Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru na kuwapongeza wale wote walioshiriki katika kuwaandaa na hatimaye, wanamichezo wa Vatican kushiriki kikamilifu na hivyo kutoa ushuhuda wa uzuri wa michezo. Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru na kuwapongeza wale wote walioshiriki katika kuwaandaa na hatimaye, wanamichezo wa Vatican kushiriki kikamilifu na hivyo kutoa ushuhuda wa uzuri wa michezo.  (ANSA)

Papa Leo XIV Mashindano ya Olympiki 2026: Ujumbe wa Kibinadamu, Kitamaduni na Kiroho

Michezo ni lugha, simulizi inayomwilishwa katika matendo, hali ya kuchoka, matarajio, maanguko na hatimaye kuweza kusimama tena na kuendelea na safari. Wanamichezo hawa wameonesha miondoko ya mwili, historia na sadaka, nidhamu pamoja na ukakamavu na kwamba, mapungufu ya kibinadamu yanaweza kuwa ni mahali pa ufunuo na wala si kikwazo kwa mwanamichezo, lakini hali inayoweza kuleta mabadiliko katika maboresho ya maisha ya mwanamichezo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Michezo ya Olympiki kuanzia tarehe 6 Februari hadi tarehe 22 Februari 2026 na tena kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 15 Machi 2026 imefanyika huko Milano na Cortina, Kaskazini mwa Italia, Baba Mtakatifu Leo wa XIV amewatumia barua washiriki wa michezo hii huku akionesha: Thamani ya michezo: Michezo na ujenzi wa amani; tunu msingi za michezo katika makuzi na majiundo; Mchezo, shule ya maisha na ya kisasa; Michezo na maendeleo binafsi.Aligusia pia mambo yanayohatarisha tunu msingi za michezo; Mashindano na utamaduni wa watu kukutana; Michezo, Mahusiano na mang’amuzi; sanjari na Mpango mkakati wa michezo kwa ajili ya kuwa na maisha tele! Kipindi chote cha mashindano ya Olimpiki, vita na misigano yote ya kisiasa na kijamii ilipaswa kusitishwa ili kutoa fursa kwa wananchi kufurahia michezo na hivyo michezo katika muktadha huu ikawa ni fursa ya kujenga na kudumisha amani; ukuaji wa udugu wa kibinadamu, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, vita, kinzani na mipasuko ni dalili za kushindwa kwa ubinadamu.

Papa Leo XIV: Michezo ni shule ya haki, amani, nidhamu na utu
Papa Leo XIV: Michezo ni shule ya haki, amani, nidhamu na utu   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Dunia ina kiu ya amani kumbe, kuna haja ya kutumia nyenzo mbalimbali zitakazo saidia kusitisha matumizi mabaya ya madaraka na hivyo kujikita katika utawala wa haki na sheria. Kuna haja ya kuhakikisha kwamba, tunu msingi za michezo zinatumika katika makuzi na majiundo ili kuweza kuwa na maisha tele pamoja na utimilifu wake. Rej. Yn 10:10. Mama Kanisa hana budi kutekeleza dhamana na utume wake hapa ulimwenguni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu katika michezo kama anavyosema Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa kuhusu utaratibu kwa wanariadha: “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate. Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika.” 1Kor 9:24-25. Hiki ni kielelezo cha mashindano ya kiroho; na kwamba Binadamu ni umoja wa mwili, roho na nafsi na hivyo Mama Kanisa anakazia umuhimu wa michezo katika maisha ya mwanadamu kama mambo muhimu sana katika kuhubiri na kufundisha.

Michezo ni shule ya upendo mshikamano
Michezo ni shule ya upendo mshikamano   (@VATICAN MEDIA)

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Michezo ya Olympiki huko Milano na Cortina, Kaskazini mwa Italia, iliyohimishwa hivi karibuni, Baba Mtakatifu Leo wa XIV Alhamisi tarehe 9 Aprili 2026 amekutana na kuzungumza na viongozi na wanamichezo wa Vatican “Athletica Vatican waliokuwa wamesindikizana na viongozi wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu. Amesema, mashindano haya ya Michezo ya Olympiki kwa mwaka 2026 yametoa ujumbe wa kibinadamu, kitamaduni na kiroho. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wale wote walioshiriki katika kuwaandaa na hatimaye, wanamichezo wa Vatican kushiriki kikamilifu na hivyo kutoa ushuhuda wa uzuri wa michezo. Kwa hakika michezo ni lugha, simulizi inayomwilishwa katika matendo, hali ya kuchoka, matarajio, maanguko na hatimaye kuweza tena kusimama na kuendelea na safari. Wakati wa mashindano, wanamichezo hawa wameonesha miondoko ya mwili, historia na sadaka, nidhamu pamoja na ukakamavu na kwamba, mapungufu ya kibinadamu yanaweza kuwa ni mahali pa ufunuo na wala si kikwazo kwa mwanamichezo, lakini hali inayoweza kuleta mabadiliko katika maboresho ya maisha ya mwanamichezo. Kwa hakika anasema, Baba Mtakatifu Leo XIV kwamba, wanamichezo hawa wamekuwa ni vitabu hai vinavyoleta hamasa kwa watu wengi.

