Papa:Katika nyanja za kichungaji,kijami&kisiasa mema hayatoki katika ukandamizaji

Safari ya Yesu inatufunulia kwamba nia ya kupoteza,kujitoa nafsi,si lengo lenyewe,bali ni sharti la kukutana na kuwa karibu.Upendo ni wa kweli tu unapokuwa bila silaha;hauhitaji mzigo mdogo, haujioneshi na kwa upole huhifadhi udhaifu na utupu.Haya yamo katika mahubiri ya Papa Leo XIV wakati wa kuadhimisha Misa ya Crisma kwa mara ya kwanza na kutafakari maana ya utume wa Kikristo,katika Basilika ya Mtakatifu Petro,Aprili 2,2026.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV ameongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe 2 Aprili 2026, kwa kubariki mafuta ya Crisma ikiwa ni Alhamisi Kuu. Ni siku ambayo inajulikana kama ya Mapadre.  Hii ni kwa mara ya kwanza akiwa Papa kubariki Mafuta ya Crisma.  Mafuta aliyobariki ni ya mizeituni ambayo aliyachanganywa na balsamu ili kuweza kutumia kwa  matumizi ya kisakramenti kama vile ubatizo, kipaimara upako wa wagonjwa na katika daraja Takatifu na hivyo yalikuwa ya aina Tatu: Wagonjwa, Wakatekumeni na ya wakfu. Baba Mtakatifu akianza mahubiri yaliyojaa upendo wa kibaba, alisema, “Wapendwa Kaka na dada,  sasa tuko kwenye kizingiti cha Tridium ya Pasaka. Kwa mara nyingine tena, Bwana atatuongoza hadi kilele cha utume wake, ili mateso yake, kifo chake, na ufufuko wake viwe kitovu cha utume wetu. Kiukweli, kile tunachotaka kukiishi tena kina nguvu ya kubadilisha kile ambacho kiburi cha mwanadamu huelekea kukifanya kigumu: utambulisho wetu, nafasi yetu duniani.

Wote waliobatizwa, sisi ni Mwili wa Kristo, uliopakwa mafuta

Papa Leo XIV aliendelea kuelezea kuhusu kuadhimisha kwa mara ya kwanza misa hiyo: “Katika mwaka wangu wa kwanza wa kuongoza Misa ya Crisma kama Askofu wa Roma, ningependa kutafakari nanyi kuhusu utume ambao Mungu anatuweka wakfu kama watu wake. Ni utume wa Kikristo, sawa na wa Yesu, si mwingine. Katika huo kila mtu anashiriki kulingana na wito wake mwenyewe na katika utii wa kibinafsi kwa sauti ya Roho, lakini kamwe bila wengine, kamwe bila kupuuza au kuvunja ushirika! Maaskofu na mapadre, tukipyaisha ahadi zetu, tuko katika huduma ya watu wa kimisionari. Pamoja na wote waliobatizwa, sisi ni Mwili wa Kristo, uliopakwa mafuta na Roho wake wa uhuru na faraja, Roho wa unabii na umoja.

Misa Takatifu katika  Basilika ya Mtakatifu Petro
Misa Takatifu katika Basilika ya Mtakatifu Petro   (@Vatican Media)

Mungu huweka wakfu ili kutuma

Kile ambacho Yesu anapitia katika nyakati za mwisho za utume wake kilitabiliwa na unabii wa Isaya, ambao aliutambulisha katika sinagogi la Nazareti kama Neno kwamba "leo" linatimia (taz. Lk 4:21). Kiukweli, katika saa ya Pasaka, inakuwa wazi kabisa kwamba Mungu huweka wakfu ili kutuma. "Alinituma" (Lk 4:18), Yesu anasema, akielezea harakati inayounganisha Mwili wake kwa maskini, kwa wafungwa, kwa wale wanaopapasa gizani, na kwa waliokandamizwa. Na sisi, washiriki wa Mwili wake, tunauita "Utume." Kanisa lililotumwa, lililosukumwa mbali na nafsi yake, lililowekwa wakfu kwa Mungu katika utumishi wa viumbe vyake: "Kama Baba alivyonituma mimi, nami ninavyowatuma ninyi" (Yh 20:21).

