Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumatatu tarehe 13 hadi 23 Aprili 2026 anafanya hija ya kitume ya Siku 10 kwa kutembelea miji 11nchini Algeria, Cameroon, Angola pamoja na Guinea ya Ikweta “Equatorial Guinea.” Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumatatu tarehe 13 hadi 23 Aprili 2026 anafanya hija ya kitume ya Siku 10 kwa kutembelea miji 11nchini Algeria, Cameroon, Angola pamoja na Guinea ya Ikweta “Equatorial Guinea.” 

Hija ya Kitume ya Papa Leo XIV Barani Afrika: Kuanzia Tarehe 13-23 Aprili 2026

Papa Leo XIV kuanzia Jumatatu tarehe 13 hadi 23 Aprili 2026 anafanya hija ya kitume ya Siku 10 kwa kutembelea: Algeria, Cameroon, Angola pamoja na Guinea ya Ikweta. Baba Mtakatifu Leo XIV anatembelea Barani Afrika kama shuhuda wa matumaini, amani na upatanisho Mkazo ni kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inajikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho, ili kweli Afrika iwe ni mahali pazuri pa kuishi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija za Kitume za Khalifa wa Mtakatifu Petro nje ya Vatican zinapania pamoja na mambo mengine: kuwatia shime, ari na mwamko wa kimisionari, watu watakatifu wa Mungu ili wawe tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi Kristo Yesu ili kwa njia ya: Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma aweze kuwagusa na kuwatakasa kutoka katika undani wa maisha yao, kama ilivyokuwa kwa yule mtu kipofu tangu kuzaliwa kwake. Rej Yn 9:1-25. Hii ni changamoto ya kusikiliza kwa makini na hatimaye kumwilisha tunu msingi za Kiinjili, Kiutu, Kitamaduni, Kijamii na Kisiasa katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji na kama sehemu mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili mambo ambayo ni sawa na chanda na pete. Rej. Yn 9:1-25. Ni hija zinazopania kuwaimarisha watu wa Mungu katika imani, matumaini na mapendo, kielelezo makini cha imani tendaji. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia Jumatatu tarehe 13 hadi 23 Aprili 2026 anafanya hija ya kitume ya Siku 10 kwa kutembelea miji 11nchini Algeria, Cameroon, Angola pamoja na Guinea ya Ikweta “Equatorial Guinea.” Baba Mtakatifu Leo XIV anatembelea Barani Afrika kama shuhuda na mjumbe wa matumaini, amani na upatanisho. Hapa mkazo ni kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inajikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho, ili kweli Bara la Afrika liweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi! Kanisa ni chombo na shuhuda wa upatanisho, dhamana ambayo limepewa na Kristo Yesu!

Papa Leo XIV akiwa na ujumbe kutoka Algeria
Papa Leo XIV akiwa na ujumbe kutoka Algeria   (@Vatican Media)

Kanisa linawaalika na kuwahimiza waamini kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao pamoja na kujipatanisha na mazingira, nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Hiki ni kipindi kilichokubaliwa cha kufanya toba na wongofu wa ndani; tayari kuambata huruma, msamaha na upendo wa Mungu. Kwa hakika kuna haja ya kutubu, kuongoka na kujipatanisha na Mungu. Waamini Barani Afrika wawe ni vyombo, mashuhuda na mabalozi wa upatanisho ndani ya jamii zao. Hii ni dhamana waliyojitwalia walipopokea Sakramenti ya Ubatizo inayowashirikisha kwa namna ya pekee: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu katika maisha yao! Baba Mtakatifu Leo XIV anafanya Hija yake ya Tatu ya Kitume, tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki mwezi Mei, 2025. Tayari amekwisha kutembelea Uturuki na Lebanon kati ya Mwezi Novemba na Desemba 2025 kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Na tarehe 28 Machi 2026 ametembelea Nchi ya Ufalme wa Monaco. Hii ni hija ambayo inamkutanisa Baba Mtakatifu Leo XIV na: Lugha na Tamaduni mbalimbali za watu wa Bara la Afrika. Ni Bara ambalo pamoja na utajiri wake wote wa rasilimali za asili ana watu wake, lakini bado linasiginwa na baa la njaa, umaskini, magonjwa, vita; misimamo mikali ya kidini, mashambulizi ya kigaidi; wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum; ukosefu wa fursa za ajira na changamoto kwa vijana wa kizazi kipya ambao wanawakilisha sehemu kubwa ya idadi ya watu Barani Afrika; dhamana, utume na mchango wa dini mbalimbali katika kukoleza ustawi, maendeleo, mafao ya wengi; haki, amani na maridhiano.

