Papa Leo XIV:Sala,upendo na umoja ni uhai wa Wakristo wa Algeria!

Papa Leo XIV akikutana na Jumuiya ya Wakristo nchini Algeria aliwasihi walendelezae mizizi ya sala,upendo na umoja,unaojitambulisha nchi hiyo na kuwapongeza ushuhuda wao sadaka yao.Alihimiza kutazama taswira ya jangwa,ambalo ni sehemu kubwa ya nchi yao,ili kutambua udhaifu wake dhidi ya dhana yoyote ya kujitosheleza.Papa alikaa mbele ya ukumbusho wa waathirika wa ajali ya meli na kusali kimya.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Basilika ya Mama Yetu wa Afrika huko Algiers  inatazama Bahari ya Mediterania kutokea juu, ikiwa imeegemea kwenye sehemu ya juu zaidi ya mita 120 juu ya usawa wa bahari. Hii ni sehemu yenye rutuba, lakini pia ukame ambao ni ukweli wakati mwingine unaoonekana kuamsha jangwa, hata kama hiyo ingeweza kuonekana kitendawili, kutokana na siku ya mvua iliyo nyesha sana katika mji mkuu wa Algeria. Ni katika Kanisa hilo  ambapo Papa Leo XIV katika siku ya kwanza ya Hija yake ya Kitume tarehe 13 Aprili 2026 aliweka mguu  kwa kumalizia siku, akikutana na Jumuiya mahalia.

Papa katika Basilika ya Mama Yetu wa Afrika
Papa katika Basilika ya Mama Yetu wa Afrika   (@Vatican Media)

Urithi wa kale na mashahidi wa imani wanaong'aa

Baada ya kukaribishwa na Kardinali Jean-Paul Vesco, Askofu Mkuu wa Algiers na kuwakaribisha baadhi ya walio toa ushuhuda, huku wakisindikizwa na nyimbo, Baba Mtakatifu alitoa tafakari iliyojikita na mambo matatu:  Sala, upendo na umoja. Papa alianza  kusema: "Amani iwe nanyi! Wapendwa ndugu katika Uaskofu, Wapendwa mapadre na mashemasi, wanaume na wanawake watawa, Wapendwa watoto wa Kanisa nchini Algeria. Ni kwa furaha kubwa na upendo wa kibaba ninapokutana nanyi leo, ninyi ambao uwepo wenu wa kipekee na wa thamani katika nchi hii unaoneshwa na urithi wa kale na mashahidi wa imani wanaong'aa. Jumuiya yenu ina mizizi mirefu kweli. Ninyi ni warithi wa kundi la mashahidi waliotoa maisha yao, wakichochewa na upendo kwa Mungu na jirani.”

Damu yao ni mbegu isiyo acha kuzaa matunda

"Ninakumbushwa hasa kuhusu wanaume na wanawake kumi na tisa watawa waliouawa kishahidi nchini Algeria, Papa aliongeza " wakichagua kusimama kidete pamoja na watu hawa katika furaha na huzuni zao. Damu yao ni mbegu hai ambayo haiachi kamwe kuzaa matunda. Pia ninyi ni warithi wa utamaduni wa kale zaidi, unaoanzia karne za mwanzo za Ukristo. Katika nchi hii ilisikika sauti ya bidii ya Agostino wa Hippo, ikitanguliwa na ushuhuda wa mama yake, Mtakatifu Monica, na wa watakatifu wengine. Kumbukumbu yao inang'aa kama wito wa kuwa ishara halisi za ushirika, mazungumzo na amani leo."