Pasiwepo mahali penye uzio au pango la kujificha

Tunajua kwamba kutumwa kunahusisha, kwanza kabisa, kuacha, yaani, hatari ya kuacha kile kinachojulikana na uhakika ili kuingia katika kipya. Inashangaza kwamba "kwa nguvu ya Roho" (Lk 4:14), ambaye alishuka juu yake baada ya ubatizo wake katika Yordani, Yesu anarudi Galilaya na kuja "Nazareti, ambapo alikuwa amekulia" (Lk 4:16). Ni mahali ambapo lazima aondoke sasa. Anahama "kama kawaida" (Lk, 16), lakini ili kuanzisha kipindi kipya. Sasa lazima aondoke kabisa kutoka kijiji hicho, ili kile kilichochanua huko, Sabato baada ya Sabato, katika kusikiliza Neno la Mungu kwa uaminifu, kiweze kukomaa. Pia atawaita wengine waondoke, wajihatarishe, pasiwemo mahali penye uzio na pasiwepo utambulisho wa pango la kujificha.

Hadhi yetu kama wana na mabinti haiwezi kuondolewa

Baba Mtakatifu Leo XIV aliendelea kuwaelekea waamini kwamba, tunamfuata Yesu, ambaye "hakuhesabu usawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikiliwa, bali alijifanya hana utukufu" (Flp 2:6-7): kila utume huanza na aina hiyo ya utupu ambapo kila kitu huzaliwa upya. Hadhi yetu kama wana na binti wa Mungu haiwezi kuondolewa kwetu, wala kupotea, lakini pia mapenzi, mahali, na uzoefu wa asili ya maisha yetu hayawezi kufutwa. Sisi ni warithi wa mema mengi, na wakati huo huo, kwa mapungufu ya historia ambayo Injili lazima ilete nuru na wokovu, msamaha na uponyaji. Kwa hivyo, hakuna utume bila upatanisho na asili yetu, pamoja na vipaji  na mapungufu ya malezi tuliyopokea; lakini, wakati huo huo, hakuna amani bila kuondoka, hakuna ufahamu bila kujitenga, hakuna furaha bila hatari.

Wakati wa tendo la kupuliza pumzi katika Mafuta ya Crisma
Wakati wa tendo la kupuliza pumzi katika Mafuta ya Crisma   (@Vatican Media)

Sisi ni Mwili wa Kristo ikiwa tutasonga mbele, tukihesabu yaliyopita bila kufungwa nayo: kila kitu hugunduliwa tena na kuzidishwa ikiwa kwanza tutaachiliwa, bila hofu. Ni fumbo la kwanza la utume. Na halipatikani mara moja tu, bali katika kila kuanza upya, na katika kila kutumwa zaidi. Safari ya Yesu inatufunulia kwamba nia ya kupoteza, kujitoa nafsi, si lengo lenyewe, bali ni sharti la kukutana na kuwa karibu. Upendo ni wa kweli tu unapokuwa bila silaha; hauhitaji mzigo mdogo, hakuna kujionyesha, na kwa upole huhifadhi udhaifu na utupu. Tunajitahidi kujitupa katika utume ulio wazi, lakini hakuna "habari njema kwa maskini" (taz. Lk 4:18) ikiwa tutawakaribia kwa ishara za nguvu, wala hakuna ukombozi wa kweli isipokuwa tuwe huru kutokana na umiliki.

Siri ya Pili ya Utume wa Kristo

Hapa tunagusa Siri ya  pili ya utume wa Kikristo. Baada kuacha, kuna  sheria ya kukutana. Tunajua kwamba katika historia yote, utume mara nyingi umepotoshwa na mantiki ya utawala, ambayo, ni ngeni  kabisa karika  njia ya Yesu Kristo. Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alikuwa na uwazi na ujasiri wa kutambua kwamba "katika kifungu hicho ambacho, katika Mwili wa Fumbo, hutuunganisha sisi sote, ingawa hatubebi jukumu la kibinafsi na bila kujibadilisha kwa hukumu ya Mungu, ambaye pekee ndiye anayejua mioyo, hubeba mzigo wa makosa na dhambi za wale waliotutangulia."