Watu wa Mungu nchini Cameroon wanamsubiri Papa Leo XIV
Watu wa Mungu nchini Cameroon wanamsubiri Papa Leo XIV   (AFP or licensors)

Huu ni ufafanuzi wa Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV uliotolewa na Dr. Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican, kwa vyombo vya mawasiliano ya jamii Alhamisi tarehe 9 Aprili 2026. Baba Mtakatifu anaanza Hija yake ya Kitume nchini Algeria, nchi ambayo ina idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam.Takwimu zinaonesha kwamba, Algeria ina idadi ya watu milioni 48 na kati yao Wakristo ni milioni 10. Hii ni nchi yenye urithi wa amana na utajiri wa maisha ya kiroho ya Mtakatifu Augustini wa Hippo, Askofu na Mwalimu wa Kanisa; Muasisi wa Shirika la Waagostiani “The Order of St. Augustine, OSA.” Tangu mwanzo wa maisha na utume wake, Baba Mtakatifu Leo XIV alitia nia ya kutembelea maeneo ya maisha na utume wa Mtakatifu Augustini, ili kuendeleza majadiliano ya kidini na kitamaduni, ili kuwasaidia Wakristo Kaskazini mwa Afrika, kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hili ni eneo lenye changamoto ya wimbi kubwa ya wahamiaji na wakimbizi kutoka Barani Afrika. Kituo cha Pili cha Hija ya Baba Mtakatifu Leo XIV ni Cameroon yenye amana na utajiri mkubwa wa rasilimali asilia, na nchi yenye matumaini, lakini inakabiliwa na changamoto ya haki, amani na upatanisho. Hii ni nchi inayokabiliwa na changamoto kubwa ya misimamo mikali ya imani na kidini, mwaliko kwa watu wote wa Mungu kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli, haki na upendo. Huu ni wakati pia wa kuwahimiza watu wa Mungu kujikita kikamilifu katika ulinzi na utunzaji wa mazingira bora nyumba ya wote, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 10 tangu Hayati Baba Mtakatifu Francisko alipochapisha Waraka wa Kitume wa Laudato si.

Kumbukizi ya Miaka 10 tangu Papa Francisko achapishe Laudato si
Kumbukizi ya Miaka 10 tangu Papa Francisko achapishe Laudato si   (@Vatican Media)

Ilikuwa ni tarehe 24 Mei 2015, Baba Mtakatifu Francisko alipochapisha Waraka wa Kitume wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa mazingira nyumba ya wote.” Huu ni Waraka unaozungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa ikolojia vinavyohusiana na watu; Ikolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya ikolojia na maisha ya kiroho. Kumbe, kimsingi Baba Mtakatifu Leo XIV katika hotuba zake pamoja na mambo mengine atagusia kuhusu: Injili ya haki na amani; rasilimali asilia na watu; madonda ya rushwa na ukwapuaji wa mali ya umma, pamoja madhara ya ukoloni mkongwe.Kituo cha Tatu cha Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Leo XIV Barani Afrika ni Angola inayojipambanua kuwa ni nchi changa yenye rutuba kubwa ya imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Na Kituo cha Nne cha Hija ya Papa Leo XIV Barani Afrika ni katika nchi ya Guinea ya Ikweta “Equatorial Guinea” inayokabiliana na hali tete ya kisiasa. Hii ni nchi ilibarikiwa kuwa na madini mengi; ni nchi yenye waamini wengi wa Kanisa Katoliki wanaojisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Leo XIV anataka kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo, ili hatimaye waweze kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Injili ya amani.

Baraza la Maaskofu Katoliki Angola
Baraza la Maaskofu Katoliki Angola   (©Sheila Pires, Joanesburgo (África do Sul))

Katika hija hii ya Kitume, Baba Mtakatifu Leo XIV anaambatana na: Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu; Kardinali George Jacob Koovakad, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini; Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu pamoja na Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa. Orodha hii inakamilishwa na Askofu Mkuu Paolo Rudelli, Katibu Mkuu Msaidizi wa Vatican aliyechukua nafasi ya Askofu mkuu Edgar Peña Parra aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Leo XIV kuwa Balozi wa Vatican nchini Italia na San Marino. Baba Mtakatifu Leo XIV anatumia fursa hii kukutana na watu wa Mungu na wanasiasa na kwamba, wote hawa analo neno la kushirikishana nao! Hija hii ya kitume inafanywa na Baba Mtakatifu Leo XIV wakati, Mama Kanisa akijiandaa kufanya kumbukizi ya Mwaka Mmoja tangu Papa Francisko alipofariki dunia, tarehe 21 Aprili 2025.

Hija ya Kitume barani Afrika
10 Aprili 2026, 15:44