Papa akitoa tafakari yake
Papa akitoa tafakari yake   (@Vatican Media)

Sala, Upendo na Umoja

"Kwa marafiki wote wapendwa, na kwa wale ambao hawakuweza kuwepo, lakini wanafuatilia mkutano huu kutoka mbali, Papa Leo XIV aliongeza "ninatoa shukrani zangu kwa kujitolea kwenu kila siku kudhihirisha moyo wa kimama wa Kanisa.” Papa Leo XIV aliwashukuru wote waliotoa ushuhuda kwa maneno yao kuanzia kwa Kardinali Vesco pia Rakel, Ali, Monia na Sr Bernadette kwa yale yote waliyoshirikisha. Kwa kuzingatia yale yaliyosikika Papa alipenda kutafakari pamoja kuhusu vipengele vitatu vya maisha ya Kikristo ambavyo aliviona kuwa ni muhimu , hasa kwa kuzingatia uwepo wao hapo kuhusu: sala, upendo na umoja.

Sala

Kwanza, sala. Sote tunahitaji kuomba. Mtakatifu Yohane Paulo II alisisitiza hili alipowaambia vijana: “Mwanadamu hawezi kuishi bila sala, zaidi ya vile anavyoweza kuishi bila kupumua” (Mkutano na Vijana Waislamu huko Casablanca, 19 Agosti 1985, 4). Aliwasilisha mazungumzo na Mungu kama muhimu sana  si tu kwa maisha ya Kanisa, bali pia kwa kila mtu binafsi. Mtakatifu Charles de Foucauld pia alitambua hili, na akakubali wito wake kama uwepo wa maombi. Aliandika: “Nina furaha, kuwa mbele ya Sakramenti Takatifu wakati wote” (Barua kwa Raymond de Blic, 9 Desemba 1907) na aliwasihi wengine: “Ombeni sana kwa ajili ya wengine. Jitoe  kwa wokovu wa jirani yako kwa kila njia katika uwezo wako: kwa sala, kwa wema, kwa mfano” (Barua kwa Louis Massignon, 1 Agosti 1916).

Nyimbo zilisindikiza shuhuda mbali mbali
Nyimbo zilisindikiza shuhuda mbali mbali   (@Vatican Media)

"Kuhusu hitaji letu la sala, Papa alisisitiza kwamba " Ali alishirikisha uzoefu wake wa huduma katika Basikia ya Mama Yetu wa Afrika , ambapo wengi hufika na kuingia kimya, kuelezea wasiwasi wao, kuwaombea wapendwa wao, na kukutana na mtu aliye tayari kuwasikiliza ili waweze kushirikisha mizigo waliyobeba mioyoni mwao." Alibainisha kuwa "wengi hupata amani hapa na wanafurahi kwamba  wamefika. Sala huunganisha, humfanya mtu kuwa binadamu, huimarisha na kutakasa moyo. Kupitia sala, Kanisa nchini Algeria hupanda ubinadamu, umoja, nguvu na usafi, na kufikia maeneo yanayojulikana kwa Bwana pekee."

Upendo

Papa alisisitizia kipengele  cha maisha ya Kanisa ambacho alipenda kuzingatia cha Upendo. "Sr Bernadette alizungumza nasi kuhusu hili hasa, katika kushirikisha uzoefu wake wa kuwasaidia watoto wenye ulemavu na wazazi wao. Kutokana na yale aliyoshirikisha, Baba Mtakatifu aliongeza, "tumeelewa kwamba huruma na huduma ni zaidi ya kutoa msaada wa kimwili kwa wanyonge zaidi miongoni mwetu. Zaidi ya yote, vitendo hivyo huwa fursa ya neema, kuwezesha kila mtu anayehusika kukua na kutajirika. Sr Bernadette alielezea jinsi ishara rahisi, ya awali ya ukaribu - kuwatembelea wagonjwa - ilivyokua kwanza katika kituo cha jamii na kisha katika shirika la utunzaji lenye muundo unaoongezeka."

Msichana kutoka Kenya akitoa ushuhuda
Msichana kutoka Kenya akitoa ushuhuda   (@Vatican Media)

Sasa imekuwa jumuiya halisi, ambapo watu wengi hushiriki nyakati za furaha na huzuni, wakiwa wameunganishwa na vifungo vya uaminifu, urafiki na ushirika. Mazingira kama hayo yanatoa uhai na uponyaji, na haishangazi kwamba wale wanaoteseka wanaweza kupata ndani yake rasilimali wanazohitaji ili kuboresha afya zao, huku wakileta furaha kwa wengine, kama ilivyokuwa kwa Fatima.