Katika michezo kuna majaribu pia
Katika michezo kuna majaribu pia   (@Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, wanamichezo hawa wameonesha kwamba, mafanikio yao katika michezo yanapata chimbuko lake kutoka katika familia, timu pamoja na mazoezi ya siku nying, shinikizo pamoja na upweke chanya. Mara nyingi ni katika nyakati kama hizi ambapo Mwenyezi Mungu hujifunua, kama mtunga Zaburi alivyoimba: “Umezifanyia njia hatua zangu, miguu yangu haikuteleza” (Zab 17:36; Tafsiri ya Biblia Takatifu, TEC.) Michezo, kwa kweli, inachangia kukomaa kwa tabia, inahitaji hali thabiti ya kiroho na ni aina ya elimu inayozaa matunda. Michezo huwafunza watu kufahamu miili yao bila kuiabudu; kudhibiti hisia; kushindana bila kupoteza hisia za udugu wa kibinadamu, kukubali kushindwa bila kukata tamaa na hatimaye, ushindi bila kiburi. Michezo inakuwa ni ya kibinadamu pale inapojikita katika uaminifu, inapokuwa ni shule ya maisha na mahali pa kukuza karama na vipaji; mahali pa kujifunza kuboresha uhusiano, bila kulewa na zawadi zinazotolewa, bali kwa kuheshimiana na kuthaminiana katika furaha shirikishi na kwamba, huu ndio uzima tele. Rej Yn 10:10.

Jengeni na kudumisha michezo ya kibinadamu
Jengeni na kudumisha michezo ya kibinadamu   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, katika Ulimwengu mamboleo unaogubikwa na ubaguzi, mashindano, na migogoro ambayo inakuwa ni chimbuko la vita vinavyosababisha maafa, majitoleo yao yanabeba thamani kubwa kwani michezo inageuka kuwa ni uwanja wa watu kukutana, sio kipimo cha nguvu lakini mahali pa kufanya mazoezi ya ujenzi wa uhusiano, amani na utulivu kwa kuvunja mantiki ya vurugu na ghasia, ili kukuza na kujenga mantiki ya watu kukutana. Katika michezo pia kuna majaribu yanayoweza kupelekea matumizi haramu ya dawa za kuongeza nguvu. Kuna majaribu ya kupata faida na hivyo michezo hugeuzwa kuwa kama soko na wanamichezo kuwa ni bidhaa. Kuna majaribu ya kuvutia yanayowafanya wanamichezo kuwa ni vivutio, hali inayopunguza thamani na utu wa wanamichezo na hivyo kuonekana kuwa ni picha au namba. Kinyume cha yote haya, wanamichezo wamekuwa ni mashuhuda makini wa ulimwengu unaosimikwa katika uaminifu; ulimwengu bora wa watu kuishi. Wanamichezo wanaweza kushinda bila kudhalilishana katika medani mbalimbali za maisha, kwa kujenga na kudumisha uhusiano mwema wa kijamii.

Msalaba wa wana michezo
Msalaba wa wana michezo

Baba Mtakatifu amewapongeza wanamichezo kwa ushuhuda wa uaminifu na uzuri wa kuishi ulimwenguni, kwa kushindana bila kumezwa na chuki; kwa kushindana bila ya kudhalilishana; kwa kupoteza bila kujipoteza wenyewe, hali ambayo inapaswa pia kutumika katika medani mbalimbali za maisha mintarafu ujenzi wa uhusiano kati ya watu, ili kuifanya michezo kuwa ni maabara ya ubinadamu uliopatanishwa, ambapo utofauti sio tishio, lakini ni utajiri. Katika enzi ya changamoto kubwa za hali ya hewa, Michezo hii pia inawakumbusha watu wa Mungu kuhusu uhusiano kati ya michezo, asili na wajibu wa kutunza mazingira nyumba ya wote. Rej. Laudato si’, 3. Wanamichezo wametumia fursa hii kutafakari Msalaba wa Wanamichezo: Msalaba wa Olimpiki na Walemavu ambao, kutoka katika Michezo ya London 2012 hadi Michezo ya Milano-Cortina, umekusanya pamoja: Sala, matarajio na matumaini, hofu na mateso ya watu ambao, katika kila umri, wanashiriki uzoefu wao wa michezo. Hii imekuwa ni fursa kwa wanamichezo kupyaisha hamu yao ya kujitolea katika shughuli mbalimbali. Mwishoni, Baba Mtakatifu Leo XIV amewashukuru wote kwa sadaka na majitoleo yao. Anamwomba kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II, kwamba Kristo Yesu “Mwanamichezo wa kweli wa Mungu aweze kuwatia moyo kila mmoja wao katika changamoto zinazozidi maisha adili na awakirimie nguvu ya kuzikumbatia kwa shauku.” Baba Mtakatifu Leo XIV amehitimisha hotuba yake kwa kuwasindikiza wanamichezo kwa baraka zake za kitume: kuendelea kuhakikisha kwamba mtu anabakia kuwa kitovu cha michezo katika usemi wake wote.

Papa Michezo
09 Aprili 2026, 15:35