Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Algeria kuanzia tarehe 13 hadi 15 Aprili 2026 inanogeshwa na kauli mbiu: “Amani iwe nanyi” Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Algeria kuanzia tarehe 13 hadi 15 Aprili 2026 inanogeshwa na kauli mbiu: “Amani iwe nanyi”   (ANSA)

Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Barani Afrika: Algeria! Mashahidi na Ddiplomasia

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Algeria kuanzia tarehe 13 hadi 15 Aprili 2026 inanogeshwa na kauli mbiu: “Amani iwe nanyi” changamoto na mwaliko kwa Wakristo na waamini wa dini ya Kiislam kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, udugu wa kibinadamu na maridhiano. Anasema, yeye si mwanasiasa bali mtangazaji na shuhuda wa Habari Njema ya Wokovu na anataka kukazia haki na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema yeye si mwanasiasa, bali anatangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na kwamba, anawahimiza viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano na wala hataki kujiingiza katika malumbano na utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani. Adhani kwamba ujumbe wa Injili unapaswa kutumiwa vibaya kama watu wengine wanavyofanya. Ataendelea kusema kwa ukali dhidi ya: vita, atatafuta kukuza amani, majadiliano na ushirikiano wa pande nyingi kati ya watu ili kutafuta suluhisho la changamoto na matatizo yanayoendelea kuwasibu binadamu. Watu wengi wanateseka, watu wasio na hatia wanaendelea kupoteza maisha na kwamba, watu lazima wasimame na kusema ukweli kwa njia bora zaidi. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV nchini Algeria kuanzia tarehe 13 hadi 15 Aprili 2026 inanogeshwa na kauli mbiu: “Amani iwe nanyi” changamoto na mwaliko kwa Wakristo na waamini wa dini ya Kiislam kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, udugu wa kibinadamu na maridhiano. Rais Sergio Mattarella wa Italia, akijibu ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV aliomwandikia wakati akianza hija yake ya Kitume ya Siku Kumi Barani Afrika anasema, Bara la Afrika lina idadi ndogo ya watu duniani, lakini Ukristo una mizizi ya kale na ya kina kama ilivyothibitishwa na Mtakatifu, Augostin Baba na Mwalimu wa Kanisa. Afrika ni Bara changa linalopitia mabadaliko na hivyo kuwa ni ishara ya matumaini makubwa na kwamba, hatima yake inahusishwa na Italia na Bara la Ulaya katika ujumla wake. Huu ni mwaliko wa kutambua na hatimaye kutoa majibu ya: matatizo, fursa na changamoto kuu hasa kutokana na athari za vita, kinzani na migogoro; utandawazi; mogogoro ya kidini na kimadhehebu, shinikizo la idadi ya watu; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, matumizi mabaya ya rasilimali hadi athari za mabadiliko ya tabianchi.

Baba Mtakatifu Leo XIV anatembelea Afrika katika hujaji na mjumbe wa amani
Baba Mtakatifu Leo XIV anatembelea Afrika katika hujaji na mjumbe wa amani   (ANSA)

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kuhusu: Utakatifu, amani, upatanisho na matumaini ni muhimu sana katika kutangaza na kushuhudia imani, kukuza maadili, Injili ya uhai na usawa ni mambo msingi sana katika mchakato wa ujenzi wa upeo wa utulivu, ustawi, mafao na ulinzi kwa wote. Rais Sergio Mattarella wa Italia, anasema wito wa haraka wa amani ni wa dharura sana katika Ulimwengu unaogubikwa katika misukosuko, pamoja na mwaliko wa umoja na udugu wa kibinadamu ni muhimu katika kukuza ufahamu utakaosaidia kuondoa migawanyiko, ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu. Haya ni maombi mazito yanayopaswa kuvaliwa njuga na vijana wa kizazi kipya, ili kuwajibika na hatimaye kupata furaha ya kuwa ni mbegu inayozaa matunda ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa nchi na Jumuiya zao. Baba Mtakatifu Leo XIV alipowasili nchini Algeria Jumatatu tarehe 13 Aprili 2026 ametembelea Mnara wa Mashahidi wa Maqam Echahid. Katika hotuba yake amekazia tunu msingi za: Urafiki, uaminifu na mshikamano mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha na hivyo kuwawezesha kushinda majaribio mbalimbali kwa ujasiri na uadilifu. Mnara huu ni kielelezo cha heshima kwa historia ya Algeria na roho ya watu waliopigania uhuru, utu na heshima ya Taifa la Algeria. Kumbe kuna haja ya kujizatiti katika kukuza na kudumisha: haki, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mwenyezi Mungu anatamani amani kwa kila Taifa, amani ambayo ni kielelezo cha haki, utu na heshima ya binadamu; amani inayosimikwa katika roho ya msamaha na upatanisho dhidi ya chuki na uhasama na kwamba, haki daima itashinda udhalimu na vurugu haitakuwa na neno la mwisho. Algeria iendelee kujizatiti katika majadiliano ya kidini, haki na umoja na kwamba udugu wa kibinadamu na upatanisho ni zawadi kutoka kwa Mungu. Mnara huu ni ishara ya wazi ya watu waliosadaka maisha yao kama kielelezo cha upendo kwa watu nchini mwao, mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Algeria kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu.