Mikitadha ya kichungaji, kijamii na kisiasa

Matokeo yake kwa hiyo sasa ni kipaumbele kukumbuka kwamba si katika nyanja za uchungaji, wala katika nyanja za kijamii na kisiasa, mema yanaweza kutoka katika ukandamizaji. Wamisionari wakubwa ni mashuhuda wa mbinu za utulivu, ambazo njia yao ni kushiriki maisha, huduma isiyo na ubinafsi, kuachana na mkakati wowote wa kuhesabu, mazungumzo, na heshima. Ni njia ya mwili, ambayo huchukua mtindo wa utamadunisho kila wakati. Kiukweli wokovu unaweza kupokelewa na kila mtu tu kwa lugha yake ya mama. "Imekuwaje kila mmoja wetu kuwasikia wengine wakisema kwa lugha yake ya asili?" (Mndo 2:8). Mshangao wa Pentekoste unarudiwa wakati hatudai kudhibiti wakati wa Mungu, bali  tunamwamini Roho Mtakatifu, ambaye "yupo, hata leo, kama ilivyokuwa wakati wa Yesu na Mitume: yupo na yupo kazini, anafika mbele yetu, anafanya kazi kwa bidii na bora zaidi kuliko sisi; si juu yetu kumpanda au kumuamsha, lakini zaidi ya yote kumtambua, kumkaribisha, kumuunga mkono, kutengenezea njia, kumfuata. Yupo na haijawahi kukata tamaa kuhusiana na nyakati zetu; kinyume chake, anatabasamu, anacheza, anapenya, anawekeza, anazunguka, anafika hata mahali ambapo hatungeweza kufikiria.

Wakati wa kuchanganya mafuta ya Crisma
Wakati wa kuchanganya mafuta ya Crisma   (@Vatican Media)

Kuheshimu fumbo la kila mtu

Ili kuanzisha maelewano haya na yasiyoonekana, lazima tufike mahali tunapotumwa kwa urahisi, tukiheshimu fumbo ambalo kila mtu na kila jumuiya  huleta. Sisi ni wageni: kama maaskofu, kama makuhani, kama wanaume na wanawake watawa, kama Wakristo. Ili kuwa mwenyeji, kiukweli, lazima tujifunze kuwa mwenyeji. Hata maeneo ambayo uzushi unaonekana kuwa wa hali ya juu zaidi si nchi za ushindi, au ukombozi: "Tamaduni mpya zinaendelea kuzalishwa katika sehemu hizi kubwa za kibinadamu ambapo Mkristo hajazoea tena kuwa mhamasishaji au kuzalisha maana,lakini hupokea kutoka kwao lugha zingine, alama, ujumbe, na dhana zinazotoa maelekezo mapya ya maisha, mara nyingi kinyume na Injili ya Yesu. […] Ni lazima  kufikia mahali ambapo masimulizi na dhana mpya zinaundwa, ili kufikia kiini cha ndani kabisa cha roho ya miji kwa Neno la Yesu." Hili hutokea tu ikiwa tunatembea pamoja Kanisani, ikiwa tume zetu si tukio la kishujaa kwa mtu, bali ni ushuhuda hai wa Mwili wenye viungo vingi.

Sehemu ya Tatu:Uwezekano wa kuelewa wa kukataa utume wa Yesu

Pia kuna sehemu ya tatu, labda yenye msimamo mkali zaidi, ya utume wa  Kikristo. Uwezekano mkubwa wa kutoelewana na kukataliwa tayari unaonekana katika majibu ya vurugu ya watu wa Nazareti kwa maneno ya Yesu: "Waliposikia haya, wote waliokuwa katika sinagogi wakajaa ghadhabu. Wakasimama, wakamtoa nje ya mji, wakampeleka hadi ukingo wa kilima ambacho mji wao ulijengwa juu yake, ili wamtupe chini kwenye mwamba" (Lk 4:28-29). Ingawa usomaji wa kiliturujia uliondoa sehemu hii, kile tunachojiandaa kusherehekea jioni hii kinatulazimisha tusitoroke, bali "kupita" katika kesi hiyo, kama Yesu, ambaye, "akipita katikati yao, akaenda zake" (Lk 4:30).

Mafuta ya Crisma
Mafuta ya Crisma   (@Vatican Media)

Msalaba ni sehemu ya utume.Ufufuko wa kufanya mazoezi

Msalaba ni sehemu ya utume: kutumwa kunakuwa kuchungu zaidi na kutisha, lakini pia ni bure na usumbufu zaidi. Uvamizi wa kibeberu wa ulimwengu kisha huingiliwa kutoka ndani, vurugu ambazo hadi sasa zimekuwa sheria hufichuliwa. Masiha  maskini, aliyefungwa, aliyekataliwa, huanguka katika giza la kifo, lakini kwa kufanya hivyo huleta kiumbe kipya kwenye nuru. Tunapewa pia ufufuko upi ili tupate wakati, tukiwa huru kutoka katika mtazamo wa kujilinda, tunashuka katika utumishi kama mbegu ardhini! Katika maisha, tunaweza kupitia hali ambazo kila kitu kinaonekana kumalizika. Kisha tunajiuliza kama utume umekuwa bure. Ni kweli: tofauti na Yesu, pia tunapitia kushindwa kunategemea mapungufu yetu wenyewe au ya wengine, mara nyingi kutokana na msongamano wa majukumu, wa mwanga na vivuli. Lakini tunaweza kufanya tumaini kuwa letu wenyewe.

