie waamini wote uwezo wa uwepo wake angavu, ili katika nyumba, jumuiya na sehemu zenye mateso na mahangaiko ya maisha ya kila siku, wapate tena fursa ya kusikia kwamba, Kristo Yesu amefufuka na anaishi kati yao!