Papa Leo XIV amewahutubia viongozi wa Serikali na wanadiplomasia
Papa Leo XIV amewahutubia viongozi wa Serikali na wanadiplomasia   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Leo XIV amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Wanadiplomasia wanaowakilisha Nchi zao pamoja na Mashirika ya Kimataifa, Wafanyabiashara maarufu pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia na kitamaduni. Amewakumbusha kwamba, yuko miongoni mwao kama hujaji wa amani, mwenye shauku ya kukutana na watu watakatifu wa Mungu nchini Algeria kwa kutambua kwamba, wao ni ndugu wamoja hivyo wanapaswa kukuza na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na upatanisho, mambo ambayo hija hii ya kitume inataka kuacha kama ishara ya kudumu. Katika ulimwengu uliojaa migogoro na kutokuelewana, watu wajitahidi kukutana kwa kutambua kwamba, wao wote ni familia moja. Amewapongeza watu wa Algeria kwa moyo wao wa ukarimu na kwamba, sadaka ni kielelezo cha haki na umuhimu wa kutekeleza Sheria ya Kimataifa kama njia ya kupambana na athari za ukoloni mamboleo, ukosefu wa usawa na hivyo kujikita katika utekelezaji wa kanuni maadili na utu wema na kwamba, uongozi ni kielelezo cha huduma makini inayosimikwa katika: haki, amani, ustawi na mafao ya wengi. Kanisa nchini Algeria ni daraja kati ya Mashariki na Magharibi. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kwa maana bahari na jangwa vimekuwa mahali pa amana na utajiri wa pamoja kati ya watu na tamaduni kwa kipindi cha milenia pasigeuzwe kuwa ni makaburi ya watu. Huu ni mwaliko wa kuzidisha chemchemi za amani, wakemee na kuondoa sababu za watu kukata na kujikatia tamaa kwa kujikita katika kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wajitahidi kuunganisha nguvu, roho, akili na rasilimali ili kweli ardhi na bahari viwe mahali pa watu kuishi, kukutana na kushangaa.

Papa Leo XIV: Majadiliano ya kidini ni muhimu katika kudumisha amani
Papa Leo XIV: Majadiliano ya kidini ni muhimu katika kudumisha amani   (@Vatican Media)

Algeria kama ilivyo katika sehemu mbalimbali za dunia kuna watu wenye misimamo mikali ya kiimani na kidini sanjari na utengano mambo yanayowafanya wengi kupoteza hisia halisi ya Mwenyezi Mungu na adhama ya viumbe vyake vyote.  Kwa hivyo, alama na maneno ya kidini yanaweza kuwa, kwa upande mmoja, lugha za kufuru, vurugu na ukandamizaji, au kwa upande mwingine, ishara ya utupu katika soko kubwa la matumizi ambayo hayawaridhishi watu. Ili kupambana na mwelekeo huu, Baba Mtakatifu Leo XIV anakazia umuhimu wa elimu katika fikra makini na uhuru; watu wajenge utamaduni wa kusikiliza na kujadiliana; watambue tofauti zao msingi ni utajiri na amana na kamwe visiwe ni vitisho. Watu wajielekeze katika uponyaji wa kumbukumbu na upatanisho kati ya wapinzani wa zamani.  Hii ndiyo zawadi ambayo Baba Mtakatifu Leo XIV anaitamani kwa Nigeria na kwa watu wake wote. Baba Mtakatifu Leo XIV amepata bahati ya kutembelea Msikiti mkuu wa Algiers peku peku na kupata nafasi ya kutafakari kidogo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu na hatimaye kutia saini kwenye Kitabu cha watu mashuhuri.

Kanisa kuu la Bikira Maria wa Afrika Algeria: Sala, Huruma na Amani
Kanisa kuu la Bikira Maria wa Afrika Algeria: Sala, Huruma na Amani   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatatu tarehe 13 Aprili 2026 amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na Jumuiya ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini Algeria katika Kanisa kuu la Bikira Maria wa Afrika Algiers alama ya ushirika, majadiliano na amani katika ulimwengu mamboleo. Katika hotuba yake Baba Mtakatifu Leo XIV amekezia umuhimu wa: Sala inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Sala inaunganisha, inatuliza na kutakasa moyo. Pili ni matendo ya huruma kwa walemavu na wadhaifu ambayo kimsingi ni chemchemi ya neema ma baraka; chanzo cha maisha mapya na uponyaji; ni mahali pa kushirikishana furaha na machungu; kuaminiana na ujenzi wa urafiki na udugu wa kibinadamu. Wafidia dini wa Algeria ni mashuhuda wa imani, ujasiri na kwamba, wao ni chemchemi ya matumaini kwa Waalgeria na ni mbegu ya majadiliano ya kidini na kitamaduni, msingi wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu na mshikamano. Tatu, Baba Mtakatifu anawataka wawe ni waragibishaji wa amani na umoja unaochota amana na utajiri wake kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kutangaza na kueneza udugu wa kibinadamu, ushirika na upatanisho. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewatia shime watu wa Mungu nchini Algeria kama Jumuiya ya imani, kielelezo cha uwepo hai wa Kanisa kuendelea kuwa Sakramenti ya wokovu kwa walimwengu wote. Amewashukuru na kuwapongeza kwa sala, ushuhuda na ujenzi wa umoja wao.

Hija ya Kitume Algeria

 

13 Aprili 2026, 17:11