Ushuhuda wa Askofu Oscar Romero

Papa Leo XIV alikumbuka shujaa wa Kikristo na kumtolea mfano, Askofu Mkuu wa San Salvador, aliyeuawa akiwa altareni mnamo mwaka 1980. Papa alisema: “Nakumbuka mmoja ambaye alinipendeza sana. Mwezi mmoja kabla ya kifo chake, katika Mafungo yake ya Kiroho, Askofu Mtakatifu Óscar  Romero aliandika: "Balozi wa Costa Rica alinionya kuhusu hatari iliyo karibu Juma  hili... Hali zisizotarajiwa zitakabiliwa kwa neema ya Mungu. Yesu Kristo aliwasaidia mashahidi, na ikihitajika, nitamhisi karibu sana nitakapomkabidhi pumzi yangu ya mwisho. Lakini, zaidi ya dakika ya mwisho ya maisha, jambo muhimu ni kumpa Yeye maisha yangu yote na kuishi kwa ajili yake... Inatosha kwangu, kuwa na furaha na ujasiri, kujua kwa uhakika kwamba ndani yake kuna maisha yangu na kifo changu; kwamba, licha ya dhambi zangu, nimeweka tumaini langu Kwake na sitachanganyikiwa, na wengine wataendelea, kwa hekima na utakatifu zaidi, kazi kwa ajili ya Kanisa na kwa ajili ya nchi."

Msafara wa kupeleka mafuta ili yabarikiwe
Msafara wa kupeleka mafuta ili yabarikiwe   (@Vatican Media)

Watakatifu wanafanya historia:Watu wapya na si waathirika ni mashuhuda

Dada na Kaka wapendwa, watakatifu wanaandika historia. Huu ndio ujumbe wa Ufunuo. "Neema na iwe kwenu na amani kutoka kwa Yesu Kristo, shahidi mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa wafu, na mtawala wa wafalme wa dunia" (Uf 1:5). Salamu hii inafupisha safari ya Yesu katika ulimwengu uliopasuka kati ya nguvu za uharibifu. Ndani yake, watu wapya wanatokea, si waathiriwa, bali mashahidi. Katika saa hii ya giza ya historia, Mungu amefurahi kututuma kueneza harufu ya Kristo ambapo harufu ya kifo inatawala. Tupyaishe "ndiyo" yetu kwa utume huu unaotuita kwenye umoja na kuleta amani. Ndiyo, tuko hapa! Tushinde hisia ya kutokuwa na nguvu na hofu! Tunatangaza kifo chako, Bwana, tunatangaza ufufuo wako, tukingojea kuja kwako,” Papa Leo alihitimisha. 

Wakati wa mageuzi Altareni
Wakati wa mageuzi Altareni   (@VATICAN MEDIA)

Katika Kanisa Kuu la Vatican lilijaa waamini, Makardinali karibia arobaini hivi, Maaskofu wakuu, Maaskofu, na mapadre wengi walikusanyika pamoja na Papa Leo XIV. Makadinali wanne waliokaribia altreni kwa ajili ya Sala ya Ekaristi walikuwa: Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Makardinali na Kardinali Leonardo Sandri, Makamu Dekano, Kardinali Baldo Reina, Makamu wa Papa Jimbo Kuu la Roma na Kardinali Mauro Gambetti, Mkuu wa Basilika ya Mtakatifu Petro.

Wakati wa kubariki mafuta hayo, ulikuwa wa kugusa moyo wakati Papa Leo XIV alipopulizia kwenye chombo (ampoule) chenye mafuta ya Crisma, akikumbusha pumzi ya Roho Mtakatifu.

Papa akisali mbele ya Sanamu ya Bikira Maria
Papa akisali mbele ya Sanamu ya Bikira Maria   (@Vatican Media)

Mwishoni mwa Misa, Papa alisimama kusali mbele ya sanamu ya mbao ya Bikira wa Montserrat, inayojulikana kama "La Moreneta," iliyowekwa karibu na madhabahu.

Papa akiwabariki katikati ya Kanisa Kuu
Papa akiwabariki katikati ya Kanisa Kuu   (@Vatican Media)

Kisha alitembea chini  katikati  ya Kanisa Kuu, akiwasalimia na kuwabariki waliokuwepo.

Misa ya kubariki Mafuta katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.

 

02 Aprili 2026, 11:10