Upendo kwa kaka na dada

Baada ya yote, Papa alisema "ni upendo hasa kwa kaka na dada zao ndiyo uliochochea ushuhuda wa mashahidi ambao tumewakumbuka." Katika kukabiliana na chuki na vurugu, waliendelea kuwa waaminifu kwa upendo hata kufikia hatua ya kujitoa mhanga pamoja na wanaume na wanawake wengine wengi, Wakristo na Waislamu. Walifanya hivyo bila kujisifu au shangwe, kwa utulivu na uthabiti, bila kuanguka katika kiburi wala kukata tamaa, kwani walimjua Yule waliyemwekea tumaini lao (taz. 2 Tim 1:12). Kwa niaba yao wote, tunaweza kukumbuka maneno rahisi ya Ndugu Luc, mtawa mzee na daktari wa jumuiya ya Mama Yetu wa  Atlas.

Hawa walishuhudia maisha yao Algeria
Hawa walishuhudia maisha yao Algeria   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo alieleza kuwa "alipopewa uwezekano wa kuondoka na kujiokoa kutokana na hatari zinazoweza kutokea, kwa gharama ya kuwaacha wagonjwa na marafiki zake, alijibu: “Nataka kukaa nao” (C. Henning - T. Georgeon, Fratel Luc di Tibhirine. Mmonaki, daktari na shahidi, Jiji la Vatican 2025, Utangulizi), na ndivyo alivyofanya. Katika hafla ya Kutangazwa kwao kuwa Mwenyeheri, Papa Francisko alizungumzia kumhusu yeye na wengine wote akisema: "Ushuhuda wao wa ujasiri ni chanzo cha matumaini kwa jumuiya ya Wakatoliki ya Algeria na mbegu ya mazungumzo kwa jamii nzima. Kutangazwa huku kuwa Mwenyeheri kuwe kwa kila mtu msukumo wa kujenga pamoja ulimwengu wa udugu na mshikamano" (8 Desemba 2018).

Kukuza amani na umoja

Na kwa hivyo Papa alifikia  hatua ya tatu ya  tafakari ile ya "kujitolea kwetu kukuza amani na umoja." Kauli mbiu ya ziara hii Papa aliongeza "inatokana na maneno ya Yesu mfufuka: “Amani iwe nanyi!”(taz. Yh 20:21). Katika maandishi yanayopatikana miongoni mwa mosai za Tipasa, tunasoma: “In Deo, pax et concordia sit convivio nostro,” ambayo tunaweza kutafsiri kama: “Katika Mungu, amani na upatanisho vitawale katika maisha yetu pamoja.” Amani na upatanisho vimekuwa sifa za msingi za jumuiya ya Kikristo tangu mwanzo wake (taz. Mdo 2:42-47), kulingana na hamu ya Yesu mwenyewe (taz. Yn 17:23), ambaye alisema: “Kwa hili kila mtu atajua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yh 13:35). Mtakatifu Agostino katika suala hilo, alithibitisha kwamba Kanisa “huzaa watu mbalimbali, lakini ni viungo vya yeye ambaye mwili wake ni” (Mahubiri 192, 2), na Mtakatifu Cyprian aliandika: "Amani yetu na makubaliano yetu ya kidugu ni sadaka  kubwa zaidi kwa Mungu  na watu waliounganishwa katika umoja wa Baba, na wa Mwana, na wa Roho Mtakatifu" (Sala ya Bwana, 23).

Papa akikutana na Jumuiya ya Algeria
Papa akikutana na Jumuiya ya Algeria   (@Vatican Media)

Kanisa ni ishara ya hamu yetu ya umoja

Baba Mtakatifu Leo alikazia kusema kuwa "Ni vizuri, leo, kusikia maneno na mifano mingi kama hiyo ikisikika katika yale tuliyosikia." Kama alivyosema Kardinali Vesco," Kanisa hili ni ishara ya hamu yetu ya amani na umoja. Linaashiria Kanisa la mawe yaliyo hai, ambapo ushirika kati ya Wakristo na Waislamu unafanyika chini ya vazi la Mama Yetu wa Afrika. Hapa, upendo wa kimama wa Lalla Meryem unakusanya kila mtu kama watoto, ndani ya utofauti wetu mwingi, katika hamu yetu ya pamoja ya utu, upendo, haki na amani. Watoto wake wote wana hamu ya kutembea pamoja, kuishi, kusali, kufanya kazi na kuota, kwani imani haijitenganishi, bali inatufungua; inatuunganisha, lakini haileti mkanganyiko; inatuleta karibu zaidi, bila kufanana, na kukuza udugu wa kweli. Hivi ndivyo Monia alivyotuambia. Rakel pia alishirikisha hisia zile zile katika ushuhuda wake kuhusu uzoefu wake katika Shirika la Tlemcen. Katika ulimwengu ambapo mgawanyiko na vita hupanda maumivu na kifo miongoni mwa mataifa, katika jamii, na hata ndani ya familia, uzoefu wenu wa umoja na amani ni ishara ya kulazimisha. Kwa pamoja, mnaeneza udugu na kuhamasisha hamu kubwa ya ushirika na upatanisho kwa ujumbe wenye nguvu na wazi unaobebwa katika urahisi na unyenyekevu.

Papa awahakikishia sala na kuwakabidhi kwa Mama Yetu wa Afrika

Sehemu kubwa ya eneo la nchi hiyo Baba Mtakatifu alisema ni jangwa, "na jangwani, hakuna anayeweza kuishi peke yake. Mazingira ya uadui huondoa dhana zozote za kujitosheleza, zikitukumbusha kwamba sote tunahitajiana, na kwamba tunamhitaji Mungu. Tunapotambua udhaifu wetu, mioyo yetu inakuwa wazi kusaidiana na kumwomba Yeye anayeweza kutoa kile ambacho hakuna nguvu ya kibinadamu inayoweza kuhakikisha: upatanisho wa kina wa mioyo na, pamoja nao, amani ya kweli. Kwa hivyo, Papa Leo XIV aliwahimiza kuendelea na kazi yao nchini Algeria kama jumuiya ya imani iliyoungana na iliyo wazi, kama uwepo hai wa Kanisa, "sakramenti ya wokovu ya ulimwengu wote" (Lumen Gentium, 48). Aliwashukuru kwa yote wanaofanya  kwa maombi yao, upendo wao na ushuhuda wao wa umoja.  Na kwa kuhitimisha aliwahakikishia ukumbusho katika sala zake mbele za Bwana, na kuwakabidhi kwa Maria, Mama Yetu wa Afrika na kuwabariki.

Papa akipokea zawadi kutoka kwa Kardinali Vesco
Papa akipokea zawadi kutoka kwa Kardinali Vesco   (@Vatican Media)

Kardinali Vesco

Kardinali Jean-Paul Vesco, Askofu Mkuu wa Algiers, katika salamu zake alieleze ushirika ambao, katika jengo hilo, unakuwa wito kama mahali pa hija na ibada, ikiwa ni pamoja na Waislamu, ambao wanawakilisha zaidi ya 90% ya wageni, Bahari na jangwa, maji na mchanga, hata hivyo vimeunganishwa na hatima moja ambayo mara nyingi humeza na kuzuia maisha yaliyovunjika ya wahamiaji "wanaotafuta mustakabali bora.  Na mbele ya mnara unaoadhimisha maisha yaliyopotea katika vilindi vya bahari, nje ya Basilika, Papa Leo XIV chini ya mwavuli wa mvua ikiwa inanyesha aliweka shada la maua na kusimama kimya kimya akitafakari.

MKUTANO PAPA JUMUIYA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.

13 Aprili 2026, 19:47